The House of Favourite Newspapers

BANKA AMENOGA BALAA, SIMBA MTAMTAMBUA

KIUNGO mchezeshaji wa Yanga, Issa Mohamed ‘Banka’ amethibitisha kuwa kweli amerudi rasmi katika uwezo wa juu baada ya kuonyesha kiwango kikubwa kilichowaduwaza mashabiki wa timu hiyo. Banka hivi karibuni alirejea uwanjani na kuanza kuitumikia timu hiyo ya Yanga aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar baada ya mkataba wake kumalizika.

 

Kiungo huyo fundi wa kuuchezea mpira, alianza kuichezea timu hiyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara baada ya kutoka kifungoni, alifungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa muda wa miezi 14.

 

Fundi huyo alianza kucheza mechi yake ya kwanza ya ligi wiki iliyopita dhidi ya JKT Tanzania akitokea benchi kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa na kucheza kwa dakika chache.

Banka alithibitisha ubora wake na kuwa kivutio kwa mashabiki wa Yanga kwenye mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, Bigwa mkoani Morogoro ambapo timu hiyo imeweka kambi.

Katika mazoezi hayo, kiungo alionyesha umahiri wake mzuri wa kupiga pasi safi zilizonyooka huku akipiga chenga cha mahudhi wakati Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alipopanga
vikosi viwili.

 

Aliwapagawisha mashabiki zaidi, pale alipokuwa anakutana na kiungo Mkongoman, Papy Tshishimbi na kumchambua huku akimnyang’anya baadhi ya mipira kwa kutumia nguvu.

 

Mazoezi hayo yakiendelea, mashabiki hao walisikika wakimzungumzia kutokana na kiwango chake kizuri alichokuwa anakionyesha huku wakiombea kiungo huyo aanzishwe kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kitakachoivaa Simba.

 

“Banka yupo vizuri na ameonekana amerudi kwelikweli, angalia jinsi anavyopiga pasi na anavyopokea mipira yake vizuri, nitafurahi nikimuona akianza katika mechi na Simba,” alisikika shabiki mmoja.

Comments are closed.