Bayo Na Imbori – 19

Bayo anatoroka kwenye maficho ya Kundi la KCK katika mazingira ya kutatanisha, nchini Marekani Imbori aligoma kufanya chochote kile ikiwemo kula, kuoga na hata kubadilisha nguo, muda wote alikuwa mtu wa kulia tu, jambo lililozidi kumchanganya Dickson aliyempeleka huko bila ridhaa yake.

Upande wa pili Josephine Carlos aliyewahi kuwa mpenzi wa Dickson anafika nyumbani kwake, akiwa hapo anasikia sauti ya msichana akiimba, baada ya kung’ang’ania kwenda kumuona anashindwa kuelewa huyo alikuwa nani na kwa nini alikuwa katika hali hiyo ya kuchakaa kuliko kawaida.

TAMBAA NAYO…

HALI aliyokuwa nayo Imbori ilimshangaza sana Josephine, akajikuta anashika pua kutokana na harufu kali aliyokuwa anaihisi ndani ya chumba hicho, pia maswali mengi yaliendelea kufukuzana akili mwake juu ya msichana huyo.

“Dickson huyu ni nani?” aliuliza.

“Ni msichana ninayempenda.”

“Unampenda? Mimi je? Dickson unanishusha hadhi kiasi cha kumpenda msichana mchafu namna hii, tena Mwafrika?”

“Huo ndiyo ukweli.”

Maneno ya Dickson kwa Josephine yalikuwa mfano wa chuma cha moto kwenye mwili wa binadamu, msichana huyo alihisi uchungu kupindukia, hakupenda kuamini maneno hayo aliyasikia kutoka kwa Dickson, akajikuta anashindwa kuvumilia kwa kuanza kuangusha kilio, akatoka ndani ya nyumba hiyo kwa kukimbia hadi nje lilipokuwa gari lake, akaliendesha kwa kasi kurudi nyumbani kwao.

Barabarani kote Josephine alikuwa analia kwa uchungu, chuki dhidi ya msichana huyo ikapanda kifuani kwake, akasema haiwezekani kunyang’anywa kidume na msichana wa aina ya aliyemuona, siku mbili baadaye alianza mazoea ya siri na Madam Catherine, wakapanga kumuua Imbori kwa sumu!

Zoezi zima la kumuua Imbori lilipangwa kwa siri na tahadhari kubwa ambapo baada ya Josephine na Catherine kujadiliana juu ya hilo walipanga kulifanya kwa kutumia sumu ya Arsenic Trioxide.

Sumu kali ya ungaunga yenye mchanganyiko wa madini ya Arsenic na Oxijeni, kwa matumizi ya kuanzia gramu 10 ina uwezo wa kumuua binadamu taratibu kuanzia masaa 36 na kuendelea.

Waliamini kutokana na hali aliyokuwa nayo msichana huyo kusingekuwa na maswali juu ya kifo chake, hata hivyo Josephine alimuahidi Madam Catherine kumpa fedha nyingi ikiwa atalifanikisha zoezi hilo.

“Imbori,” Madam Catherine aliita akiwa ameshika sahani ya chakula mkononi. Imbori hakuitika alikuwa amelala chini huku analia tu.

“Amka mdogo wangu ule, utaendelea kuwa katika hali hiyo mpaka lini?”

“Acha tu nife madam, hakuna sababu ya kuishi bila Bayo.”

“Usiseme hivyo, mimi nimeamua kukusaidia.”

“Kivipi?”

“Kula kwanza halafu nikwambie.”

“Niambie kwanza!”

“Nataka kukutorosha urudi Afrika, nakuonea sana huruma.”

“Kweli?”

“Kabisa!”

Baada ya kusikia hivyo Imbori alijiinua pale chini alipokuwa amelala, akakaa ili ale chakula akiamini mwanamke huyo mwenye umri wa yeye kuthubutu kumuita mama alipania kweli kumsaidia kutokana na mateso aliyokuwa anayapata.

Aliichukua sahani ya chakula baada ya kukaa kitako kisha akanawa na kupeleka mkono kwenye sahani ili aanze kula maana hakuhitaji kabisa kutumia kijiko.

“Kuna juisi pia hapa.” Madam Catherine alimsogezea pia juisi ya chungwa.

“Sawa mama.”

Kutokana na njaa aliyokuwa anaihisi, Imbori hakuhitaji kuremba, harakahara alibumba tonge la wali na kuanza kulitia mdomoni, moyoni madam Catherine alikuwa na furaha isiyo ya kawaida, alifahamu baada ya kumaliza zoezi hilo Imbori angekufa na yeye angeuaga umaskini.

“Catherine?” Mara sauti ilisikika ikiita.

Akiwa analipeleka tonge la wali mdomoni, Imbori aliisikia sauti hiyo na kugundua kuwa ilikuwa ya Dickson, ghafla hamu ya kula chakula ikapotea, akalirudisha tonge kwenye sahani na kuiweka chini.

“Mbona umeweka chakula chini?”

“Sijisikia kula tena!”

“Kwa nini?”

“Basi tu.”

“Kula hata kidogo!”

“Siwezi Madam.

“Hata tonge mbili tu!”

“Nimesema siwezi.”

Madam Catherine alihisi hasira zisizo za kawaida, kama isingekuwa kuisikia sauti ya Dickson iliyomaanisha uwepo wake huenda angemrukia msichana huyo na kumuua kwa kutumia mikono yake.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.


Loading...

Toa comment