visa

BABA ALIYENASWA LAIVU NA MGUU WA MWANAYE UNDANI NI HUU!

MBEYA: Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni! Tukio la baba aliyefahamika kwa jina la Tatizo Yahya Japhet Nguku (37), mkazi wa Kijiji cha Msewe, Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo, wilayani Mbarali, jijini hapa kushikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kunaswa na kipande cha mguu wa mtoto wake, Rose Japhet, limeibua mshangao mkubwa, UWAZI lina undani wa tukio hilo. 

 

Mtoto wake huyo wa kike mwenye umri wa miaka sita, alidaiwa kuuawa na kukatwa sehemu hiyo baada ya kupotea katika mazingira ya kutatanisha wiki moja iliyopita na kukutwa akiwa ameuawa kwa kunyongwa kwenye Hifadhi ya Msitu wa Chimala.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na gazeti hili, Nguku alidaiwa kumchukua mtoto wake huyo kutoka mikononi mwa babu yake anayeishi Igurusi. Walidai kuwa chanzo cha mtoto huyo kwenda kuishi kwa babu yake ni kutokana na baba yake huyo kutengana na mkewe aliyefahamika kwa jina la Scola Chafumbwa, mkazi wa Nyololo. Ilifahamika kuwa, wakati tukio hilo baya linatokea, mama wa mtoto huyo alikuwa alikuwa mkoani Njombe.

 

Kwa mujibu wa Scola, alipata taarifa za kupotea kwa mwanawe kutoka kwa kaka yake ambaye alimwambia kwa mara ya mwisho mtoto huyo alichukuliwa na baba yake kuelekea Mbalizi. Hata hivyo, ilisemekana alipofika Mbalizi mtuhumiwa huyo alifikia Mtaa wa Mtakuja alipotafuta nyumba ya kupanga kupitia kwa mwenyeji wake, lakini nyumba aliyotarajia kupanga alikuta imeshachukuliwa na mtu mwingine.

 

Ilisemekana kwamba, baada ya hapo baba huyo aliondoka na mwanawe na kwenda kupanga kwenye nyumba ya wageni almaarufu gesti. Juu ya sakata hilo, UWAZI lilizungumza na Diwani wa Kata ya Nsalala, Kissman Mwangomale ambaye alisema mtuhumiwa huyo alimwambia kuwa ameishi gesti siku moja tu, lakini rafiki yake alidai ameishi zaidi ya siku tano.

 

Mwangomale alisema baada ya kupata taarifa za kupotea mtoto huyo aliagiza ipigwe mbiu ili kumtafuta mtoto huyo kwenye maeneo mbalimbali ya Mbalizi na nje ya wilaya hiyo bila mafanikio. Alisema siku tano tangu kupotea kwa mtoto huyo ambaye picha yake ililiza wengi, waliamua kusitisha zoezi la utafutaji.

 

Alisema kama diwani na mlinzi wa amani katika kata yake, alimtilia shaka mzazi huyo hivyo alitoa taarifa Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Baadhi ya wananchi ambao hawakupenda kutaja majina yao walisema walipokuwa wakimtafuta mtoto huyo, mzazi wake huyo hakuwa na shaka na aliendelea kufanya shughuli zake kama kawaida.

Hata hivyo, ilisemekana kwamba baadhi ya wananchi walimuona akiwa na rambo nyeusi mikononi. Ilidaiwa kuwa baada ya kubanwa zaidi, mtuhumiwa huyo alidai kuwa hiyo rambo nyeusi ina mguu wa mtoto wake na alipobanwa alienda eneo alilodai kuukuta mguu na walipofukua hawakuweza kukuta mwili wa mtoto.

 

Ilidaiwa kuwa, mzazi huyo alishirikiana na baadhi ya watu kutekeleza mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kushirikina. “Naomba Polisi wambane mume wangu ili aoneshe mwili wa mtoto wangu angalau niuone na nikazike,” alisema Scola huku akibubujikwa na machozi.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, SACP Ulrich Matei, lithibitisha kuwashikilia watu wawili waliofahamika kwa majina ya Japhet Yahaya Nguku (37) na Andrew Anganile Mwambuluma kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Rose.

 

“Mnamo Mei 3, mwaka huu, majira ya saa 3:00 usiku huko kijijini Msewe, Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo wilayani Mbalali Mkoa wa Mbeya katika msitu wa hifadhi ya Chimala mtoto Rose alikutwa ameuawa kwa kunyongwa shingo na kukatwa kanyagio la mguu (unyayo) wa kulia. “Unyayo huo ulikutwa umefukiwa huko Mbalizi Wilaya ya Mbeya-Vijijini.

 

“Chanzo cha mauaji hayo ni tamaa ya kupata utajiri ambapo baba mzazi wa marehemu alimuuza mwanawe kwa Andrew Anganile ambaye ni mfanyabiashara kwa malipo ya shilingi milioni tano ili auawe na kutolewa kiungo hicho cha mguu wa kulia kisha kipelekwe kwa mganga wa kienyeji amtengenezee ndagu (dawa ya utajiri) ili afanikiwe katika biashara.

 

“Mfanyabiashara huyo amekiri kuhusika na tukio hilo na ufuatiliaji unaendelea ikiwa ni pamoja na msako mkali wa kumtafuta mganga huyo kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema Kamanda Matei.
Toa comment