The House of Favourite Newspapers

Baba Anayedaiwa Kuua Mwanaye Auze Viungo… Mazito Yaibuka

0

SIMULIZI ya kusikitisha inayohusu mauaji ya mtoto Aminata Katunzi (7), aliyekutwa amekufa Januari 24, mwaka huu, eneo la Mpiji Majohe, jijini Dar es Salaam, inachukua sura mpya baada ya mambo mapya kuibuka.

Habari ya mauaji ya Aminata yaliripotiwa kwa mara ya kwanza na gazeti ndugu na hili; Risasi Jumamosi, toleo la juzi Jumamosi ya Februari 01, mwaka huu.

Baba (wa kambo) wa Aminata aliyetajwa kwa jina la Ayubu ndiye anayehusishwa na tukio hilo, ambapo hadi sasa anashikiliwa na jeshi la polisi.

Mambo yaliyoibuka ni mosi; kuhusishwa kwa imani za kishirikina na pili; kukamatwa kwa mganga anayedhaniwa kuhusika na mauaji ya mtoto Aminata.

USHIRIKINA

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mjomba wa marehemu Aminata, ambaye ni kaka wa mama wa mtoto huyo aitwaye Idd Athumani, anafafanua mambo hayo kwa kirefu.

“Dada yangu aliponieleza suala la mtoto kutoweka akiwa na baba yake (wa kambo) Ayubu, niliungana naye kuanza kumtafuta,” anasema Idd na kuongeza:

“Lakini tukawa tunashangazwa namna ambavyo shemeji hayupo nasi. Binafsi nilihisi kuna kitu, na kweli nilipombana akaniambia kuwa mtoto alimpeleka kwa mganga, ambapo alimpa mganga huyo shilingi elfu tatu (Tsh. 3,000) na kumpigia ramli.

“Akasema eti alimwambia mtoto angerudi mwenyewe, maana alikuwa maeneo yaleyale ya jirani. Nikamwambia atupeleke, akatupeleka lakini tukagundua kuwa alipotupeleka siyo kwa mganga.”

Anasema wakiwa katika harakati za kumlazimisha awaonyeshe nyumbani kwa mganga huyo, likafika gari la polisi na kumchukua hadi Kituo cha Polisi Sitakishari.

“Sisi tulirudi nyumbani tukaendelea na kumtafuta mtoto huku tukimwacha shemeji kule kituoni, ndipo Jumatatu tulipofanya utaratibu wa kuingia kwenye pori la jeshi. Tulifanikiwa kumpata akiwa amefariki na kukatwa viungo vya mwili. Basi, tukafanya taratibu na tukachukua mwili na kwenda kuuzika,” anasema.

Idd anasema, Ayubu alipokuwa kituoni alibanwa na kukiri kushiriki tukio hilo kwa vile alipewa oda na mfanyabiashara wa ng’ombe, Pugu – Mnadani ambaye anafahamika kwa jina moja la Riziki.

“Alisema aliambiwa angepewa shilingi milioni moja na laki mbili (Tsh. 1.2 milioni). Alimtangulizia laki mbili, ambapo aliahidiwa angemaliziwa milioni baada ya kukamilisha zoezi hilo,” alisema.

Baada ya maelezo hayo, Idd anasema walianza msako wa mganga na baadaye wakafanikiwa kumkamata eneo la Kwa Ngozoma ambapo alifikishwa polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishna Msaidizi (ACP) Zuberi Chembera alipotafutwa ili kuzungumzia kukamatwa kwa mganga huyo, akasema hana taarifa kwa vile alikuwa nje ya ofisi.

Leave A Reply