The House of Favourite Newspapers

Bangala: Niwekeni Kokote Nikichafue

0

WAKATI Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, akiwa anaumiza kichwa juu ya eneo gani la kumtumia jembe lake jipya, Yannick Bangala ndani ya kikosi cha Yanga, nyota huyo ameibuka na kuweka wazi kuwa sehemu yoyote atakayopangwa atapiga kazi.

 

Benchi la ufundi la Yanga lilianza kumtumia Bangala kama kiungo wa ukabaji kwenye mechi ya Wiki ya Mwananchi dhidi ya Zanaco na kuonyesha uwezo wa juu wa kutuliza timu, kuzuia mashambulizi ya wapinzani lakini pia kupiga pasi.

 

Baada ya mechi hiyo, Bangala akachezeshwa tena kwenye eneo hilo katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba akishirikiana na Khalid Aucho na kuendelea kufanya vizuri.

 

Kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Bangala alichezeshwa kama beki wa kati baada ya nahodha Bakari Mwamnyeto kukosekana kutokana na majeraha na bado nyota huyo akaonyesha uwezo mkubwa wa kuwazuia wapinzani, uharaka wa kupandisha timu na kupiga pasi zenye macho.

 

Akizungumzia juu ya nafasi yake ndani ya Yanga, Bangala ameliambia Championi Jumamosi, kuwa kokote ambapo atapangwa na kocha wa timu hiyo Nasreddine Nabi yeye atacheza na kuonyesha kiwango.

 

“Popote ambapo nitapangwa kwenye kikosi mimi nitacheza kutokana na mwalimu mwenyewe atahitaji nicheze katika nafasi ipi ndani ya uwanja, iwe ya beki au kiungo wa ukabaji.

 

“Lakini mimi binafsi napenda nicheze katika eneo la beki wa kati licha ya muda mwingine kutumiwa na mwalimu kama kiungo wa chini.

 

“Kwangu nitatimiza malengo yote ya timu kwa kufanya kazi bora uwanjani na kushinda vile vitu ambavyo tumejiwekea, hilo ninawaahidi mashabiki wa Yanga msimu huu,” alisema Bangala, raia wa DR Congo.

 

Wakati huohuo chanzo kutoka Yanga kimeliambia Championi Jumamosi, kuwa kutokana na kukoshwa na kazi ya Bangala ndani ya michezo hiyo mitatu, kocha Nabi amefanya maamuzi ya kumuondoa Mukoko Tonombe katika eneo la kiungo cha ukabaji.

 

“Mechi yetu na Simba imetosha kabisa kwa kocha Nabi kumvuta rasmi Bangala katika dimba la kati, ambapo sasa rasmi Mukoko atampisha, kufuatia uwezo wake wa kuvuta mashambulizi na pasi bora alizoonyesha.

 

“Kwenye mchezo wetu na Kagera Sugar, Bangala alionekana kumudu pia nafasi ya beki wa kati, jambo ambalo kocha ameona ni vyema kumtumia kama kiungo na katika nafasi ya beki ataendelea kumchezesha Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kama Mwamnyeto (Bakari) akiwa na dharula, na sio Bangala tena,” kilisema chanzo hicho.

MUSA MATEJA NA MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

Leave A Reply