The House of Favourite Newspapers

Balinya Aiteka Moro, Mashabiki Wapagawa

Straika mpya Juma Balinya.

MASHABIKI wa Yanga waliomuona kwa macho yao, straika mpya Juma Balinya wamewaambia wenzao kwamba jamaa ni fundi na ana kiwango bora.

 

Balinya raia wa Uganda, amejiunga na Yanga hivi karibuni kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Polisi FC ya Uganda na sasa yupo mkoani hapa na kikosi cha timu hiyo kilichopiga kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa 2019/20.

 

Mshambuliaji huyo ameonyesha uwezo mkubwa wa kuwasumbua mabeki na kufunga tangu mazoezini na jana Ijumaa aliwateka mashabiki wengi wa soka mkoani hapa kutokana na kufanya makubwa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Moro Kids.

 

Licha ya kwamba timu hiyo waliyopambana nayo ni ndogo lakini mashabiki wamevutiwa na ufundi wake na akili ya kufanya mambo.

 

Mechi hiyo ilikuwa ni maalum kwa kocha kujaribu kile alichowafundisha mastaa wake kwa siku kadhaa walizokaa hapa. Katika mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku wachezaji wengi wakionekana kucheza kwa tahadhari kuhofia kuumia, Balinya alifunga bao la kwanza kwa penalti, huku lingine likifungwa na Paul Godfrey ‘Boxer’. Bao la Balinya licha ya kuwa la penalti, lakini lilikuwa gumzo kutokana na ufundi wa hali ya juu alioutumia.

 

Alimchambua vizuri kipa wa Moro Kids, Godfrey Mmasa na kumuonyesha kwamba bado anahitaji kujifunza kwa wakubwa.  Championi Jumamosi ambalo lilishuhudia mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Highland uliopo Chuo cha Biblia maeneo ya Bigwa, liliwasikia mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo wakizungumzia kiwango cha Balinya huku wakisema jamaa huyo anaweza kuwa mfalme mpya kwa kuibeba Yanga msimu ujao kwani ana vitu adimu.

 

Mbali na maoni ya mashabiki hao, lakini kwa tathmini ya Championi Jumamosi uwanjani hapo pamoja na kwenye mazoezi ya wiki hii, inaonyesha kuwa mshambuliaji huyo amekamilika vizuri katika suala la kufunga kwa maana ya kuzitumia vema nafasi anazopata.

 

Mbali na hilo katika mazoezi hayo chini ya Kocha Noel Mwandila, Balinya ameonyesha umahiri katika kuuchezea mpira pamoja na kuwa na kontroo za kutosha jambo ambalo linawapa Yanga matumaini kwamba msimu ujao kitaifa na kimataifa mambo yatakuwa ni moto.

Comments are closed.