The House of Favourite Newspapers

Balaa MC Alivyokiwasha Muziki wa Singeli Kwenye Tamasha la Mashindano ya Mapishi

0

Staa wa muziki wa singeli, Hussein Mashaka almaarufu Balaa MC, jana alifanya shoo ya aina yake kwenye Tamasha la Chakula la Coca-Cola maarufu ‘Coca-Cola Food Fest’ iliyofanyika katika Viwanja vya CCM Mwinjuma, Mwananyamala, Dar es Salaam.

Msanii huyo anayekimbiza kwenye Singeli kwa sasa, aliwapagawisha mashabiki kwa ngoma zake kali kama Kasuku, Jeje, Stress, Utajibu Nini, Nakuja, Najuta, Msumbufu, Mama Ashura, We Nani na nyingine kibao.

Nyimbo hizi ziliwafanya mashabiki kurukaruka na kumshangilia kwa nguvu kila alipokuwa jukwaani, akionyesha uwezo wake wa kipekee wa kutumbuiza.

Katika tamasha hilo linalowakutanisha wapishi na wafanyabiashara ya chakula kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Baba Lishe maarufu Stanslaus Baron aliibuka na ujumbe mzito kuhusu mitazamo ya kijinsia.

Baron alisema dhana ya kuwa jikoni ni eneo la wanawake pekee ni potofu, akisema wanaume pia wana uwezo mkubwa wa kupika na kuonyesha vipaji vyao.

Baron alisema tamasha hilo limekuja wakati muafaka, likitoa fursa kwa wauza chakula kutoka mitaa mbalimbali kuonyesha ujuzi wao wa kupika vyakula vya aina mbalimbali na kuvutia wateja.

“Mimi napinga kabisa dhana kwamba jiko ni kwa ajili ya wanawake pekee, kwani hata sisi wanaume tuna uwezo wa kupika vizuri na kuonyesha vipaji vyetu kupitia tamasha hili,” alisema Baron.

Tamasha hilo linatarajiwa kumalizika kwa kutangazwa mshindi wa jumla, ambaye atakuwa ameonyesha umahiri wa hali ya juu katika upishi, huku likiwapa nafasi wauzaji wa chakula kutoka mitaa mbalimbali kujiimarisha na kuhamasisha utamaduni wa kula chakula safi na kitamu.

Leave A Reply