The House of Favourite Newspapers

Barabara za Mawe Mwanza zageuka Kivutio, TARURA kilimanjaro waja kujifunza

0

Wafanyakazi 25 kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Kilimanjaro wamewasili mkoani Mwanza kwa ziara ya siku 1 ya mafunzo ya namna ya kujenga barabara kwa kutumia teknolojia ya mawe hususani kwenye maeneo ya miinuko.

Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Miundombinu, Mbunifu Majengo Chagu Nghoma amesema Teknolojia hiyo inasaidia kuwafikia wananchi wanaoishi kwenye miinuko kutokana na kuwapelekea barabara ya kudumu kwa gharama nafuu tofauti na siku za nyuma ambapo walijengewa kwa udongo na changarawe na kupelekea kutodumu kwa muda mrefu.

Vilevile, amebainisha kuwa kutokana na kufikika kwenye maeneo hayo kutokana na uwepo wa barabara, inaweka pia mazingira rahisi ya kupeleka huduma za jamii kama Shule, Masoko, Maji na Umeme kwenye makazi ya miinuko kutokana na mipango miji kuwa inayoeleweka tofauti na kwenye makazi ambayo kunakua na barabara za asili zisizopitika kwa urahisi.

“Ujenzi wa barabara hizi unasaidia sana kutumia nguvu kazi za wananchi kwenye eneo husika kwa ajira za muda na inailetea sifa Serikali kwa kutekeleza miradi hiyo kwa kundi kubwa la wananchi wanaoishi kwenye makazi ya miinuko ambao hali zao wengi ni za chini kiuchumi.” Amefafanua Nghoma.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Goodluck Mbaga amesema Teknolojia ya Ujenzi wa barabara za mawe ni nzuri na nafuu kwani kwa barabara ya Kilomita Moja inagharimu wastani wa Milioni 360 tofauti na gharama za kujenga barabara za kiwango cha Lami ambayo hugharimu zaidi ya Milioni 800 kwa Kilomita.

“Teknolojia hii ni nafuu na bora sana yaani inakupa uwezo hata wa kuyatumia mawe hayo kwa shughuli zingine baada ya muda wa barabara kuisha na tunawashukuru sana wetaalamu walioileta teknolojia hii hapa nchini miaka ya 2007 ambapo ilijengwa barabara ya kwanza Kigoma kabla ya mwaka 2008 kuitumia mkoani Mwanza.” Mhandisi Mbaga

Meneja TARURA Kilimanjaro Mhandisi Francis Nicholas amesema ziara yao ina tija kwani wamekuja Mwanza kujifunza namna ya kutumia teknolojia ya ujenzi wa barabara za mawe huku akibainisha kuwa wana maeneo ya miinuko na wana utajiri wa mawe mkoani kwao hivyo wameona waje wajifunze namna ya kutekeleza hususani kuyadhibiti maji.

Amesema kuwa Same na Mwanga ni miongoni mwa wilaya zenye jiografia ya milima na mawe mengi na katika kutimiza adhma ya kumsaidia Mhe. Rais Samia kutekeleza miradi ya barabara kwa gharama za chini lakini kwenye ubora hivyo wameona waangazie kwenye matumizi ya teknolojia hiyo ambayo huzalisha barabara za kudumu muda mrefu.

Awali Mhandisi David Christopher kutokka Ofisi ya Meneja wa TARURA Mwanza alielezea kuwa Mkoa huo una barabara zenye Urefu wa Kilomita 18.74 na kwamba halmashauri ya Jiji la Mwanza ilikua ya kwanza kujenga barabara zenye Urefu wa Kilomita 1.5 Mwaka 2008 kabla ya kuanzishwa kwa TARURA.

Leave A Reply