The House of Favourite Newspapers

Bandari Ya Kilwa Masoko Yapongezwa Kwa Huduma Bora

0

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepongezwa kwa Huduma bora zinazotolewa na Bandari ya Kilwa Masoko.
Pongezi hizo zimetolewa na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Uchukuzi walioshuhudia Safari za Meli za Kitalii zilizotia nanga katika Bandari hiyo zikiwa na Idadi kubwa ya Watalii kutoka mataifa mbalimbali
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Nobert Kalembwe amesema, TPA inaona fahari kushirikiana na Taasisi nyingine za Umma na binafsi katika kuwezesha ufanisi wa shughuli za Taasisi hizo.
“Nahodha wetu ametumika katika kuingiza Meli Bandarini na kuitoa, miundombinu yetu imetumika kufanikisha tukio hili ambalo ni moja ya vyanzo vya mapato yetu.
Wenyeji wa tukio hili ni Wizara ya Maliasili na Utalii na Sisi TPA ni Wadau muhimu kwa kuwa tumepewa dhamana ya kusimamia shughuli za kibandari katika Nchi yetu.
Nahodha wa Meli ya Utalii ya LE JACQUES CARTIER Capt C. DUPUY amesema, ushirikiano alioupata kutoka kwa Nahodha wa TPA na Wasaidizi wake, umeifanya Safari ya Meli hiyo kuwa na mafanikio makubwa kutokana na uzoefu mkubwa wa Wataalamu hao wa TPA uliowezesha kundi hilo la Watalii kufurahia muda wao katika ardhi ya Tanzania.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Uwakala wa Meli ya Inchcape Bw. Zakaria Urassa amesema, Kampuni yake itaendelea kuwezesha safari za Meli kuja Tanzania kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia TPA ambazo zimeleta mageuzi makubwa ya huduma katika Bandari zote za Tanzania.
Bandari ya Kilwa ni moja ya Bandari kongwe nchini ambayo hutumika kupokea Watalii wanaotembelea vivutio vya utalii vya Kihistoria vilivyo katika Mji Mkongwe wa Kilwa.
Serikali ya Awamu ya Sita kwa sasa inatekeleza mradi mkubwa wa Ujenzi wa Bandari ya Kimataifa ya Uvuvi katika Bandari hiyo.
Mradi huo ambao umeanza kutekelezwa, utagharimu fedha TZS Bilioni 260 ambapo Gati lenye urefu wa Mita 315 litajengwa na kuwezesha Meli kubwa za Uvuvi 10 kuhudumiwa kwa wakati mmoja.
Leave A Reply