Bayo Na Imbori – 18

Wakati Bayo akitoweka katika mazingira ya kutatanisha kwenye maficho ya Kundi la Kid Can Kill huko Kimara, baada ya kufikishwa Marekani na Dickson, mpenzi wake Imbori aligoma kufanya chochote kile ikiwemo kula, kuoga na hata kubadilisha nguo, muda wote akawa mtu wa kulia, jambo lililomchanganya zaidi Dickson.

Kipindi hayo yote yanaendelea msichana Josephine Carlos, aliyewahi kuwa mpenzi wa Dickson siku za nyuma kabla ya kupotezana kutokana na kujikita kwake kwenye masomo anarudi Marekani kutoka India alikokuwa, baada ya kufika anapanga kumtafuta Dickson kwa njia yoyote ile ili amrudishe kwenye himaya yake, wawe wapenzi kama ilivyokuwa kabla.

SONGA NAYO…

KAMA yalivyokuwa mawazo yake, Josephine aliianza haraka sana kazi ya kumtafuta Dickson ambapo baada ya kufanya upelelezi wake alielekezwa nyumbani kwa kijana huyo, akaenda akiwa na matumaini makubwa ya kuirejesha furaha yake iliyokuwa imepotea kwa muda mrefu.

“Sijui itakuwaje nikikutana na Dickson!” Josephine aliwaza kila wakati lakini ilikuwa vigumu kuipata picha halisi.

Alizidi kukanyaga mafuta ya gari lake aina ya Mercedes Benz akielekea nyumbani kwa Dickson huku akikatiza katika mitaa hiyo ya Martin Ruther King Block A, hatimaye akafika.

“Habari, naitwa Josephine.” Alijitambulisha mbele ya mwanamke mzee wa Kiafrika, mrefu na mwembamba.

“Nzuri, mimi ni Catherine, nikusaidie nini?”

“Nahitaji kumuona Dickson?”

“Una mihadi naye?”

“Hapana.”

“Hahitaji kuonana na mtu yeyote.”

“Haiwezekani ni lazima nimuone.”

“Dada naomba unielewe hilo ndilo agizo la bosi wangu!”

“Haliwezi kufanya kazi kwangu, kamwambie, Josephine mpenzi wake nimekuja.”

“Subiri…”

Baada ya kutamka maneno hayo, Madam Catherine aligeuka na kufunga mlango nyuma yake kisha akatembea hadi alipokuwa Dickson, dakika mbili zilitosha kurudi alipokuwa Josephine.

“Karibu ndani.”

“Asante.”

Josephine alimfuata nyuma Madam Catherine kuelekea alipokuwa Dickson, alipokaribia na kumuona kijana huyo Josephine alijikuta akipata furaha ya ajabu, akaanza kumkimbilia Dickson lakini kilichomshangaza, kijana huyo hakuonesha ushirikiano wowote ule, alikuwa amekaa akimtazama kama televisheni, hata alipomfikia na kujaribu kumkumbatia Dickson alikuwa anamuangalia tu.

“Dickson, ni mimi Josephine, umenisahau mara hii?”

“Nakukumbuka umekuwa mdada mkubwa.”

“Mbona huoneshi kunifurahia?”

“Karibu, siko tu vizuri.”

Ukweli ni kwamba lilikuwa jambo gumu kwa Josephine kuamini juu ya mapokezi hayo aliyoyapata kutoka kwa Dickson kijana aliyeishi muda wote ndani ya akili na moyo wake.

Mategemeo aliyokuwa nayo kabla hawajakutana ilikuwa ni kupokelewa kama Malkia Elizabeth atembeleapo taifa lolote duniani, lakini ilikuwa tofauti, Dickson hakuwa na furaha kabisa jambo lililomfanya abubujikwe na machozi.

Kwa upande wa Dickson alielewa ni kwa nini msichana huyo alihisi vibaya kutokana na mapokezi hayo aliyomuonesha, lakini ukweli ni kwamba hakuwa na namna ya kuilazimisha furaha ambayo hakuwa nayo, moyo wake ulikuwa katika maumivu makali yaliyosababishwa na penzi la Imbori.

Wakiwa mahali hapo wanaendelea na maongezi, taratibu Josephine alianza kuisikia sauti nzuri ya msichana akiimba, kwa jinsi ilivyosikika ilionesha msichana huyo alikuwa katika majonzi, Josephine akaamua kumuuliza Dickson juu ya kilichokuwa kinaendelea nyumbani kwake, kijana huyo alikosa majibu ya kumjibu.

“Au umeshaoa Dickson?”

“Hapana!”

“Huyo anayeimba ni nani?”

“Unataka kumfahamu ili iweje?”

“Basi tu, nijue anakuhusu vipi!”

“Siyo kilichokuleta!”

Josephine hakuweza kukubaliana kabisa na majibu hayo ya Dickson aliamua kuinuka na kuanza kuelekea kule sauti ilipokuwa inasikika, Dickson alijaribu kumuita bila mafanikio, ikambidi naye ainuke na kuanza kumfuata nyuma.

“Nataka nimfahamu huyo anayeimba?” Josephine aliongea akiongeza kasi ya kutembea.

Baada ya kufika kwenye chumba hicho sauti ilipokuwa inasikika, aliusukuma mlango kwa nguvu na kuingia ndani, alipofika huko hakuyaamini macho yake, alimkuta msichana mchafu, mwenye nguo zinazotoa harufu akiwa amelala kwenye malumalu, analia na kuimba kwa hisia sana.

Je, b aada ya Josephine kumuona msichana huyo alifanya nini? Bayo je, alifanikiwa vipi kutoroka kwenye maficho ya Kundi la KCK? Usikose kufuatilia wiki ijayo.


Loading...

Toa comment