The House of Favourite Newspapers

Baada ya Kufungiwa na Kufunguliwa, Roma Anena Haya

Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’

MACHI 1, mwaka huu ni mwezi usiosahaulika katika maisha ya Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ katika Muziki wa Hip Hop Bongo mara baada ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza kumfungia kutojihusisha na shughuli zozote za muziki kwa muda wa miezi sita baada ya kukaidi kufanya marekebisho wimbo wake wa Kibamia.

 

Hata hivyo, Machi 29, mwaka huu, Waziri Harisson Mwakyembe alitangaza kumfutia adhabu hiyo baada ya kukamilisha taratibu za kujisajili Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kukubali wimbo wake usiendelee kupigwa katika vituo vya redio na TV.

 

Ukiachilia hayo, tukio jingine ambalo Roma hatalisahau ni siku moja baada ya kufunguliwa kufanya muziki yaani Machi 28, mkewe, Nancy alijifungua mtoto wa kike na kuongeza furaha katika familia mbapo hadi sasa ana watoto wawili akiwemo wa kwanza ambaye ni wa kiume anayeitwa Ivan. Mikito Nusu Nusu imefanya ‘exclusive interview’ na Roma baada ya kupitia yote hayo na katika makala hii fupi anafunguka zaidi;

 

Mikito: Hongera kwanza kwa kupata mtoto wa kike, unaweza kutuambia anaitwa nani?

Roma: (Anaanza kwa kucheka) Asante sana, mwanangu nimempa jina la Ivan.

Mikito: Ilikuwaje mpaka ukamuita jina hilo maana linafanana na la mtoto wa rapa kutoka Marekani, Jay Z ambaye mtoto wake anaitwa Blue Ivy?

Roma: Ni kweli unayosema lakini nilianza kwanza kuangalia jina la mtoto wangu wa kwanza anaitwa Ivan nikaona na huyu wa kike nimpe jina lenye kuanzia na Iv ndipo nikalipatata Ivy.

Mikito: Ivan ulimuimbia wimbo, huyu naye vipi?

Roma: Watu wengi wamekuwa wakitaka nifanye hivyo na hata mke wangu naye aliniambia hilo, Ivy ni mtoto wa kike lazima naye nitamuimba kwani nikimuimba mwanamke huwa nawakilisha wanawake wengi.

 

Mikito: Tumeona watoto wengi wa mastaa wakila mashavu ya ubalozi katika makampuni makubwa vipi wa kwako?

Roma: (anacheka tena..) Duh! Kwangu bado aisee, baba yake mwenyewe nina miaka kumi sijawahi kupata dili lolote la makampuni makubwa.

Mikito: Ngoma mpya vipi?

 

Roma: Nipo katika michakato hiyo kwani ni muda mrefu hajasikika Roma wala Rostam na kama unavyojua Kibamia haipo tena hivyo najipanga.

Mikito: Umekuwa ukiongelewa sana kuwa umebadilika kutoka kuimba nyimbo za harakati mpaka kuimba Kibamia hili limekaaje?

Roma: Ujue wakati mwingine unaweza kuwafuata wanachotaka mashabiki ukajikuta umepotea. Kuna wakati niliimba sana nyimbo za harakati wakanisema ‘ohh Roma habadiliki kila siku yuleyule’ nikaamua nianze kujichanganya nawaletea za mapenzi, wameanza kusema tena.

 

Mikito: Muziki sasa unaonekana kama umehamia kwenye kiki, unaongeleaje hili?

Roma: Huko sitaki kuingilia sana kwani ninaangalia katika muziki wangu sanasana nachoweza kusema ni vema mtu ukajipima uwezo wako kiakili na kifikra kabla ya kufanya kiki za ajabu.

MAKALA: ANDREW CARLOS

Comments are closed.