The House of Favourite Newspapers

Baba Amshangaa Msuva Kukataa Mshahara wa Mil. 9

0

SIKU chache baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva amekataa kupokea mshahara wa Sh milioni 9 kwa mwezi kutoka timu ya Difaa El Jajida ya nchini Morocco na kuamua kubaki Bongo, hali hiyo imemshangaza baba yake mzazi, mzee Happygod Msuva.

 

Dafaa El Jajida ni timu ya Ligi Kuu Morroco na msimu ujao itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufanikiwa kushika nafasi ya pili katika ligi kuu ya nchini humo nyuma ya Waydad Casablanca.

 

Inadaiwa kuwa, timu hiyo ilikuwa imepanga kumlipa kila mwezi kiasi cha dola 4,000 (takribani Sh milioni 9) lakini inaelezwa amekataa fedha hizo kuwa ni kidogo huku pia Yanga nayo ikidaiwa kukataa kitita cha dola 80,000 (takriban Sh milioni 177) ambazo timu hiyo ilikuwa tayari kuzitoa kama ada ya usajili.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, mzee Msuva alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ni kingi ukilinganisha na kile anacholipwa mwanaye huyo na Klabu ya Yanga, kwa hiyo anashangaa ni kwa nini amekikataa.

 

Inaelezwa kuwa katika kikosi cha Yanga, Msuva anachukua mshahara wa Sh milioni nne kwa mwezi.

“Ni fedha nyingi lakini sijui ni kwa nini amezikataa kwa sababu sijui chochote kuhusiana na taarifa hizo zaidi ya kuziona katika vyombo vya habari.

 

“Kwa hiyo, hivi sasa siwezi kusema chochote kile mpaka hapo nitakapozungumza naye kwa sababu mambo yake mengi huwa ananishirikisha na mpaka anaondoka hivi karibuni kwenda Afrika Kusini na timu ya taifa hakuniambia chochote kuhusiana na taarifa hizo, labda kama zimekuja akiwa ameshafika huko.

 

“Nilichokuwa nakijua mimi ni kwamba kulikuwa na timu moja ya Morocco ilikuwa inamhitaji ila jina lake limenitoka kidogo sasa siwezi jua kama ni timu hiyo au ni nyingine, lakini pia mbali na hiyo, alikuwa anatakiwa Algeria, Misri pamoja na Afrika Kusini.

 

“Kwa hiyo ukweli wa jambo hilo nadhani tutaujua pindi atakapokuwa amerudi kutoka Afrika Kusini, “ alisema mzee Msuva.

 

Sweetbert Lukonge | Dar es Salaam

Leave A Reply