The House of Favourite Newspapers

Baraza la mawaziri; haijawahi kutokea

0

pombeNampongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuteua baraza dogo la mawaziri.Baada ya kutangazwa kwa baraza hilo wiki iliyopita, kama ilivyo ada wapo waliolikosoa kama vile mtaalamu wa uchumi ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ingawa alipongeza kuwapo kwa idadi ndogo ya mawaziri.

Alikosoa kwa upande wa uwakilishi wa Zanzibar, ambapo alisema kwa kawaida Wizara ya Mambo ya Nje, waziri wake anatokea Bara na naibu Zanzibar lakini safari hii wote wametokea Tanzania Bara.

Ukweli ni kwamba Rais Magufuli ametimiza ahadi yake ya kuwa na baraza dogo kwa kuchanganya baadhi ya wizara pamoja ili kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali.

Ametimiza ahadi yake kwa kuwa na wizara 18 ambazo ni chache ukilinganisha na serikali iliyopita, lakini ameonesha umakini katika uteuzi wa mawaziri wake kwani ametumia muda kuwatathimini na hadi sasa wizara nyeti kama vile Uchukuzi, Ujenzi na Miundombinu, Fedha na Mipango, Elimu, Sayansi na Ufundi na Wizara ya Utalii hajapata mawaziri, bado anaendelea kuwatafuta watakaomfaa.

Katika historia ya taifa hili ni Rais Jakaya Kikwete tu ndiye alikuwa na baraza kubwa la mawaziri, lakini kabla yake yalikuwa mabaraza madogo na ndicho alichofanya Rais Magufuli.

Kikubwa tumpe rais na mawaziri wake muda tuwaombee heri wafanye kazi nzuri tusonge mbele kwani ameondoa utitiri wa wizara. Pia ameteua wazoefu, wasomi na kuna mchanganyiko wa vijana na wazee. Pia alivyomrudisha Profesa Sospeter Muhongo wakati wananchi wana matumaini makubwa kwake wakitegemea kusukwa upya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hilo ni jambo jema.

Nimpongeze Rais Magufuli kwa kumteua Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo. Nimepokea kwa furaha na matumaini makubwa ya kikazi, uteuzi wa Nape kuwa waziri mwenye dhamana ya habari. Namhakikishia ushirikiano wa dhati wakati akitekeleza majukumu yake mapya.
Baadhi ya wananchi baada ya Rais Dk. Magufuli, kutangaza baraza hilo wamesema wana imani kubwa na mawaziri na manaibu walioteuliwa kwa kuwa uteuzi umezingatia mahitaji ya Watanzania.

Rais Magufuli, amezingatia uwiano wa mikoa na ameteua mawaziri na manaibu ambao tunawaomba wachape kazi na wasimuangushe.

Wapo wanaokosoa kila kitu kinachofanywa na serikali, wanakosea. Nasema hivyo kwa sababu si vema kukosoa kila jambo hata kama jambo hilo lina manufaa kwa taifa.
Kwa jinsi ninavyolipiga darubini baraza hilo jipya la mawaziri, sioni alipokosea rais.

ote walioteuliwa ni wachapa kazi. Wapo wanaodai kwamba kuna waliowahi kujiuzulu kwa kashfa lakini tujiulize mbona Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliwahi kujiuzulu uwaziri wa mambo ya ndani ya nchi lakini baadaye akawa rais wa nchi?

Lakini Ukawa pia kwa upande wao, mbona Edward Lowassa aliwahi kujiuzulu uwaziri mkuu wa umoja huo ukampendekeza kuwa mgombea urais? Ni kwamba mawaziri wanaojiuzulu kwa kuwajibika kutokana na makosa ya watendaji wao, hawana doa la kusababisha wasipewe nafasi ya kuongoza, mbaya ni yule anayeiibia serikali tena kwa ushahidi. Hivyo wanaokosoa jambo jema wanakosea sana.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply