The House of Favourite Newspapers

Eric Shigongo James: Barua Kwa waheshimiwa wabunge

0

Parliament_chamber01Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Nawasalimu nyote katika jina la nchi yetu Tanzania,
Mimi ndugu yenu sijambo, naendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kujenga nchi yetu. Nawapongezeni sana kwa ushindi mkubwa mlioupata
ambao leo umewawezesha kutuwakilisha Watanzania wote katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, muhimili namba mbili katika nchi yetu.
Najua mmepita katika safari ndefu, wengi wenu mna majeraha, hayo yote yamepita, sasa ni kazi moja tu; kuwawakilisha vyema wananchi waliowatuma ili
muweze kulisogeza taifa letu mbele kwa kuisimamia vyema serikali na zoezi zima la utungaji wa sheria.
Nawapongezeni sana kwa uchaguzi wa Spika Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika Mheshimiwa Dk. Tulia Mwansasu  na pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wa
10 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. Hongereni sana.
Najua mtawakumbuka sana wabunge wenzenu ambao hawakupata nafasi ya kurejea bungeni, kama David Kafulila, kijana aliyejitolea kwa nguvu zake zote
na hata kuhatarisha maisha yake mwenyewe katika Sakata la Escrow, lakini wananchi wa jimbo lake wakamuona alikuwa mbunge wa taifa si mbunge wao,
wakamkata.
Pia mtawakumbuka sana wabunge walioaga dunia kama Deo Filikunjombe, Dk. Abdallah Kigoda, Celina Kombani, Kapteni John Komba, Mariam Mfaki,
Clara Diana Mwatuka, Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, ni vyema mkasimama hata kwa dakika moja kuwakumbuka na ninamwomba Mungu
wa Mbinguni, atuinulie watu wengine kama wao katika Bunge hili, watakaokuwa tayari kusimama kidete kutetea maslahi ya wanyonge.
Baada ya kusema hayo nielezee dhumuni la kuwaandikia barua yangu, kwani imekuwa ni desturi yangu sasa kuandika barua moja kila wiki, naandika
barua hii kuwakumbusheni juu ya jukumu lililowapeleka Dodoma na matarajio ya wananchi waliowatumeni kazi, najua mnafahamu lakini si jambo
baya kukumbushana ili asiwepo mtu atakayedhani amekwenda Dodoma kufaidi maisha, akabweteka kwa sababu ya heshima anayoipata hivi sasa kama
mbunge, miaka mitano si karne, 2020, mtakutana na wananchi kwenye boksi la kura, yasije yakawapata yaliyowapata ambao hawakurejea.
Ndugu zangu waheshimiwa wabunge wa Jamhuri ya Tanzania,
Mmepata bahati ya kuwa wabunge wa kwanza wa Bunge la 11 la awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, mmeupata ubunge katika kipindi
ambacho uchumi wa nchi yetu katika robo ya pili ya mwaka 2015 unakuwa kwa kasi ya  asilimia 7.9, hii ni kasi nzuri kwani  kuanzia mwaka 2002 -2014
uchumi wa taifa hili hili ambao ninyi ni wabunge wake ulikuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 6.72.
Waheshimiwa wabunge,
Wakati uchumi wa nchi yetu ukikua kwa asilimia 7.9, nchi nyingi za Afrika zinasuasua sana nyuma yetu, kasi ya ukuaji  wa uchumi wetu kwa  mujibu
wa taarifa za benki ya dunia umezidi mataifa makubwa duniani kama China ambayo uchumi wake umekuwa kwa asilimia 6.9 tu! Na India ni asilimia 7,
kwangu mimi hii ni dalili nzuri inayonyanyua matumaini yangu kwamba, hata kama hali ni mbaya hivi sasa, kama serikali itasimamiwa vizuri na Bunge
ambalo ninyi ni wabunge wake, hakika tumekaribia kufika katika nchi ya ahadi.
Kwa nini nimeamua kuwaandikia barua hii? Waheshimiwa wabunge, pamoja na takwimu zote zilizoko hapo juu ambazo zinaashiria mema huko
tuendako, ni ukweli ulio wazi kwamba ukuaji wa uchumi wetu haujaonekana kwenye meza ya chakula na maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Katika nchi yetu yenye jumla ya watu wasiopungua milioni 48, milioni 12 kati yao bado wanaishi katika umaskini mkubwa, hizi ni takwimu za mwaka
2015! Huduma za afya bado ni mbaya, watu wengi wanakufa kwa magonjwa yanayoweza kutibika, elimu yetu bado ni duni, watumishi wetu wa umma bado
hawalipwi vizuri na wamevunjika moyo, huduma za maji na umeme vijijini bado ni duni, vifo vya akina mama na watoto bado viko juu.
Sarafu yetu inazidi kuporomoka, imeshuka kwa karibu asilimia ishirini ikilinganishwa na thamani ya dola ya Kimarekani! Jambo ambalo limesababisha
kupanda katika bei ya vitu vinavyoagizwa nje ya nchi na kufanya mfumuko wa bei ambao mwaka 2011 ulikuwa asilimia 20 ukashuka mpaka asilimia 4 ,
Juni 2015, upande tena mpaka asilimia 6.4 jambo ambalo limechangiwa pia na kupanda kwa vyakula.
Waheshimiwa wabunge mnaingia bungeni Tanzania ikiwa na tatizo kubwa sana la ajira, takwimu zikionyesha kwamba karibu nguvu kazi ya vijana
800,000 huingia sokoni kila mwaka, soko ambalo halina ajira kwa ajili yao! Hili ni tatizo kubwa sana kwa taifa kama Tanzania ambalo vijana wake wengi
wametegemezwa kuwa mara wamalizapo vyuo (ambazo hivi sasa ni vingi kila kona ya nchi)  kutakuwa na ajira za kuwapa.
Nawaandikieni barua hii kuwakumbusheni ndugu zangu juu ya jukumu kubwa mlilonalo kwa taifa na watu wenu, hakika haiko sababu ya ninyi kusherehekea
kuwa wabunge, kwani ushindi wenu ndiyo mwanzo wa kazi kubwa mliyonayo mbele, ambayo kwa mtu mwenye uzalendo wa kweli kwa taifa lake ubunge
ni mzigo. Najua mmeingia Bungeni kwa kupitia vyama mbalimbali, wengine mmeteuliwa, najua mnazo tofauti mbalimbali, zikiwemo za dini, rangi, kabila
na itikadi, nawaombeni sasa muweke tofauti zenu zote pembeni na kusimama pamoja kama wawakilishi wa watu ili kuisimamia Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania vyema iweze kutimiza majukumu yake.
Kuendelea kusimama na U-CCM, U-Chadema, U-Cuf, U-NCCR MAGEUZI, hakika hakutaisaidia lolote Tanzania yetu na watu wake, hivi sasa ninyi ni
wawakilishi wa Watanzania, simamieni maslahi ya watu wa taifa hili na maslahi ya taifa kwa ujumla wake.
Mnapoingia bungeni katika kipindi hiki ambacho taifa letu linakabiliwa na hali ngumu ya uchumi, kukiwa hakuna fedha za kutosha kujiendesha,  si
jambo jema hata kidogo kuendelea kugawanyika, umoja peke yake ndiyo utaweza kubadilisha mambo. Najua ninyi nyote ni wazalendo kwa taifa lenu,
basi uonyesheni uzalendo wenu kwa vitendo ili kuhakikisha uwepo wenu Bungeni kwenye Bunge la 11 unakuwa ni wa kihistoria, wengi wenu ni vijana,
matarajio yangu ujana, elimu na vipaji mlivyonavyo mtavitumia vizuri katika kuhakikisha vipaumbele vya taifa hili vinaandaliwa vyema kwa faida ya
waliopo na watakaofuata baada ya sisi.
Nasi tulioko huku nje ya Bunge hatutawaachia mzigo huu peke yenu, tutatimiza wajibu wetu kama Watanzania wawajibikaji. Tutapiga kelele kila
tutakapoona mambo hayaendi sawa, ufisadi unafanyika hadharani na rasilimali za taifa hili zinatumiwa na watu wachache kwa faida yao wao na familia
zao, huu kwetu utakuwa ni uzalendo kwa taifa ambalo tumeapa kulitetea wakati wote na kuvitetea vyama  vyetu pale tu vinapostahili.
Tanzania inasonga mbele, ilipo leo ni bora kuliko ilikokuwa jana, kama uchumi wetu ukiendelea kukua jinsi unavyokua kwa kasi, nina uhakika tutawapita
waliokuwa mbele yetu wakiwa wamekaa! Hili halitakuja kama zawadi bali matokeo ya matendo yetu mema tutakayoyafanya, ninyi Bungeni na sisi huku
nje ya Bunge, sote tuna wajibu wa kujenga taifa letu. Baada ya kusema haya niwatakieni bunge jema lenye mafanikio na nimtakie Mheshimiwa Spika Job
Ndugai hekima na Busara za kuliendesha bunge hili vizuri, vivyo hivyo kwa msaidizi wake, pia waziri mkuu wetu mpya ambaye ni msimamizi wa shughuli
zote za serikali Bungeni, namtakia kila la kheri.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu libariki Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wabariki wabunge wote na wape moyo wa kizalendo na hekima za kuwafikiria wananchi wa taifa hili katika maamuzi yao.

Wasalaam,
Eric Shigongo James
………………………………………..
BARUA KALI

Leave A Reply