The House of Favourite Newspapers

Bayo Na Imbori – 20

0

Kutokana na wivu wa kimapenzi Josephine anapanga mpango wa siri wa kumuua Imbori. Kila kitu kinakwenda sawa, Madam Catherine anaingia kwenye chumba cha Imbori na chakula chenye Sumu na kumlaghai Imbori kula, wakati anataka kula anaisikia sauti ya Dickson jambo lililomfanya ahairishe zoezi hilo, Madam Catherine alikasirikika sana.

SONGA NAYO…

AKIWA katika maficho ya Kundi la Kid Can Kill (KCK), yaliyopo Kimara, jijini Dar es Salaam Bayo alirejewa na fahamu zake kutokana na kiubaridi kilichokuwa kinapuliza katika usiku huo pia alikuwa anahisi uchovu kuliko kawaida. Jambo lililomshangaza zaidi ni kuhusu mahali alipokuwa, alijiuliza alifika kwa namna gani au alifikishwa na nani lakini hakuweza kupata jibu.

Kwa shida sana alianza kujaribu kuvuta kumbukumbu zake, akakumbuka mara ya mwisho yeye na mkewe Imbori walikuwa katika Kituo cha Frank’s Centre of Orthopaedic and Neurological Surgery (FCONS) walikopokea taarifa za kifo cha mtoto wao lakini baadaye walitekwa na watu waliokuwa wamevalia mavazi ya kidaktari. Kumbukumbu zikaishia pale alipopigwa kwa kitu kizito kichwani kisha giza jeusi likatanda mbele yake.

Kumbukumbu hizo ndizo zilizomshtua, akazidi kujiuliza maswali mengi bila kuyapatia majibu, swali lililompa shida zaidi ni kuhusu wapi alikuwa mkewe Imbori.

Bila kupoteza muda akifahamu hakuwa katika eneo salama, Bayo alijiinua kwa shida kisha kwa tahadhari kubwa akaanza kutembea kuelekea nje, alipofanikiwa kutoka ndani ya pagale hilo alitokomea mitaani.

Muda mrefu ulipita Bayo akitangatanga katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam utadhani mwendawazimu bila kufahamu aelekee wapi, mpaka giza lilipoingia alikuwa tayari amekwishafika maeneo ya Mtaa wa Ubungo, akatafuta sehemu na kulala kwa ajili ya kulipisha giza la usiku huo akipanga siku inayofuata kuanza safari ya kumtafuta mkewe Imbori.

*     *     *

Madam Catherine alitoka ndani ya chumba alichokuwa Imbori huku mkononi ameshika sahani yenye chakula chenye sumu pia alikuwa anaonekana mwenye wasiwasi kiasi fulani.

“Ulikuwa unafanya nini humo ndani?” Dickson alimuuliza baada ya kugonganisha macho yao.

“Nilimpelekea chakula Imbori.”

“Amekula?”

“Hapana.”

“Kwa nini?”

“Basi tu, hataki.”

“Umejaribu kumlazimisha?”

“Sana, lakini hataki.”

Dickson aliachana na mwanamke huyo, akaingia kwenye chumba alichokuwa Imbori, ukweli roho yake ilimuuma kutokana na hali aliyomkuta nayo msichana huyo, Imbori alionekana katika hali mbaya sana kiasi kwamba hata kulia alikuwa anashindwa kutokana na njaa kali aliyokuwa anaihisi.

“Kwa nini hutaki kula mama?” Dickson aliinama, akamuuliza Imbori huku machozi yakianza kumbubujika kwa kumuonea huruma.

“Siwezi kula, niache tu nife.”

“Haiwezekani, niambie nikufanyie nini?”

“Nirudishe nyumbani, nikaonane na Bayo.”

“Basi naomba ukubali kula halafu nikurudishe.”

Dickson alitumia nguvu kubwa sana kuhakikisha msichana huyo anakubali kula chakula ili kuyaokoa maisha yake maana ukweli ni kwamba hakuwa katika hali nzuri hata kidogo.

Baada ya kumshawishi kwa muda mrefu huku akimdanganya kumrudisha Afrika, Imbori alikubali kula, jambo lililomfurahisha sana Dickson, akawaza badala ya kusafiri kwenda Afrika, ampeleke katika nchi zenye sifa nzuri ya utalii wakafurahie maisha, ambapo katika siku iliyofuata taratibu za safari zilianza.

*     *     *

Taarifa aliyoipokea kutoka kwa Madam Catherine ya kushindikana kwa mpango wa kumuua Imbori ilimkasirisha sana Josephine, lakini hakuwa na budi kukubaliana na hali halisi, jambo alilolifanya ni kuanza upya kushirikiana na mwanamke huyo kupanga mpango mwingine ili kuhakikisha anampoteza duniani Imbori, abaki analifurahia penzi la kijana aliyempenda sana, Dickson.

“Dickson ameniambia wanasafiri,” Madam Catherine alikuwa anaongea kupitia simu yake ya mkononi.

“Kwenda wapi?”

“Barbados.”

“Kweli?”

“Ndiyo”

“Lini?’

“Kesho.”

“Saa ngapi?”

“20:15.”

“Sawa, hakikisha unanitaarifu kila hatua.”

“Usijali.”

Baada ya maongezi hayo, Madam Catherine alikata simu.

Taarifa aliyoipokea kutoka kwa Madam Catherine ilimtibua sana Josephine, akauhisi mwili wake ukichemka kuliko kawaida, hasira za kumuua Imbori zikazidi kuongezeka, akaamua kuwasiliana na kundi la kihalifu aliloamini lingeweza kumfuatilia Dickson hadi nchini Barbados na kumuua Imbori.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply