visa

BAADA YA MUMEWE KUFARIKI BIBI YAMKUTA MAZITO

UKIONA mtu mzima analia, basi ujue kuna jambo! Haya ni maneno yanayopatikana kwenye wimbo wa Kilio cha Mtu mzima ulioimbwa miaka hiyo na Msondo Ngoma Music Band ukimaanisha kwamba ukimuona mtu mzima analia, basi ujue yamemfika mazito. 

 

Hicho ndicho kilichomtokea bibi Mary Njogela, mkazi wa TPDC-Mikocheni jijini Dar, ambaye amejikuta akiangua kilio kizito, akidai kudhulumiwa nyumba na watoto wa marehemu mumewe, Said Hamza ambazo walishirikiana kujenga na kuacha wosia (will) kuwa yeye ndiye mmiliki halali.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi akiwa kwenye nyumba ambayo amepewa kama msaada na msamaria mwema ambaye ni mke wa Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, bibi huyo alisema kuwa aliishi na mumewe huyo yapata miaka ishirini ndani ya ndoa. Alisema kuwa, katika maisha yao walifanikiwa kufungua kampuni iliyojulikana kwa jina la General Guard and Cleaning na kujenga nyumba mbili za kifahari, moja ikiwa Mikocheni B na nyingine Msasani, zote jijini Dar.

 

“Niliishi na mume wangu kwa raha mustarehe kwa miaka ishirini na nne ndani ya ndoa na tulifanikiwa kufungua Kampuni ya General Guard and Cleaning kwa kushirikiana kwa sababu wote tulikuwa tunafanya biashara na nikawa na hisa zangu pale.

 

“Maisha yalikwenda vizuri mno na tukajaliwa kujenga nyumba mbili; moja ipo maeneo ya Msasani na nyingine Mikocheni B ambapo ndipo tulipokuwa tukiishi mimi na mume wangu. “Enzi za uhai wake, mume wangu alinirithisha nyumba ya Mikocheni B na vielelezo vipo, lakini baadaye Mungu alimpenda zaidi akafariki dunia na kuniacha mimi nikiendelea kuishi pale.

“Mume wangu alikuwa na watoto ambao alizaa na mwanamke mwingine, ikabidi wao wapate mgao wa nyumba ya Msasani na mimi nibaki na nyumba ya Mikocheni B. “Siku moja, nakumbuka ilikuwa ni mwaka 2001 walikuja hao watoto wa mume wangu na kuvunja mlango kisha kuingia na kunifukuza na kuninyang’anya kila kitu yakiwemo mavazi.

 

“Baada ya hapo nilikwenda kituo cha polisi ili wanisaidie, lakini waliniambia hawawezi kunisaidia niende mahakamani. “Nilipokwenda mahakamani, mwaka 2006 nilishinda kesi na nikatangazwa na mahakama kuwa mmiliki halali wa nyumba hiyo ya Mikocheni B.

 

“Hata hivyo, wale watoto walikata rufaa na kesi ikaanza upya. Nikiwa naendelea na ile kesi, mara faili likapotea, nikahangaika sana ndani ya miaka minne ndiyo faili la kesi likaonekana na nilipofuatilia nikaambiwa kesi imeshapita muda, niandike barua upya na kutafuta wakili wa kujitegemea.

 

“Hapa nilipo sina ndugu, ndugu zangu walikuwa Bukoba na wameshafariki dunia, uwezo wa kutafuta wakili nimlipe sina na ninaumwa, niligongwa na pikipiki, mpaka sasa hali yangu siyo nzuri kwa hiyo najua Rais wetu (Dk John Pombe Magufuli) ni Rais wa wanyonge, namuomba aniokoe maana nateseka, aniangalie mimi niweze kupata haki yangu angalau nipate hata nyumba.

 

“Hapa ninapoishi sasa sasa hivi nimesaidiwa tu na Mama Maria Nyerere ambaye aliamua kuingilia suala langu kati baada ya kuona ninateseka. Kuhusu chakula napewa na majirani zangu,” alisema bibi huyo akiangulia kilio kizito.

 

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa TPBC-Mikocheni, Idrisa Ramadhani alisema kuwa ni kweli bibi huyo wanaishi naye katika maeneo yao, lakini nyumba ambayo inadaiwa kuwa amedhulumiwa haipo katika mtaa wake.

 

“Sisi kama Serikali ya mtaa tunamtambua huyu bibi ambaye ni mjane na anaishi maeneo ya mtaa huu, amepata msaada hapo, lakini suala la yeye kudhulumiwa nyumba, hajaleta taarifa ofisini na pia hiyo nyumba ambayo anasema kuwa amedhulumiwa haipo maeneo haya, ipo Mikocheni B kwa hiyo aende kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mikocheni B kule atasaidiwa,” alisema mwenyekiti huyo.
Toa comment