The House of Favourite Newspapers

Baada ya Kuruhusu Wimbo wa Nay upigwe, Mastaa Wampa Big Up Magufuli

Rais Magufuli.

Na GLADNESS MALLYA| RISASI MCHANGANYIKO| HABARI

DAR ES SALAAM: Saa chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kulitaka Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam kumuachia huru, msanii Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ aliyekamatwa kwa tuhuma za ukosefu wa maadili katika wimbo wake mpya wa Wapo, wasanii mbalimbali wameibuka na kumpa big up kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya agizo hilo la Rais Magufuli kutolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, baadhi ya wasanii hao wamempongeza kwa hatua hiyo kwani ameona umuhimu uliopo katika sanaa ya muziki. Mwanaisha Said ‘Dayna Nyange’ ambaye ni staa wa Bongo Fleva, alisema anamshukuru rais kutoa agizo la Nay kuwa huru, kwani msanii huyo ni kaka yake na alikuwa na huzuni sana kutokana na kushikiliwa kwake.

Dayna.

“Binadamu yeyote ni bora akose yote lakini awe huru, nimefurahi sana Nay kuwa huru ninachoweza kumwambia ni kumkaribisha ili tuendeleze harakati kama kawaida,” alisema Dayna.

 

Bob Junior akwa na mdau wa muziki wa Bongo Fleva.

Kwa upande wa Raheem Rummy Nanji ‘Bob Junior’ alisema anajisikia faraja kwa kuwa rais ametambua thamani ya Wanamuziki wa Bongo Fleva, kwani kitendo cha kuagiza Nay aachiwe huru na wimbo wake kupigwa kwenye vyombo vya habari inaonesha yupo pamoja nao.

Naye Amini Mwinyimkuu ‘Amini’ alisema ameona heri na rais amefanya kitu kizuri kuruhusu wimbo huo upigwe na Mbongo Fleva huyo kuachiwa huru.

Nay wa Mitego ambaye anatajwa kuwa mtukutu kutokana na tabia yake ya kutoa nyimbo zenye maneno makali na wakati mwingine yenye kuudhi, alikamatwa Jumamosi iliyopita akiwa katika shoo huko Turiani mkoani Morogoro kabla ya Jumapili yake kusafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam.

Jumatatu asubuhi, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) liliamuru kuufungia wimbo huo, likitaka kutotumika kwa namna yoyote hadi hapo itapotoa maelezo zaidi, kwa kile kilichosemwa ni kukosekana kwa maadili ndani ya wimbo huo.

Lakini mchana wa siku hiyohiyo (Jumatatu) Rais Magufuli, kupitia kwa Waziri Mwakyembe alitaka kuachiliwa kwa msanii huyo, sambamba na kuuruhusu wimbo huo kuendelea kupigwa kama ulivyo katika vyombo vyote vya habari

Comments are closed.