Babu Alalamikia Shamba Lake Kugeuzwa Machimbo Holela ya Mchanga

Mzee Francis Muturi Maigua na mkewe, Adventina Rweyemamu Maigua wakazi wa Mbande, jijini Dar wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kumsaidia kuokoa shamba analodai mali yake ambalo limevamiwa na kugeuzwa machimbo holela ya mchanga.

Akizungumza na Mwanahabari wetu, Mzee Muturi amesema watu wasiojulikana wamevamia mashamba yake yaliyopo Mwanajilatu na Mwanambaya mkoani Pwani na kuanzisha machimbo holela ya mchanga na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwenye mashamba hayo.
Mzee huyo ameongeza kuwa ameshakwenda kwenye mamlaka husika za maeneo hayo na kufikisha malalamiko yake lakini mpaka sasa hajapata msaada wowote ambapo alisema;
“Naiomba serikali yetu tukufu inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Kitengo za Kuzuia na Kupambana na Rushwa maarufu kama Takukuru inisaidie ili hawa waharifu wakomeshwe maana hata serikali ya kijiji sina imani nayo kabisa maana nimeshailalamikia sana kuhusu uharifu huu unaofanywa kwenye mashamba yangu na mke wangu lakini hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa.
“Na mbaya zaidi uharifu huo unazidi kuendelea mpaka sasa”. Alimaliza kusema Mzee Muturi.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Serikali ya vijiji husika zinaendelea na wakipatikana nao watapata fursa sawa ya kulizungumzia sakata hilo. HABARI/PICHA NA ISSA MNALLY /GPL