Barbara: Tutafanya Maamuzi Magumu Dirisha Dogo

BAADA ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amefunguka kuwa wanatarajia kufanya maboresho kadhaa kwenye kikosi chao kipindi cha usajili wa dirisha dogo ili kuijenga timu ya ushindani kwenye michuano ya kimataifa.

 

Simba imeandika historia mpya ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa makundi uanzishwe baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-2 dhidi ya Red Arrows ya Zambia.

Akizungumzia ishu hiyo, Barbara alifunguka kwamba: “Kwanza kabisa tunamshukuru Mungu kwa hiki tulichokipata japo matokeo hayakuwa mazuri kwa upande wetu.

 

Suala ambalo tulikuwa tunahitaji ni kufuzu hatua ya makundi na tumefanikiwa. Kwa sasa tunaangalia mchezo unaofuata ili tufanye vizuri.

 

“Kulekea kipindi cha dirisha dogo tumejipanga kufanya maboresho makubwa ili kutengeneza kikosi cha ushindani kwenye ligi ya ndani na michuano ya kimataifa, tunasubiri ripoti ya mwalimu ambayo anatarajia kuiwasilisha wiki ijayo ili tuweze kuona ni wapi tunatakiwa kuboresha na wapi tupunguze.

 

“Ili tuwe na kikosi imara chenye uwezo wa kupambana ni lazima tufanye maamuzi magumu kama uongozi ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea ya kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na kutetea ubingwa wetu wa ligi na Kombe la FA.”

STORI NA HUSSEIN MSOLEKA, DAR


Toa comment