The House of Favourite Newspapers

Barca; Jahazi Ndiyo Linazama

0

NI kama unasoma ukurasa wa mwisho wa hadithi tamu ambayo kamwe haukutaka imalizike. Hali hiyo ndiyo inayowakumba Klabu ya Barcelona ya Hispania baada ya utawala wa muda mrefu barani Ulaya sasa wanaonekana wamegota ukingoni.

 

Klabu hiyo siyo tishio tena kama ilivyokuwa miaka 10 nyuma ambapo ilikuwa inashinda mechi zake huku ikitoa burudani ambayo iliwakonga nyoyo mashabiki wake na hata wale wa upinzani.

 

Kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Benfica Jumatano hii kinadhihirisha kuwa timu hiyo kwa sasa ipo ‘unga’ na haina tena ule utawala wake ambao ulikuwa tishio kwa timu nyingi pale ilipokuwa inakutana nayo.

Kuna mambo mengi yamechangia kuifikisha timu hiyo hapo ilipo lakini haya yanatajwa zaidi;

 

PENGO LA LIONEL MESSI

Hili lipo wazi kabisa kuwa Lionel Messi alikuwa nyota wa timu hiyo kwa miaka mingi hata pale ambapo walikuwa na kiwango kibovu. Tangu kuondoka kwa Messi msimu huu Barcelona wana hali ngumu kwenye Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ na hata kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo wanashika nafasi ya mwisho kwenye kundi E wakiwa hawana pointi hata moja.

 

Barcelona bila ya Messi inaonekana kuwa timu ya kawaida tu ndiyo maana baadhi ya timu zimekuwa zikipambana nayo na kupata hata sare ikiwa ni tofauti na wakati ambao alikuwepo nyota huyo klabuni hapo.

 

Pengo la nyota huyo mzaliwa wa Argentina linaweza kuendelea kuitesa timu hiyo kwa kuwa hadi sasa bado haijaonekana nani atakuwa mbadala wake.

 

Mastaa wanawaangusha

Sababu nyingine kubwa ambayo imeifikisha timu hiyo mahali hapo ni mchango mdogo wa mastaa ambao wanawanunua. Kwa nyakati tofauti Barcelona imewanunua mastaa Philippe Coutinho, Ousmane Dembélé na Antoine Griezmann ambao hata hivyo hawajaonyesha thamani halisi ya kununuliwa kwa fedha kubwa. Hata pia kwa Sergio Aguero ambaye hajacheza hadi sasa.

 

Coutinho amekuwa na kiwango cha panda shuka, Dembele muda mwingi amekuwa majeruhi wakati Griezmann baada ya mambo kumuelemea klabuni hapo ameamua kurudi zake Atletico Madrid kwa mkopo. Nyota hao walitarajiwa ndiyo wataibeba klabu hiyo lakini imekuwa tofauti.

 

Usajili wa kawaida

Unapoitaja Barcelona unaitaja moja ya timu ambayo imeche zewa na wac hezaji wenye majina makubwa duniani ambao wamewahi kusajiliwa n atimu hiyo. Nyota kama Rivaldo, Ronaldinho, Figo, Ronaldo de Lima ni sehemu ya usajili wa viwango vikubwa ambao umewahi kufanywa na timu hiyo.

 

Suala hilo ni tofauti na sasa kwani timu hiyo inaonekana kusajili wachezaji wa kawaida ambao wengine wanatajwa hawana hadhi ya kuvaa jezi ya timu hiyo.

Nyota Martin Braithwaite, Clément Lenglet ni sehemu tu ya nyota ambao wanatajwa kutokuwa na hadhi ya timu hiyo.

 

La Masia imekufa, haina msaada

Tatizo lingine ambalo linachangia anguko la Barcelona kwa sasa ni kutokuwa na wachezaji wakali wanaozalishwa na akademi yao ya La Masia. Akademi hiyo ilikuwa na msaada mkubwa kwenye mafanikio ya Barcelona ndani ya miaka 10 ilioyopita.

 

Nyota kama Messi, Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Carles Puyol ni sehemu ya wachezaji ambao walipandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kutoka akademi hiyo lakini kwa sasa haifanyi hivyo na kuchangia timu kusajili wachezaji wengine wa nje ambao viwango vyao siyo vikubwa.

 

Koeman haeleweki

Anguko zaidi la Barcelona linachangiwa na kocha wao wa sasa, Mholanzi Ronald Koeman ambaye inaonekana nafasi hiyo kuwa kubwa kumzidi. Kocha huyo amekuwa haeleweki namna ya ufundishaji wake na baadhi ya wachezaji. Lakini pia kuwa na migogoro na nyota wake.

 

Koeman inaonekana amekuwa akiwapa zaidi nafasi wachezaji ambao wanatoka taifa la Uholanzi jambo ambalo linachangia mpasuko na kutofanya vizuri kwa timu hiyo.

BARCELONA, Hispania

Leave A Reply