The House of Favourite Newspapers

Bayo Na Imbori – 21

0

Zoezi la kumuua Imbori kwa kutumia sumu ya Arsenic Trioxide iliyochanganywa kwenye chakula linagonga mwamba, Josephine anapanga mpamgo mwingine, baada ya kudokezwa na Madam Catherine kuwa Dickson alikuwa ana safari ya kwenda nchini Barbados pamoja na Imbori, alilitafuta kundi la wauaji ambao aliwataka kwenda kuikamilisha kazi hiyo hukohuko.

TAMBAA NAYO…

TARATIBU za safari zilipomalizika, Dickson aliwaaga watu wake wa karibu akiwemo Richard Seth mhisani mwenza wa jarida la BIB  lililokuwa linachapisha habari za burudani na picha za wanamitindo maarufu kutoka Afrika, kila mwaka.

“Mbona ni safari ya ghafla?” Richard alimuuliza.

“Ni kweli, mapenzi yananiendesha kaka.”

“Unatakiwa kuwa makini.”

“Sawa, ngoja nijaribu njia hii nione kama itasaidia kumshawishi Imbori kuwa mpenzi wangu.”

“Mungu akutangulie.”

“Asante.”

Saa za safari zilipowadia Dickson na Imbori walielekea hadi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Compton, walikopanda ndege ya kuelekea jijini Briggeton nchini Barbados.

Wakiwa ndani ya ndege Imbori alionekana kuwa mwenye furaha sana siku hiyo, jambo ambalo Dickson alilielewa lilisababishwa na nini, lakini ndege ikiendelea kuchana mawingu kuna jambo moja lilionekana kumpa wasiwasi Dickson.

“Kwa nini hao watu wanatuangalia sana?” Dickson alimuuliza Imbori akimuonesha wanaume wawili wa kizungu waliovalia suti nyeusi na tai.

“Siwezi kuelewa.”

“Nina mashaka nao.”

“Kwa nini?”

“Basi tu, macho yao siyo ya kawaida.”

Safari iliendelea, mwishowe baada ya saa 7 ndege hiyo Boeing 654AD ya Shirika la Anga la Mason Luxuiry ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Grantley Adams, nje kidogo ya jiji la Briggeton.

Baada ya kushuka na kufanyiwa ukaguzi, Dickson alishangaa kuona bado wale wazungu wawili waliokuwa wanawaangalia kwa macho ya hatari ndani ya ndege wakiendelea kuwatazama, lakini baada ya dakika chache hakuwaona tena na hakuelewa walipotelea wapi, Dickson aliamua kulipotezea jambo hilo, akakodi usafiri binafsi kuelekea katika Hotel ya Good Time iliyopo ndani ya Fukwe za Memsi, huku akimdanganya Imbori kuwa wangechukua mapumziko hapo kabla ya kuelekea Afrika.

*   *   *

“Msaaada… msaada jamani… msaada..!” Zilisikika kelele za mwanaume wa kizungu, mfupi aliyekuwa amevaa pensi huku akiwa hana viatu miguuni.

Watu wote waliokuwa katika ufukwe huo wa Memsi walianza kukusanyika akiwemo Dickson, ndani ya muda mchache walijaa na kumzunguka mwanaume huyo aliyejitambulisha kwa jina la Thomas.

“Mwanamke wangu ametekwa, nimemuona ameingizwa kwenye gari jeusi lililotoweka muda si mrefu,” mwanaume huyo aliwaeleza.

Watu wote walistaajabishwa na hizo taarifa, haraka sana waliomba msaada kwenye uongozi wa ufukwe huo, ukaahidi kuwafuatilia maharamia hao hadi kuhakikisha wanampata huyo mwanamke.

“Mwanamke wako anafanana vipi?” Dickson alimuuliza Thomas baada ya kumkosa Imbori.

“Ni mweusi, mrefu na si mwembamba wala mnene.”

“Mbona huyo yuko kama wangu, maana na mimi simuoni!”

Kauli ya Dickson iliwafanya watu wazidi kupigwa butwaa, walishindwa kuelewa nini kilikuwa kinaendelea mahali hapo lakini walifahamu kuwa kulikuwa na tatizo kubwa ambalo lingesababisha kuondoa maisha ya watu wengi, kabla ya kuchukua maamuzi mengine waliamua kumtafuta kwanza Imbori ufukweni hapo.

*   *   *

Josephine Carlos alikuwa amedhamiria kumuua Imbori kutokana na wivu wa mapenzi aliokuwa nao dhidi ya Dickson, ambapo kutokana na taarifa alizozipokea kutoka kwa Madam Catherine kuwa Dickson na Imbori wangesafiri hadi Barbados, alifanya mawasiliano na maharamia wa kundi la Nato, walioelewana naye kuifanya kazi ya kumuua Imbori kwa dola za Kimarekani 20,000.

“Mtafanikiwa kweli?” alimuuliza Conred Cessy kiongozi wa kundi hilo, kumsaili.

“Hiyo kazi ndogo sana kwetu.”

“Sawa.”

Baada ya kufanyika malipo ya awali, Gabriel na Sudan wa kundi la Nato walisafiri kwenye ndege moja na kina Dickson hadi Barbados, wakaendelea kufuatilia mienendo ya watu hao mwisho wa siku wakapanga vyumba katika hoteli moja ya Good Times, dhumuni lao kubwa likiwa kumteka Imbori na kwenda kumuulia katika eneo ambalo hakukuwa na watu.

Kila hatua vijana hao walionekana kuifanya kwa umakini sana. Siku ya kwanza ilikatika bila kulifanikisha zoezi lao, lakini siku iliyofuata walipanga kufanya juu chini kulikamilisha maana hawakupenda kabisa kupoteza muda wakiwa jijini hapo Briggeton.Je, nini kitaendelea? Aliyetekwa ni Imbori? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply