BABA MATATANI UBAKAJI WA MWANAYE

DAR ES SALAAM: AMA kweli dunia imekwisha! Wakati wazazi wengi wakiaminika kuwalea watoto katika maadili mema hali imekuwa tofauti kwa jamaa mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Ally mkazi wa Manzese Kilimani jijini Dar baada ya kuingia matatani kwa ubakaji wa mwanaye, Happines (7). Risasi Mchanganyiko lina ripoti kamili.  

 

Akisimulia mkasa huyo wa kusikitisha, mama wa mtoto huyo, Beatrice Emmanuel alisema kuwa, yeye na Ally ni mtu na shemeji yake ambapo Happy anamuita baba mdogo na wamekuwa wakiishi mtaa mmoja nyumba tofauti na ndugu yake huyo.

 

“Kwa kawaida kila siku huwa naenda kwenye mihangaiko yangu na kumuacha mwanangu pamoja na dada yake japokuwa kuna siku Ally huwa anamchukua na kumpeleka nyumbani kwake akidai anaenda kumsalimia ndugu yake mwingine.

 

“Huku nyuma nilikuwa sijui kitu. Kumbe mwanangu huwa anaharibiwa kila siku na ilipofika kama mara nne, mwanangu alishindwa kujizuia na kumwambia dada yake juu ya tabia anayofanyiwa na Ally,” anasema Beatrice huku akitokwa na machozi.

 

Akiendelea kusimulia kwa uchungu, Beatrice anasema kuwa, baada ya taarifa kumfikia alimshirikisha mama yake ambaye anakaa maeneo ya nyumbani na hapo moja kwa moja na kuanza kumhoji mtoto.

 

“Alituambia kuwa Ally alikuwa akimchukua na pikipiki mara kwa mara na kumpeleka kwake, akifika anamuweka kwenye kochi kisha anamuwashia TV na kumuwekea CD anayoipenda baada ya hapo huvua nguo zake na kuanza kumfanyia mchezo mchafu.”

 

Beatrice anasema kwa kusaidiana na mama yake walimpeleka mtoto wao Hospitali ya Kinondoni kumpatia vipimo ambapo vilionesha kuwa ameathiriwa. “Tulipeleka taarifa katika Kituo cha Polisi, Urafiki jijini Dar na kupatiwa RB, URP/RB/1246/2019 na kwa kushirikiana na maaskari tulifanikiwa kumkamata Ally na kumfikisha kituoni hapo,” alimaliza kusema Beatrice.

 

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko Mjumbe wa Manzese Kilimani, Neema Idd Kibwana anasema kuwa, alipoletewa tukio hilo alikuwa mmoja kati ya walioenda hospitali hadi polisi na anachokitaka sheria ichukue mkondo wake kwani kwa kijana huyo siyo tukio lake la kwanza.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mussa Taibu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa yupo ndani akisubiri uchunguzi. “Ni kweli tukio hili lilitokea maeneo ya Manzese Kilimani baada ya mama wa mtoto kubaini. Mtoto alichukuliwa na kutibiwa ikabainika kwamba si mara moja amefanyiwa hivyo na alipoona anaumia ndipo akatoa taarifa kwa ndugu zake.

 

“Tumemuhoji mtuhumiwa mbali na kukanusha mtoto anakiri amekuwa akipelekwa nyumbani kwake na mkewe. Upepelelezi umeshakamilika tunaandaa tu mashtaka ili apelekwe mahakamani kujibu shtaka lake. Tunaomba vijana waache tamaa ya mwili na waache ushetani wamuogope Mungu pia wanayofanya ni kinyume na sheria za nchi hii,” alisema Kamanda Taibu.

Stori: NEEMA ADRIAN, RISASI MCHANGANYIKO

Toa comment