The House of Favourite Newspapers

Baraza la Ulamaa Watoa Tamko Ndoa Dk. Mwaka na Mkewe Queenie Haijavunjika

0

BARAZA la Ulamaa, limefutilia mbali uamuzi wa “kuvunja ndoa,” uliyofanywa na sheikh wa BAKWATA mkoani Dar es Salaam, Alhadj Mussa Salum. Taarifa ya baraza hilo, iliyotolewa leo Ijumaa, tarehe 27 Januari 2023, imeeleza kuwa hatua ya viongozi wa Bakwata jijini Dar es Salaam, kuingilia shauri la ndoa ya Juma Mwaka na mkewe Queenie Oscar, ni kinyume na misingi na maadili ya uislamu.

“Ndoa ya Bwana Juma Mwaka (Dk. Mwaka) na mkewe Bi. Queenie Oscar Masanja, haijavunjika na kwa kuwa kuna malalamiko yaliyopelekwa kwenye ofisi ya Qadhi, baraza linaelekeza kuwa shauri hilo ni sharti likasikilizwa,” imeeleza taarifa hiyo, iliyosainiwa na katibu wa baraza hilo, Sheikh Hassan Said Chizenga.

Ameongeza, “Baraza la Ulamaa, linapenda kuwafahamisha Waislamu popote waliko, pale wanapoona kuna upindishwaji wa mambo wasisite kufanya mawasiliano na baraza hili.”

Hatua ya Baraza la Ulamaa – chombo muhimu cha Waislamu katika kushughulikia masuala ya ndoa, talaka na mirathi – kujitosa katika sakata la ndoa ya Dk. Mwaka, imekuja siku mbili tangu “mganga huyo,” kulalamika kuvunjwa kwa ndoa yake, kinyume na taratibu za kiislamu.

Kwa mujibu wa Dk. Mwaka, ndoa kati yake na mkewe, imevunjwa kupitia mkutano na waandishi wa habari, uliyoitishwa na Sheikh Mussa, kinyume cha taratibu.

Akizungumza kwa hisia kali, Dk. Mwaka alisema, hata kama Sheikh Mussa alikuwa na mamlaka ya kuvunja ndoa yake, bado hakustahili kufanya hivyo.

“Kwanza, huyu mtu nimekuwa na mgogoro naye kwa muda mrefu, hivyo hana mamlaka ya kimaadili ya kusikiliza shauri langu. Lakini pia, hawezi kuvunja ndoa ya mtu, bila mhusika au wahusika kupewa haki ya kusikilizwa,” alieleza.

Aliongeza: “Kwa msingi huo, ndoa yangu haijavunjika. Ni kwa sababu, waliotangaza kuwa ndoa yangu imevunjika, ni wasela tu. Hawana mamlaka yoyote ya kisheria na kimaadili ya kufanya hivyo.

SAKATA LA DR MWAKA – “NDOA YANGU HAIWEZI KUVUNJWA na WAHUNI, BADO ni MKE WANGU” | KATAMBUGA

Leave A Reply