The House of Favourite Newspapers

Baba’ke Diamond Atema Cheche Kesi ya Mwanaye

Abdul Jumaa ‘Baba D’

WAKATI leo mwanaye ambaye ni staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Jumaa ‘Diamond Platnumz’ akitakiwa kuripoti kwenye Kituo Kikuu cha Polisi ‘Sentro’ jijini Dar kwa kesi ya Makosa ya Mtandao, baba’ke mzazi, Abdul Jumaa ‘Baba D’ ametema cheche, Ijumaa linaripoti.

 

Diamond anakabiliwa na msala wa kusambaza video chafu kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akiwa kitandani, akicheza na mzazi mwenzake, mwanamitindo Hamisa Mobeto na nyingine akiwa na mwanamke mwingine ambaye hakujulikana.

 

Akizungumza na Ijumaa, Baba Diamond aliwaka kuwa, alichokifanya mwanaye huyo siyo sawa kwani si jambo la kimaadili kama ambavyo serikali imeeleza. Lakini pamoja na yote, Baba Diamond alisema kuwa, yeye kama mzazi hawezi kumtupa hivyo ataungana naye katika hatua zote za kesi hiyo kuanzia leo atakapokwenda kuripoti Sentro.

 

“Mimi kama mzazi, siungi mkono alichokifanya hadi serikali ikaamua kulizungumzia suala lake bungeni mapema. “Nimeshtushwa na jambo hilo, lakini kama mzazi, siwezi kumwacha hivyo nitakuwa naye hatua kwa hatua katika jambo hili kwani siwezi kumwacha mwenyewe,” alisema Baba Diamond.

 

Pamoja naye, katika msala huo Diamond ameunganishwa na Mobeto na watuhumiwa wengine ambao ni wasanii wa Bongo Fleva, Faustine Charles Mfinanga ‘Nandy’ na William Nicholaus Limo ‘Bill Nas’ ambao hivi karibuni, nao ilisambaa video yao mitandaoni wakifanya uchafu chumbani.

 

Nasibu Abdul Jumaa ‘Diamond Platnumz’

 

Akijibu swali la Mbunge wa Ulanga, Godluck Mlinga aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani kukomesha tabia za baadhi ya watu wanaotumia mitandao vibaya, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison George Mwakyembe alisema kuwa, polisi walishamkamata Diamond juu ya video hiyo na kwamba anahojiwa.

 

Iwapo watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani, wanaweza kushtakiwa chini ya kifungu Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 ambayo inakataza kuweka kwenye mfumo wa kompyuta au taarifa nyingine yeyote kwenye mfumo wa mawasiliano ikiwemo picha mbaya kama za ngono.

 

Sheria hiyo kifungu cha 14 (1) kinaeleza kuwa, mtu hatachapisha au kusababisha kuchapishwa kwa kupitia katika mfumo wa kompyuta (a) Ponografia au (b) Ponografia yoyote iliyo ya kiasherati au chafu.

 

Inaeleza kuwa, mtu akatayekiuka kifungu kidogo cha (1) atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika, iwapo ni uchapishaji kuhusiana na (a) Ponografia, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka saba au vyote; au (b) Ponografia iliyo ya kiasherati au chafu, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni thelathini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka kumi au vyote.

Stori: Mwandishi Wetu.

Comments are closed.