The House of Favourite Newspapers

Baba Mbaroni kwa Ubakaji wa Binti Yake wa Miaka 6

DAR ES SALAAM: Aibu, aibu nzito ambayo si rahisi kuielezea kwa mtu mzima mwenye ufahamu wake kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za ubakaji wa mwanaye wa kumzaa mwenye umri wa miaka 6, tukio likitokea hivi karibuni wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.

 

Tafakari ya tukio hili la kuhuzunisha linafikirisha akili kwenye swali la “ilikuwaje, na alianzaje mzee huyo anayeonekana pichani ukurasa wa mbele wa gazeti hili kumfanyia mtoto wake unyama huyo katika ulimwengu huu uliojaa wanawake wa kila aina?”

Hapo ndipo OFM (Kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu) kinapoleta majibu kwa kukusimulia habari hii ya kusikitisha ambayo imefanyiwa uchunguzi wa kina kwa zaidi ya wiki mbili na kufanikisha mtuhumiwa kuwekwa katika mikono ya sheria.

 

OFM YANASA TETESI

Kutokana na umahili wake wa habari za uchunguzi, wiki mbili zilizopita OFM ilipenyezewa tetesi kuwa, Mzee Abdalah Said mkazi wa Keko Mwanga B ana tuhumiwa kumfanyia vitendo vya ubakaji binti yake wa kumzaa ambaye ni mwanafunzi katika shule ya awali ambapo jina la shule la lake vinahifadhiwa kwa sababu maalum.

Kutokana na uzito wa madai hayo, awali ilikuwa vigumu kuamini lakini kwa kuwa timu ya wachunguzi wetu huwa haikatii tamaa taarifa yoyote kabla ya kuichunguza, vijana waliingia kazini kutafuta ukweli.

 

SIKU YA KWANZA ENEO LA TUKIO

“Nendeni mkatafute ukweli wa tukio,” Mkuu wa OFM kutoka chumba cha bahari cha Global Publishers alikiaga kikosi chake kiende eneo la tukio kufanyia kazi tetesi na kuja na majibu sahihi ambapo ilifanyika hivyo.

Aidha, baada ya kufika Keko na kukabiliana na changamoto kadhaa za kumpata mzee Abdalah na mwanaye hatimaye OFM ilinasa harufu kuwa kuna asilimia kadhaa za ukweli lakini ilibainika kuwa watu wa eneo husika walikuwa na uoga wa kuliweka wazi jambo hilo kwa hofu ya kuharibu ujirani wao na mtuhumiwa wa ubakaji.

Hata hivyo, kama waswahili wasemavyo ‘hakuna mkate mgumu mbele ya chai’ siku hiyo ilimalizika kwa OFM kuweka msingi imara wa uchunguzi ambao baadaye ulifukua habari nzima iliyowatoa machozi watu wengi.

 

MTOTO AHOJIWA KWA SIRI

Pamoja na kwamba halikuwa jambo rahisi kumpata mtoto anayedaiwa kufanyiwa unyama wa kuingiliwa sehemu zake za siri na kufanya naye mahojiano, Risasi liliweza, lilimpata binti huyo na mahojiano yalikuwa hivi:

RISASI: Unaitwa nani.

MTOTO: (Anataja jina) kisha anainama.

RISASI: Usiiname niangalie mimi unieleze vizuri usiogope si nimekuambia zawadi yako ipo.

MTOTO: Mmmh (anaitikia kwa mguno wa kukubali).

RISASI: Hebu niambie usinifiche baba amekuwa akikufanya nini?

 

MTOTO: Amekuwa …(anataja kitendo cha kuingiwa na baba yake huku akionesha sehemu zake za siri. Mahojiano hayo yamerekodiwa kwa sauti na video ambavyo vinapatikana Global TV Online.

Simulizi ya mtoto huyo ambaye anatajwa kuwa ana siku tatu tu tangu aanze shule ilichoma moyo wa kila mwana OFM, kitu kilichowasukuma makamanda kuamua kuchukua hatua ya kuifikisha habari hiyo kwenye vyombo vya sheria ili haki ipatikane.

 

OFM YATINGA SERIKALI ZA MITAA

Kutokana na baba wa mtoto kutokuwepo nyumbani na wenyeji wa eneo hilo kugoma kutoa ushirikiano kwa madai kuwa mtuhumiwa ana asili ya ubabe, makamanda wa OFM walimchukua binti huyo hadi Ofisi za Serikali za Mitaa, Keko ambako walipata ushirikiano.

Hatua ya kwenda polisi kuchukua Fomu Namba Tatu ya Matibabu maarufu kama PF3 ilifanyika huku ushirikiano ukifanyika kati ya OFM, serikali za mitaa na Hamza Bakari Zayumba mmoja kati ya watoa huduma za afya za kijamii wilayani humo.

 

RIPOTI YA DAKTARI

Majibu ya vipimo kutoka katika Hospitali ya Temeke yalionesha kuwa sehemu za siri za binti huyo zimeharibika na kwamba anahitaji kuendelea kupatiwa huduma za afya.

Hii inaonesha kuwa binti huyo amekuwa akiingiliwa lakini uchunguzi wa daktari na wa OFM ulishindwa kubaini moja kwa moja kuwa mhusika wa kitendo hicho cha kifirauni ni baba yake mzazi au mtu mwingine jambo ambalo linaliweka tukio hilo mikononi mwa vyombo vya kugawa haki ambavyo vinalitazama kwa kina.

 

KUKAMATWA KWA ABDALAH

Baada ya hatua zote kukamilika, suala la kumtia mbaroni mtuhumiwa lilipewa kipaumbele ambapo OFM kwa kushirikiana na Polisi na Serikali za Mitaa walikwenda nyumbani kwa Abdalah ili kumuweka chini ya ulinzi.

Aidha, baada ya kufika walimkuta na kumtaka yeye na binti yake waongozane na wana usalama hadi Ofisi za Serikali za Mitaa, jambo ambalo mtuhumiwa hakupinga kwa kuwa aliamini kuwa ujumbe uliomfuata nyumbani huenda ulikwenda kuwapatia msaada watoto wake ambao maisha yao ni duni.

Lah! Alichokikuta katika Ofisi za Serikali za Mitaa hakikuwa alichofikiria bali ni tuhuma nzito za ubakaji ambapo binti yake alipohojiwa kwa mara ya pili alizidi kumtuhumu baba yake kumfanyia unyama.

Wakati mtuhumiwa akilia kwa kile alichodai kuangamizwa na mtoto wake kwa kupewa tuhuma nzito baadhi ya mashuhuda nao walimwaga machozi wakiguswa na maelezo aliyokuwa akiyatoa biti yule.

 

PACHA AIBUKA

Kwa kuwa binti huyo amezaliwa pacha na mwenzake wa kiume, wakati dada mtu akitoa maelezo ya kumtuhumu baba yake, kaka mtu alipigilia msumali wa mwisho kwa madai kuwa amekuwa akitolewa chumbani na baba yake kubaki na dada yake peke yao.

“Eee baba amekuwa akinifukuza mimi na kubaki na dada,” maneno ya mtoto huyo yaliwachoma wanawake wengi waliokuwepo eneo hilo, jambo lililowalazimu polisi kumchukua mtuhumiwa na kumpeleka kituoni kwa mahojiano.

 

WATOTO WAMUAGA BABA YAO

Tukio jingine la kusikitisha ni kwamba wakati baba akichukuliwa na vyombo vya usalama watoto wake hao mapacha walimpungia mkono kwa kumuaga kwa kusema; ‘kwa heri baba eee.’

Inawezekana wengi hawakujua kwa nini watoto wale walimuaga baba yao, je ni kwa sababu wamemchoka au kwa vile wanabaki wapweke kutokana na kukosa mtu wa kuwalea kwa sababu habari zinaeleza kuwa mama yao mzazi aliwatelekeza toka kitambo, ndiyo maana wengi waliangua kilio.

Kama mtu asiyeelewa kitakachotokea, baba yao naye kwa tabasamu la kulazimisha aliitikia kwa heri ya watoto wake kwa kusema “ninyi bakini salama si mmeamua iwe hivi.”

 

HAWA HAPA MWENYEKITI WA MTAA, DIWANI

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Keko, Shilingi Hashim alionesha kusikitiswa na tukio ambapo ameviomba vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa tukio hilo linachunguzwa kikamilifu na haki kutolewa.

Naye Diwani wa Viti Maalum Kata ya Keko, Manispaa ya Temeke, Pilly Mfaume alisema tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa wanawake ambao wanawatelekezea wanaume watoto na kuacha wakiteseka.

“Kwanza pamoja na mwanaume huyu kukamatwa mimi naomba na mwanamke naye atafutwe kule aliko wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria, haiwezekani uondoke uache watoto wakiteseka halafu usichukuliwe hatua.”

 

MAISHA YA WATOTO

Uchunguzi unaonesha kuwa watoto hao mapacha wamekuwa wakiishi maisha ya dhiki pamoja na baba yao, jambo ambalo linatia hofu kuwa huenda hali yao ikazidi kuwa mbaya zaidi ya hapo awali na kuyaweka hatarini maisha yao.

Maana hadi Risasi Jumamosi linaondoka eneo la tukio watoto hao walikuwa mikononi mwa Serikali za Mitaa, Keko.

CHONDE TUWASAIDIE

Kama umeguswa na tukio hili na ungependa kuwasaidia watoto hawa mapacha ambao wako na hali ngumu, wasiliana na mjumbe wao aitwaye Hamza Bakari Zayumba kwa namba 0688 664626, 0715 101204 au 0744 929557. Unaweza kutuma chochote kupitia namba hizo ili kuwasaidia watoto hao na Mungu atakubariki!

Comments are closed.