Bayo Na Imbori – 22
Josephine anazidi kupanga mipango ya kumuua Imbori, ili kuikamilisha azma hiyo anawatafuta vijana wawili kutoka Kundi la Kigaidi la Nato aliowaahidi malipo ya dola za Kimarekani 20,000 kama wakilifanikisha zoezi hilo, baada ya maelekezo na malipo ya awali vijana hao waliwafuatilia Bayo na Imbori hadi nchini Barbados bila wao kufahamu.TAMBAA NAYO…
KULIPOPA-MBAZUKA Gabriel na Sudan ndiyo walikuwa wa kwanza kuamka kabla ya Dickson na Imbori, kwa umakini wa hali ya juu waliendelea kupanga mipango kwa kutumia mbinu walizozifahamu zitawasaidia kufanikisha kumteka Imbori.
Saa zikazidi kukatika, ambapo majira ya saa sita mchana vijana hao walikuwa wamekaa karibu kabisa na mahali walipokaa kina Dickson mgahawani wakipata chakula cha mchana, walikuwa wanawafuatilia karibu kila hatua, kifo cha Imbori kwao kilimaanisha dola za Kimarekani 20,000 walizoahidiwa na Josephine ikiwa wataikamilisha kazi hiyo.
Kwa upande wa Dickson na Imbori hawakuwa na habari yoyote juu ya kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia, ingawa mara kadhaa Dickson alionekana kuwa na wasiwasi kila alipowaona vijana hao wawili hasa kutokana na namna walivyokuwa wanawatazama lakini hakujali sana, aliamini wasingeweza kumfanyia lolote maana hata yeye aliiweza michezo ya kimafia.
“Sijihisi vizuri,” Imbori alimwambia Dickson.
“Kivipi?”
“Nahisi kichefuchefu!”
“Mh! Pole, hujakipenda chakula?”
“Hapana, sijui tatizo ni nini!”
Baada ya kauli hiyo Imbori aliinuka na kuanza kutembea kwa kasi kuelekea maliwatoni maana alikuwa anahisi kutapika, Dickson alianza kumfuata nyuma, lakini alipopiga tu hatua chache alisikia sauti kutoka nyuma yake ikimuita, alipogeuka alisogelewa na mmoja wa wale wazungu waliokuwa wanawatazama sana yeye na Imbori, lakini kilichomshangaza mwenzake hakumuona.
“Tunafahamiana?” Dickson alimhoji Gabriel.
“Ndiyo, hunikumbuki?”
“Hata kidogo.”
“Inawezekana, muda mrefu umepita tangu tukutane, lakini kifupi nimekufahamu kupitia jarida lako la BIB.”
“Oke, hapo sawa.”
Gabriel aliamua kumsimamisha Dickson makusudi kabisa maana wakati huo mwenzake Sudan alimfuatilia Imbori kule mariwatoni alikokuwa amekwenda, alipotazama huku na huko na kuona hakuna mtu, alimvamia msichana huyo kwa shambulio moja la kiufundi lililomsababisha azimie kisha akambeba na kutoka naye nje kupitia lifti, akampeleka hadi kwenye gari walilolikodi kwa ajili ya kazi hiyo kisha akamtumia sms Gabriel kumtaarifu aliimaliza kazi.
Baada ya kupiga stori mbili tatu na Gabriel, Dickson alielekea kwa kasi ya ajabu hadi maliwatoni alikomuona Imbori akielekea, alipofika alishangazwa kwa kutokumuona lakini akiendelea kumtafuta alishtushwa na kelele kutoka nje za mtu aliyekuwa anaomba msaada aliyedai mkewe alitekwa na watu wasiojulikana.
Dickson aliamua kukimbia moja kwa moja hadi nje walikoelekea watu wengi, baada ya kufika na kusikiliza maelezo ya jamaa huyo na baadaye kumtafuta Imbori hakumuona.
Hali hiyo ilizidisha sintofahamu, kwa kitendo cha haraka uongozi wa hoteli hiyo ulitoa taarifa kwenye vyombo vya usalama ili wawafuatilie watekaji lakini hakuna walichoambulia, wauaji walitokomea kusikojulikana.
Baadaye mke wa yule mzungu alikutwa amefia chooni, baada ya uchunguzi wa madaktari walibaini alikufa kwa shinikizo la damu baada ya presha yake kupanda juu ghafla, kilichomsababisha mumewe kupiga kelele akidai ametekwa yalikuwa ni mavazi ya mkewe kufanana na aliyokuwa amevaa Imbori, lakini haikuwa kweli alitekwa zaidi ya Imbori, taarifa hiyo ilizidi kumchanganya Dickson.
* * *
“Hapa kazi tu!” Sudan aliongea huku uso wake ukichanua tabasamu pana.
“Kama kawaida yetu,” Gabriel alimjibu akionesha kuwa na furaha kupindukia pia.
“Lazima tuisimamishe Marekani.”
“Kweli kabisa, pesa tutakazopata si mchezo.”
Gari hiyo waliyokuwa wameikodi Bugatti Veyron ilizidi kusaga lami katika mitaa ya jiji hilo la Briggeton hadi ikatoka nje kabisa ya mji huo walikoshika barabara ya St. Stephano wakaelekea hadi jirani na yalipokuwa maporomoko ya Jidawi yaliyopakana na Msitu wa Keneth Bull, ulioaminika kuwa na wanyama wakali wakiwemo nyoka wakubwa kama vile Chatu, Swira, na Kipiribao.
“Huku hawezi kupona,” Sudan alisema.
Kwa tahadhari ya hali ya juu walimtoa Imbori aliyekuwa bado amepoteza fahamu kwenye buti la gari hilo kisha wakampeleka hadi mahali walipoamini watu wasingeweza kufika kisha wakamlaza wakiamini kabisa ni lazima ataliwa na wanyama wakali.
“Wasalimie kuzimu.” Sudan aliongea akitema mate juu ya Imbori.
“Twend’zetu,” Gabriel alimwambia, wakalifuata gari lao, wakaondoka mahali hapo wakimuacha Imbori peke yake akiwa hajitambui!
Je, nini kitaendelea? Huo ndiyo mwisho wa Imbori? Vipi kuhusu Bayo? Usikose wiki ijayo.