BAADA YA KUOA BINTI WA KIBONGO…MZUNGU AUAWA KIKATILI BONGO!

KUSEMA kweli kuna wakati Dunia Haina Huruma! Ndivyo ambavyo unaweza kusema baada ya Familia ya Mzee Boniphace Raphael Umela wa Mfuru, Mkuranga mkoani Pwani kuvamiwa na kundi la watu wanaosadikika kuwa ni majambazi na kuwasababishia majeruhi na kifo cha mtu mmoja mwenye Uraia wa Sweden.  

 

Raia huyo wa kigeni aliyepote­za maisha katika tukio hilo la kikatili amefahamika kwa jina la Joseph Kiss ‘Papy’ mwenye umri wa miaka 68 ambaye ni mume wa binti wa Kibongo aitwaye Juliana Boniphace Umela.

 

KISA CHA UVAMIZI

Chanzo chetu kilidai kuwa, tangu mzungu huyo aingie nchini na kuishi na binti huyo kama mume na mke na makazi yao yakiwa mkoani Pwani, watu wengi wamekuwa wakiamini kuwa, familia hiyo ina fedha jambo am­balo linatajwa kuwa limechangia majambazi hao kufanya uvamizi huo wa kinyama. “Tangu wafike wamekuwa wakionekana wakipiga picha sehemu mbalimbali za fukwe na maeneo ya starehe nadhani watu kuona hivyo wakajua wana fedha,” chanzo kilidai.

BINTI MBONGO, PAPY WALIVY­OKUTANA

Juliana na mume wake ambaye kwa sasa ni marehemu waliku­tana nchini Sweden miaka kad­haa iliyopita na kuamua kurudi Tanzania ambako walifunga ndoa mwaka mmoja uliopita. Baada ya hapo Papy alianza kufanya jitihada za kuhamisha makazi kutoka Sweden kuja nchini lakini Mungu hakupanga hilo likamilike kwa sababu hadi anapoteza maisha hakuwa ame­kamilisha mpango wake.

TUKIO LILIVYOTOKEA

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Desemba 20, mwaka jana majira ya saa sita usiku nyumbani kwa wazazi wa Juliana ambako yeye na mumewe pia walikuwa wakiishi. Chanzo kililiambia gazeti hili kuwa, majambazi hao wa­naokadiriwa kuwa zaidi ya kumi walivamia nyumba hiyo wakiwa na silaha mbalimbali zikiwemo bunduki.

MAMA WA JULIANA AELEZA

Mama mzazi wa Juliana am­baye ni mkwe wa marehemu Papy aitwaye Sarah aliliambia gazeti hili kuwa: “Walipofika walivunja mlango kisha kuingia ndani na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba alichokuwa mkwe wangu, am­bapo baada ya muda nilianza kusikika kelele kama wanalum­bana.

 

“Mimi wakati huo nilikuwa sebuleni ghafla nikasikia kama makelele ya watu wanaongea nje nikaamua kwenda kuchun­gulia ni nini; kumbe walikuwa wanavunja mlango. “Sasa wakati nipo kwenye korido nikashangaa kumuona mtu kashika bunduki na tochi, niliogopa sana.

 

“Akanisukuma na moja kwa moja akawa anaelekea kwenye chumba cha marehemu mkwe wangu, nikamuuliza wewe nani? Hakunijibu. “Ikabidi nikimbie hadi chumbani kwa mume wangu kumuambia nimeona watu wengi wameingia ndani. Kipindi naendelea kuongea naye na kutaka kupiga kelele majambazi wengine walikuja na kunipiga panga la kichwani.

Nikawa nimeanguka, ma­jambazi waliokuwa chumbani kwa mkwe wangu walien­delea kumshambulia kwa kumcharanga mapanga huku wakimwambia wanataka hela. “Wale wengine waliokuwa chumbani kwetu mimi na mume wangu waliendelea kumpiga na mapanga baba Juliana maeneo ya miguuni naye walikuwa wakimwambia atoe fedha.

 

“Tukawaambia sisi hatuna hela, walikaa pale kama nusu saa hivi wakaiba TV, kuna TV nyingine kubwa iliwashinda kwa sababu ni nzito. “Ndiyo wakaanza kusaka vitu sehemu mbalimbali chum­bani wakafanikiwa kuiba vitu vya Juliana ikiwemo dhahabu na laptop na baadhi ya vitu vya Papy ambavyo alikuwa amevileta kwa ajili ya kuanza maisha hapa nchini.” Alisema mama huyo.

 

MAJAMBAZI WAACHA BUN­DUKI

Aliongeza kuwa, baada ya kufanya unyama huo wa kuti­sha na kusikitisha majambazi hayo yalitoweka huku yakitele­keza moja ya silaha ya moto ambayo hakuitambua ilikuwa ni ya aina gani. “Ikabidi tutoke na gari yetu na kuwapigia simu polisi kuelekea Hospitali ya Vikindu tukaambiwa tuende Hospitali ya Temeke, tulipofika pale tuliambiwa kuwa mkwe wangu alikuwa ameshafariki lakini mume wangu alipewa kitanda na kupewa huduma lakini ilishindikana, akahamishiwa Moi mpaka sasa anaendelea na matibabu.

 

“Hii ni wiki ya tatu mwili wa mzungu bado hatujajua mua­faka wake kwa sababu wote tulichanganyikiwa, tulichelewa kwenda ubalozini kukamilisha utaratibu kwa kuwa si raia wa hapa. “Nafikiri wiki ijayo tunaweza kukamilisha na kujua nini ki­fanyike kama tunasafirisha au tunazika hapa,” alisema mama mkwe huyo wa marehemu Papy.

 

MWENYEKITI ASIMULIA

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mfuru, Hashimu Juma alisema kuwa tukio hilo limetokea na kila kitu kinachoendelea wameliachia Jeshi la Polisi kwa kuwa ndiyo wenye mam­laka.

 

“Tukio hili lilitokea ma­jira ya saa sita na dakika ishirini usiku ambapo taarifa nilizipata nikiwa nyumbani kwangu, kwa kuchelewa lakini nilijitahidi kuwahi eneo la tukio ingawa sikufanikiwa kuwakuta walikuwa wameshakimbizwa hospitali. “Na kwa taarifa nilizozipata ni kwamba majambazi wali­vamia nyumbani kwa mzee Umela na kuwajeruhi sana lakini yule mzungu pamoja na mzee Umela ndiyo walidhurika vibaya kwa kuwa walikuwa wakihitaji hela kutoka kwao.

 

“Lakini hawakupata hizo hela hata baada ya kupekuwa ndani humo ila walifanikiwa kupata baadhi ya vitu kama vile kompyuta na vitu vya dha­habu, basi kesho yake nilifika tena eneo la tukio nikakutana na polisi na kwa kuwa mimi nipo katika kamati ya ulinzi na usalama wakanikabidhi nyumba hiyo niangalie kwa muda ambao wenyewe wana­patiwa matibabu hadi wataka­porudi lakini mpaka sasa nimeshawakabidhi wenyewe na taratibu zingine ziendelee,” alisema mwenyekiti.

 

DIWANI AFUNGUKA

Kwa upande wake Diwani wa eneo hilo Nassoro Chuma alikiri kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha na kusema kwamba tuviachie vyombo vya usalama viendelee kufanya kazi ya uchunguzi juu ya tukio hilo.

 

KAMANDA ANENA

Naye Kamanda wa Kanda Maalumu ya ya Kipolisi Kibiti, Onesmo Lyanga alipotafutwa ili athibitishe tukio hilo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza: “Kama unavyoona tukio hilo ni la muda mrefu nilishalizun­gumzia na kama huyo raia wa kigeni bado hajazikwa hadi hivi sasa nadhani ni taratibu za kibalozi ndizo bado hazija­kamilika.”

Stori: Shamuma Awadhi na Neema Adrian,Dar

INATISHA! MZUNGU Auawa Kikatili Baada Ya Kuoa Binti Wa Kibongo

Loading...

Toa comment