BALAA LA TALAKA 3 MAMA NA WANAYE WALAZWA NJE SIKU 9

TALAKA tatu alizopewa na mumewe zinaonekana kumtesa mwanamke mmoja aitwaye Kaigo Salila (34), mkazi wa Kigogo Freshi jijini Dar es Salaam ambaye amelazimika kulala nje kwa siku tisa akiwa na watoto wake wawili baada ya kuambiwa na mtalaka wake kuwa hana ruhusa kuingia ndani.

 

Chanzo kililiambia UWAZI kuwa, mwanamke huyo yuko kwenye mateso huku habari zikidai kuwa nyumba anayozuiliwa kuingia Kaigo amejenga yeye kwa jasho lake.

 

“Hata kama sina ushahidi wa kutosha lakini kusema kweli huyo mwanamke ndiye aliyenunua eneo na kuanza kujenga, mimi nilikuwa fundi na hela za kazi alikuwa ananilipa yeye.

“Baadaye ndiyo mwanaume mmoja akawa anakuja, wakawa wanaishi kama mume na  mke,” alisema Ramadhani Saidi maarufu kwa jina la Kibatari ambaye ni jirani na nyumba inayodaiwa ni ya Kaigo.

 

UWAZI lililazimika kumtafuta Kaigo na kufanikiwa kufika hadi eneo la tukio na kujionea baadhi ya vitu vya vyumbani likiwemo godoro vikiwa vimewekwa nje.

Alipoulizwa Kaigo juu ya mkasa unaomlaza nje ya nyumba, kwanza alimtaja mwanaume mmoja kwa jina la Ramadhani Muhamed kuwa alifunga naye ndoa mwaka 2003 na kufanikiwa kuzaa naye watoto wawili mmoja wa kike.

 

“Mwaka 2008 alinipa talaka tatu, nikarudi nyumbani, wakati baba alipofariki mimi nilipata fedha ya mirathi nikaenda kununua eneo huko Kigogo nikawa najenga taratibu.

“Baadaye huyo mume wangu wa zamani akawa anakuja kwa ajili ya kumwangalia mwanaye wakati huo ameshanipa talaka, lakini kwa sababu ya ibilisi tukawa tunashiriki tendo la ndoa akanipa ujauzito mwingine ambao nilijifungua mtoto wa kiume.

 

“Nilipohamia kwenye nyumba yangu, yule mwanaume akawa anakuja mwisho tukawa tunaishi naye kama mume na mke, mara akaanza ukorofi, kuna siku alinipiga na kunishikia kisu akinilazimisha nitoe hati ya nyumba ili tuiuze.

 

“Kutokana na vurugu hizo nilimpeleka polisi, akapelekwa mahakama ya Ukonga akahukumiwa kifungo cha miezi sita, alipofungwa mimi nikafunga nyumba nikarudi kwetu Gongolamboto. “Nikakaa huko kwa muda baadaye nikasema nirudi kwangu, nilipofika nikakuta huyo mtalaka.

 

wangu kabadilisha makufuli na yeye hayupo, nilipomtafuta na kumpata akasema yeye hatoki kwa sababu pale ni kwake. “Ikabidi niende Serikali ya Mtaa ambapo aliambiwa atoke anipishe kwenye nyumba yangu,” Kaigo alitiririka madai ambayo UWAZI halikuweza kuyapatia uthibitisho.

Aliongeza kuwa, wakati wote wa vuta nikuvute kumtaka mwanaume huyo atoke kwenye nyumba yake Kaigo alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kupanga ambapo baadaye fedha zilimuishia hadi hivi karibuni alipoamua kubeba vyombo vyake na kuvipeleka kwenye nyumba anayodai ni yake ambako Ramadhani alimzuia kuingiza vyombo vyake ndani.

 

Inaelezwa kuwa, kumekuwa na msigano mkali kati ya watalaka hao kuhusu nyumba ambapo imedaiwa kwamba mwanaume huyo ameruhusu watoto kuishi pale lakini si mkewe wa zamani kwa sababu nyumba wamejenga wote na kwamba hivi sasa yeye  ana uhusiano na mwanamke mwingine ambaye Kaigo amekiri kumuona akiingia kulala kwenye nyumba anayodai ni yake.

 

Alipotafutwa mwanaume huyo ili aweze kueleza ni sababu ipi imesababisha kuiacha familia yake ilale nje alisema: “Nyumba tulijenga wote na tulijaliwa kupata watoto wawili kwa hiyo suluhisho ni kwamba nawaachia Serikali kwa kuwa suala hilo limeshapelekwa kwenye ofisi za Serikali tunasubiri uamuzi.

 

“Kuhusu watoto nitawaingiza ndani walale lakini mama yao hapana kwa kuwa kuna vitu vyangu ndani,” alisema Ramadhani katika mahojiano kwa njia ya simu na mwandishi wetu. Hata hivyo, Kaigo ameiomba Serikali kuigilia kati suala lake ili apate haki yake huku akiomba mashirika yanayotoa masaada wa kisheria au Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) yamsaidie kudai jasho lake.

 

MWIJAKU Afunguka – ‘ALIKIBA Kumuacha MKEWE / DIAMOND Hawezi KUOA”
Toa comment