Baregu, Mbatia wazidi kuiponda Twaweza

1E9A8714

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia.

Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI Mwenza wa Ukawa, James Mbatia (pichani) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Baregu Mwesiga kwa pamoja jana wameiponda Taasisi ya Twaweza kutokana na utafiti wao wa hivi karibuni ulioonesha kuwa Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. John Magufuli amemzidi Mgombea Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa kwa asilimia 40 na kuuita kuwa umejaa propaganda za kisiasa.

Katika utafiti huo, Magufuli kama uchaguzi ungefanyika mwezi uliopita au huu angepata asilimia 65 na Lowassa asilimia 25, kwa mujibu wa Twaweza.

Mbatia alisema utafiti huo ambao Twaweza umesema ni wa kitaifa, haukuhusisha sehemu moja ya muungano wa Tanzania ambayo ni Zanzibar na watafiti hao wameshindwa kujua uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 unapaswa kutoa wabunge au madiwani wangapi.

“Picha moja iliyowekwa kwenye taarifa ya wagombea wanane wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaonesha kutokuwepo utaratibu wa kuzingatia usawa wa binadamu na hivyo kudhalilisha baadhi ya wagombea,” alisema Mbatia huku akiungwa mkono na Profesa Baregu.

Aliongeza kwamba utafiti huo ni wa uongo na hauwezi kudhuru matokeo ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu kwani wahojiwa waliweza kutoa maoni yao kuhusu sera za wagombea urais kabla hazijatolewa, hivyo wamehojiwa kabla ya kuzisoma.

Aidha, wamewaponda wahojiwa ambao wamedai ni zao la uongozi wa chama tawala kwa zaidi ya miaka 54 na hawadhani uzoefu wa uongozi ni kigezo muhimu katika kumchagua rais na mbaya zaidi walidai watafitiwa walipewa simu za bure na watafiti kama walivyoandika kwenye ripoti yao ukurasa wa pili kuwa; “Simu za mkononi na chaja zilizotumia mwanga wa jua ziligawiwa kwa kaya zilizoshiriki.”


Loading...

Toa comment