Barakah: Sitaki Kusikia Rockstar

WAKATI nalainisha moyo kupenda, siyo kama ninakosea…

Ipo sababu ya mimi kurejesha namba ambayo ilipotea…

Hali ya mtoto kumsusa mama akishachapwa…

Ni sawa na mapenzi…

Ukishapendwa…

Unasahau hata kama ulishafanyiwaga ushenzi…

Nakumbuka nilijuta sana kupenda… Kupenda kusikokua na thamani…

Ila hitaji la moyo lalazimisha kurudia zamani…

Mimi bado nina imani…

Ipo siku utanipa thamani…

Mimi bado nina imani…

Jua mi siachani nawe…

Na sishindani nawe…

Maana upo moyoni ndani…

Acha nisote miye…

Ila mi siachani nawe…

Na sishindani nawe…

Maana upo moyoni ndani…

Acha nisote miye…”

Pamoja na kwamba ni ngoma ya kitambo kidogo ya Siachani Nawe, lakini bado mashairi yake yaliyojaa mahaba ndani yake, yanaendelea kuponya maumivu ya mapenzi ya wengi. Ni kutoka kwa Baraka Andrew Odiero almaarufu Barakah The Prince.

Huyu jamaa ni bonge moja la kipaji kunako Bongo Flevani. Kila kona ukitaja jina la Barakah, mashabiki wake huishia kusikitika kwamba anakwama wapi?

Kipaji chake kilianza kuonekana akiwa na umri wa miaka kumi tu. Ilikuwa mwaka 2004. Alianza kama mwimbaji wa Injili kabla ya kubadili upepo na kutumbukia kwenye Bongo Fleva.

So Fine ndiyo ngoma iliyomtambulisha kwenye gemu akiwa chini ya Lebo ya Tetemesha Records.

Nyota yake ilizidi kung’aa baada ya kupata nafasi ya kutumbuiza jukwaa moja na wanamuziki wa kimataifa kama T.I wa Marekani, Davido na Waje wa Nigeria na Victoria Kimani kutoka Kenya. Mwaka 2015 kwenye Tuzo za Kili Music, Barakah alilamba Tuzo ya Mwanamuziki Chipukizi Bora wa Mwaka 2015.

Barakah alizidi kutikisa zaidi kwenye uwanda wa Bongo Fleva ambapo aliachia mkwaju juu ya mkwaju kama Jichunge, Nisamehe, Mawazo, Furaha, Nivumilie, Unanigasi, Sina na nyingine kibao.

Kwa sasa Barakah anasikika na ngoma yake mpya ya Nimekoma.

IJUMAA SHOWBIZ inamsogeza Barakah karibu na wewe kwenye mahojiano maalum (exclusive) ambapo anafunguka mambo kibwena. Kubwa kuliko ni ishu nzima ya kutokufanya kazi tena na Lebo ya Rockstar ambayo kwa hapa nchini inawakilishwa na mwanamuziki Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’;

IJUMAA SHOWBIZ: Kwanza hongera kwa ngoma yako mpya ya Nimekoma…

BARAKAH: Ahsante sana.

IJUMAA SHOWBIZ: Mapokeo ya Nimekoma yakoje?

BARAKAH: Nimekoma ni ngoma kubwa kwa upande wangu, ninamshukuru Mungu maana imepokelewa vizuri.

IJUMAA SHOWBIZ: Umekuwa ukitoa kazi kali, lakini Nimekoma ni kama haisumbui sana mitandaoni, tatizo ni nini?

BARAKAH: Unajua mashabiki ndiyo wana uwezo wa kuiweka kazi ya msanii kwenye chati na wenyewe ndiyo wanajua ngoma gani iko poa. Kwa upande wangu naona ngoma ni nzuri, labda upepo tu haujakaa sawa.

IJUMAA SHOWBIZ: Umekuwa slow mno katika kutoa kazi (back to back) kama ulivyozoeleka, shida ni nini?

BARAKAH: Ni kweli kwa sasa nimekuwa slow kwenye kutoa kazi, lakini nimeona nifanye hivi kwa sababu muziki wa sasa si kama ule wa zamani. Kingine naangalia upepo unaendaje, muziki umekuwa na nguvu sana tofauti na kipindi kile. Ni bora utumie nguvu kufanya ngoma ambayo itapendwa zaidi kuliko kuachia ngoma nyingi ambazo hazina impact.

IJUMAA SHOWBIZ: Lebo yako ya sasa ya Bana Music imekuwa kimya mno katika kuachia kazi mpya, kulikoni?

BARAKAH: Bana Music haiwezi kutoa kazi hadi mimi nitoe. Kwa sasa wapo close sana na mimi kwenye kusukuma kazi zangu, ndiyo maana ukiona Bana Music ipo kimya, ujue sijatoa kazi.

IJUMAA SHOWBIZ: Uhusiano wako na lebo yako ya zamani ya Rockstar iliyokuwa ikisimamia kazi zako ukoje?

BARAKAH: Uhusiano wetu ulikuwa ni kwa ajili ya kazi na kazi imeisha. Kwa hiyo na uhusiano wetu umeisha, hatuko sawa.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini unasema hamko sawa, je, kuna ugomvi?

BARAKAH: Hapana, hakuna ugomvi wowote. Huu ni uamuzi wangu mwenyewe, nimeamua kuwa kivyangu.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, una mpango wa kurudi Rockstar?

BARAKAH: Tuachane na hayo mambo, suala la kurudi Rockstar sitaki kulisikia. Kwangu hakuna kitu kama hicho.

IJUMAA SHOWBIZ: Rais Dk John Pombe Magufuli ameruhusu maisha yaendelee baada ya makali ya Corona kupungua, je, umejipangaje kurudi tena kwenye chati na kurudisha pesa ulizopoteza? BARAKAH: Kwanza shukrani kwa Rais wetu kwa kuruhusu mambo yaendelee, tulimisi sana kukutana na mashabiki wetu, hapa nilipo nimeshapata shoo za mikoani. Kuanzia mwezi huu nitakuwa Mbeya na pia nitakwenda Bukoba (Kagera).

IJUMAA SHOWBIZ: Mipango yako ikoje kwa sasa?

BARAKAH: Mipango ipo mingi, kuanzia Oktoba (mwaka huu), nitaanza kutangaza album yangu.

IJUMAA SHOWBIZ: Album hiyo itaitwaje na ina maajabu gani?

BARAKAH: Album yangu inakwenda kwa jina la Hakuna Ugumu. Ni album ambayo imebeba content (maudhui) kubwa ikiwemo maisha yangu ya muziki, uhusiano na nyimbo za dini.

IJUMAA SHOWBIZ: Album itakuwa na ngoma ngapi?

BARAKAH: Ina jumla ya ngoma 18.

IJUMAA SHOWBIZ: Sasa hivi upo kwenye menejimenti nyingine?

BARAKAH: Hapana. Nipo chini ya lebo yangu ya Bana Music.

IJUMAA SHOWBIZ: Unaizungumziaje menejimenti yako?

BARAKAH: Ni watu ambao tunafanya kazi kwa mikakati, kauli moja, wananipambania kuhakikisha nafika sehemu inayostahili.

IJUMAA SHOWBIZ: Muziki wa sasa umekuwa na ushindani mkubwa, vipi kuhusiana na mikakati yako kuhakikisha hushuki?

BARAKAH: Cha muhimu ni kufanya kazi nzuri tu, ndiyo itakayonifanya nizidi kukaa kwenye nafasi yangu bila kushuka.

IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusu mipango yako ya kwenda kimataifa?

BARAKAH: Kila kitu ni ngazi kwa ngazi, ikifika hiyo levo ya kimataifa, nitashukuru sana.

IJUMAA SHOWBIZ: Umepitia changamoto kiasi gani kwenye muziki wako hadi hapa ulipofikia?

BARAKAH: Bila changamoto huwezi kupata mafanikio, huwa tunakabiliana nazo ili tuweze kufikia malengo.

IJUMAA SHOWBIZ: Unajivunia mafanikio gani kwenye muziki wako?

BARAKAH: Kujuana na watu wa aina tofauti ni mafanikio makubwa kwangu. Kingine ni kuweza kubadilisha chakula na kupata ninachokitaka, hayo kwangu ni mafanikio tosha.

IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusu nyumba na magari?

BARAKAH: Hivyo ni vitu vyangu binafsi. Mimi huwa sipendi kuweka mambo yangu wazi. Mimi siyo wa hivyo.

IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusu mipango ya ndoa na mchumba’ko Naj maana uchumba wenu umekuwa sugu sasa?

BARAKAH: Hilo ninamuachia Mungu, yeye ndiye muweza wa yote, akipanga nifunge ndoa, mimi ni nani nipinge? IJUMAA SHOWBIZ: Tunajua Naj anaishi Uingereza na wewe upo Bongo, je, kuishi mbali na mpenzi wako haikuathiri?

BARAKAH: Hapana, naona kawaida tu, wala hainiathiri chochote. Unajua mtu ukitaka kufurahia mapenzi yenu bila kukwazana, kikubwa ni kuheshimiana na kutambua thamani ya mpenzi wako. Hiyo ndiyo siri kubwa ya kudumu kwenye uhusiano.

MAKALA: KHADIJA BAKARI, BONGO

Toa comment