Baada ya Maajabu ya Royal Tour, Dkt. Samia Aja na Maajabu Mengine ya Utalii Kusini
Kwa lugha ya Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Tabora, Mzee Aggrey Mwanri, tunaweza kusema ardhi ya Kusini mwa Tanzania “inalia” kwa jinsi inavyotifuliwa kiujenzi wakati huu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyotekeleza miradi mikubwa ya kiutalii kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii na ukanda huo.
Zaidi ya Bilioni 300 zinatumika kupitia Mradi wa Kuendeleza Utalii Kusini (Regrow) ukifadhiliwa na Serikali na Benki ya Dunia ambapo mjini Iringa leo, eneo la Kihesa-Kilolo, wabunge na viongozi waandamizi wa Serikali wamejionea ujenzi wa majengo ya kisasa kwa ajili ya utalii na utafiti wa wanyamapori yanayoendelea kwa kasi ili kuanza kutoa huduma mapema Januari, 2025.
“Miradi hii ni mageuzi makubwa ya Dkt. Samia ambaye sasa anaifungua Kusini kiutalii,” anasema Mhe. Timotheo Mzava, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii baada ya kutembelea eneo hilo leo Jumamosi Septemba 7, 2024, akiungwa mkono na Waziri wa Utalii, Mhe Pindi Chana aliyesisitiza kuwa miradi hiyo itakamilika kwa wakati:
“Kazi hii njema ya Rais wetu Dkt. Samia sisi tunaisimamia usiku na mchana kuhakikisha miundombinu hii inakamilika kwa wakati na ubora,” alisema.
“Filamu ya Royal Tour imeifungua nchi, uwekezaji huu wa Kusini mwa nchi yetu ni wa kimkakati kwani watalii sasa watakaa zaidi nchini kwa kuwa na maeneo mengi ya kuvinjari nchini,” aliongeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi.
Kama ambavyo Mkutano wa Dunia, the World Travel and Tourism Summit 2022, Riyadhi Saudi Arabia, ulivyoazimia: “The future of tourism is service and experience,” Serikali ya Dkt. Samia inaifungua Kusini kimiundombinu na kuongeza maeneo zaidi ya dunia kuja kuvinjari.
“Sisi tumetenga maeneo mengi hapa. Mkoa tumepata wawekezaji mpaka wapo wanaokuja kujenga uwanja wa gofu,” anasisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba naye akiwa amefika eneo la Kihesa-Kilolo leo kujionea “ardhi ikilia” chini ya mageuzi ya Dkt. Samia kupitia Mradi wa Regrow.
“Hatari sana” kwa maneno ya muwekezaji Leonardo, kupitia Regrow kunajengwa viwanja vya ndege, majengo ya kushukia na kupandisha abiria, majumba ya malazi, barabara na upanuzi wa maeneo ya kiutalii na utafiti lakini pia wananchi maeneo ya karibu wanawezeshwa kushiriki katika mnyororo wa thamani wa utalii hasa kina mama na vijana.