The House of Favourite Newspapers

Babu Seya, Papii Kocha Walituma Ujumbe Mzito kwa JPM

Babu Seya na mwanaye wakitoka gerezani.

BADO mitaani kuna shangwe inayotokana na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Joseph Magufuli ‘JPM’ kutangaza kuwaachia huru mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanawe, Johnson Nguza ‘Papi Kocha’, waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha gerezani.

Akihutubia taifa katika sherehe za uhuru mjini Dodoma, Jumamosi iliyopita, mbali na Babu Seya na Papii, JPM pia alitangaza kuwasamehe wafungwa wengine 8,157 na kuagiza 1,828 kati yao watolewe magerezani na waliobaki wapunguziwe muda.

Kufuatia shangwe hizo, Ijumaa Wikienda linakumbushia makala ambayo miezi kadhaa iliyopita ilifanywa na gazeti ndugu la hili, Risasi pamoja na Babu Seya na Papii Kocha ndani ya Gereza la Ukonga, Dar.

Katika mahojiano hayo maalum ambayo ilikuwa ni mara ya kwanza tangu waklipohukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2004 kwa kosa la unajisi wa watoto 10 wa Shule ya Msingi Mashujaa iliyopo Sinza, Dar, wawili hao walituma ujumbe mzito kwa JPM, fuatilia;

Baada ya salamu, Risasi lilianza maswali papohapo.

Risasi: “Tulipata taarifa kwamba, mmeandika barua kwa Rais Magufuli kuomba msamaha. Hii habari imeenea mtandaoni. Hebu tuambieni, ipoje?

Babu Seya: “Iko hivi, sisi…”

Papii: (akadakia yeye, baba yake akanyamaza) “ngoja niseme mimi. Ukweli ni kwamba, barua niliandika mimi mwaka 2010. Ilikwenda kwa Rais Kikwete (Jakaya, wakati huo). Lakini tangu pale sijawahi kuandika tena barua. Hiyo inayosambaa mtandaoni ni ileile inajirudia. Kwa Magufuli hatujawahi kuandika barua.”

Risasi: “Sawa. Kwa nafasi hii tungependa kuzungumza na ninyi mambo mbalimbali ambayo hamjawahi kuyasema tangu mmeingia gerezani. Hebu tuanze na kesi yenu. Kuna wakati ilisemekana mmekata rufaa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika yenye makao yake Arusha, mkipinga kifungo. Je, nini kinaendelea?”

Papii: “Ni kweli. Ila ilichotakiwa ni wao baada ya sisi kupeleka hati yetu, walitakiwa kuja kutuhoji ili wajue tulichoandika ni sawa au kuna ya kuongezea. Lakini hawajatokea.”

Risasi: Kwako Babu Seya. Je, mnaamini kuwa iko siku mtatoka gerezani?”

Babu Seya: “Mimi naamini kwa haki ya Mungu iko siku lazima. Nasema hivi kwa sababu, Mungu ndiye anayejua ukweli wa kesi tuliyofungiwa. Anajua nini kilitendeka.”

Rais Magufuli.

Papi Kocha: (anaunga mkono maneno ya baba yake kwa kutingisha kichwa).

Risasi: “Kwani Babu Seya, unataka kusema kuna namna katika ile kesi yenu? Hiyo namna iko wapi?”

Babu Seya: “Chanzo cha yote yale ni Wimbo wa Seya niliouimba mimi na mtoto wangu (Papii). Ule Seya wa Mivano. Pale ndipo pana chanzo, lakini siwezi kusema nini kilitokea, siko tayari kusema.”

Risasi: “Hivi siku yenu ya kwanza kuingia hapa gerezani ilikuwaje? Mlilia kwa kiasi gani?”

Babu Seya: “Wala! Tulimwamini Mungu. Tulijua Mungu ana makusudi yake na iko siku itajulikana ukweli umesimamia wapi.”

Risasi: “Maisha yenu hapa jela yakoje? Maana tukiwaangalia tunawaona mpo fiti sana.”

Babu Seya: “Kama hivi, tunaendelea vizuri sana. Tumezoea na hakuna unyanyasaji wowote.”

Risasi: “Kumekuwa na madai kwamba, Babu Seya unaumwa. Wakati mwingine ikadaiwa upo hoi. Je, kuna ugonjwa umekupata ukiwa hapa au mwanao?

Papii: (anatingisha kichwa kukataa).

Babu Seya: “Mimi niliumwa, nikaenda kupimwa na kugundulika nina diabetes (kisukari). Ni kama miaka minne iliyopita.

Risasi: “Wengi wakiingia gerezani hubadili imani. Wapo ambao huamua kuokoka. Ninyi je, tangu mmefika mmebadili madhehebu?”

Papii: “Hapana, sisi tuko na imani yetu ileile ya Romani Katoliki. Tulipokuwa nje, kanisa letu lilikuwa pale Sinza, Shule ya Msingi Mashujaa kwa mbele.”

Risasi: “Tangu mmekutwa na hatia na kutupwa huku jela, viongozi wenu wa dini wameshakuja kuwajulia hali?”

Papii: “Hapana.”

Risasi: “Tunajua Babu Seya ulikuwa na bendi yako ya muziki, Achigo Band na ulikuwa ukipiga pale Lion Hotel. Je, ulimwachia nani?”

Babu Seya: “Ile nilimwachia mwanangu mkubwa.”

Risasi: “Mbangu?”

Babu Seya: “Hapana, kaka yake.”

Risasi: “Babu Seya umeacha mke uraiani?”

Babu Seya: (anasikitika) “Hapana, mke wangu alifariki dunia kabla sijakumbwa na kesi.”

Risasi: “Msamaha wa binadamu ni jambo muhimu sana. Hata Mungu anauona na unaposema ukweli na kukiri kile ulichokifanya, anaweza kukusamahe. Maana kama ni kufungwa tayari mpo kifungoni, hakuna sababu ya kudanganya tena. Je, ukweli wenu ni upi? Ni kweli mlibaka?”

Babu Seya: “Kusema ukweli kwa haki ya Mungu nakuapia, mimi wala dogo huyu (Papii) hakuna anayehusika na yale madai. Hata siku ya kukamatwa, mimi nilikuwa nyumbani wakati ule pale Sinza, nikashangaa navamiwa, naambiwa nimebaka wale watoto. Huyu dogo (Papii) yeye alikuwa ametoka Arusha, akaunganishwa kwamba naye alikuwemo.

“Ndiyo maana nikasema kwamba ule Wimbo wa Seya wa Mivano pana kitu. Lakini sikisemi. Wale watoto mimi hata kuwajua siwajui maskini ya Mungu.”

Risasi: “Kwa hiyo hamkubaka?”

Babu Seya: “Kwa vile hukumu imeshapita, mahakama ikatuona tuna hatia, hakuna namna ambayo tunaweza kusema zaidi ya kukiri kwamba tulifanya kwa sababu tulikutwa na hatia…

Papii: (akadakia) “Maana hata tukisema hatukubaka, watu watatuuliza kwa nini sasa tuko gerezani? Mtu ukishahukumiwa tafsiri yake ulitenda kosa na ndiyo maana ulikutwa na hatia hata kama hukufanya lile kosa.”

Risasi: “Kwa maana hiyo mnapoyazungumza hayo, mnawaambia nini Watanzania?”

Babu Seya: “Tunawaomba watusamehe kwa yote yaliyotokea na watuombee kwa Mungu siku moja tutoke gerezani ili kuungana katika ujenzi wa taifa.”

Risasi: “Ni kawaida kwa watu waliofungwa wakitoka gerezani kubadili mstari wa maisha. Wengine huamua kumtumikia Mungu, wengine hufanya shughuli yoyote tofauti na ile ya awali. Je, ninyi ikitokea mmetoka jela, mmepanga kufanya shughuli gani?”

Babu Seya: “Kwanza ikitokea tukaachiwa huru tutachanganyikiwa. Hivyo hatujawahi kupanga cha kufanya. Maana tukisema tukitoka tutamtangaza Mungu, watu watasema tumechanganyikiwa (kicheko, Papii naye kicheko).

“Lakini tukisema tuendelee na muziki, pia watu watasema tunarudia mambo yetu. Kwa hiyo tutaangalia cha kufanya wakati ukifika.”

Risasi: “Babu Seya umesikika ukisema uliishi Sinza. Kwani kwa sasa maskani ya familia yako ni wapi?”

Babu Seya: “Yapo Kimara. Pale Sinza niliuza nyumba baada ya ndugu kunishauri ili nibadilishe mazingira.”

Risasi: “Familia yako ikoje sasa?”

Babu Seya: “Familia haiko sawa kwani roho ni mimi na ndiyo niko gerezani. Kwa hiyo familia haiko sawasawa maana roho haipo (kicheko).”

Risasi: “Mlisema kuwa, mliwahi kuandika barua kwa Jakaya Kikwete kabla ya Rais Magufuli. Je, kwa Magufuli mnampa ujumbe gani?”

Babu Seya: “Sisi kwa nafasi hii ya leo, tunamuomba sanasana Rais Magufuli aitishe faili la kesi yetu (huku Papii akitingisha kichwa kukubaliana na maneno ya baba yake). Asome mwenyewe mwanzo hadi mwisho, aone ukweli uko wapi! Lazima atabaini ukweli kwamba kufungwa kwetu kulitokana na nini!

“Lakini naamini kwamba, Mungu hawezi kuacha jambo ambalo si la kweli liendelee kujulikana ni la kweli kwa muda wote, lazima kuna siku atainua nguvu zake na ukweli utajulikana. ”

Risasi: “Je, endapo itatokea njia zote za kutoka jela zimeshindikana, mtafanya nini?”

Babu Seya: “Tutamshukuru Mungu na kumwachia yeye kila kitu. Kwani lazima atakuwa na makusudi yake.”

Makala Maalum: Mwandishi Wetu, Dar

 

JPM KAAGIZA! Babu Seya, Papii Kocha, Waachiwe Huru!

Comments are closed.