Bayo Na Imbori -26
Utajiri ni kitu alichokuwa anakihitaji Bayo mbapo baada ya kwenda kwa mganga Matiku na kutekeleza mitihani yote aliyopewa ili apate pesa ikiwemo kumuua rafiki yake Samson, mambo yalikwenda sawa akafanikiwa azma yake ya kupapa utajiri.
Songa nayo.
Tofauti na ilivyokuwa awali, alipofika nyumbani kwake hakukuta tena pesa zimesambaa kila mahali ndani ya chumba chake zikiwa ndani ya mifuko mitano mikubwa ya salfeti yenye rangirangi huku imepangwa pembeni imetulia.
Bayo alihisi moyoni mwake amani kupindukia, siku ya pili yake alifungua kibanda kidogo cha kuuza mafuta ya taa kilichofumuka kwa kasi kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele.
Baada ya mwaka mmoja akawa miongoni mwa matajiri wakubwa Tanzania aliyesemwa kila kona watu wakimmwagia sifa kutokana na historia yake ya kuanza na mtaji mdogo wa kuuza mafuta ya taa mpaka kufikia hatua ya kumiliki vituo vya mafuta zaidi ya nane jijini Dar es Salaam. Hakuna aliyefahamu nyuma ya utajiri wake kulikuwa na nini!
Jambo pekee lililowashangaza wengi, japo Bayo alikuwa na pesa za kumwaga lakini hakuna aliyewahi kumegewa ubuyu juu ya uhusiano wake wa mapenzi, watu wengi wakiwemo waandishi wa habari walijitahidi kufuatilia lakini waliangukia pua, walipojaribu kumuuliza alikuwa mgumu kuzungumzia hilo, kauli yake ilikuwa moja tu, “Sipendi kuweka wazi maisha yangu binafsi.”
Siku zilizidi kusonga mbele, baada ya kuhakikisha ameimarisha biashara zake ndani ya miaka miwili kwa kuwaajiri watu walioisimamia miradi yote, Bayo alipanga kuianza shughuli yake ya kumtafuta Imbori, sehemu ya kwanza aliyoiwazia ilikuwa ni katika Kituo cha FCONS (Frank’s Centre of Orthopaedic and Neurological Surgery).
* * *
Baada ya kutelekezwa katikati ya Msitu wa Keneth Bull na vijana wa Kundi la Nato, Imbori aliinuka, akaanza kujivuta taratibu huku akilia kwa uchungu, wakati huo alifahamu hakuwa na muda mrefu wa kuishi, lazima angekufa kwa kuliwa na wanyama wakali.
Aliendelea kusogea hadi mbele kabisa ambapo wakati huo giza lilikuwa limeanza kuchomoza na sauti za ajabu zilikuwa zimeanza kutanda kila kona, hofu ya kuliwa na wanyama wakali ilizidi kuongezeka.
Imbori hakukata tamaa, japo alikuwa anaogopa alizidi kusogea kwa tahadhari, akizidi kuvipangua vichaka ghafla aliiona michirizi ya damu mbichi kutoka umbali kidogo na mahali alipokuwa, moyo wake ukaanza kudunda kwa nguvu, kengele ya hatari ikagonga kichwani mwake akafahamu huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
Akazidisha tahadhari lakini akizidi kuangali damu hiyo ilitoka mahali gani bila kutegemea aliona maiti ya kijana wa Kizungu aliyeonekana kuuawa muda mfupi uliopita, pembeni yake kulikuwa na begi pamoja na tochi iliyokuwa inawaka, kwa ujasiri aliisogelea maiti hiyo akachukua tochi aliyofahamu ingemsaidia kisha akaanza kukimbia kwa nguvu zake zote.
Bila kufahamu kukimbia kwake kulifanya awatibue wanyama walioishi msituni hapo, kabla hajafika mbali kundi kubwa la wanyama wakali lilitokea mbele yake.
Imbori alisimama kwa kitendo cha ghafla akiuhisi mwili wake kumsisimka kuliko kawaida, bila habari yoyote haja ndogo ilimtoka, akaanza kutetemeka bila kufahamu afanye nini, alichokuwa anakiona kilikuwa ni kifo cha kikatili huku akifahamu mazishi yake yangekuwa tumboni mwa wanyama hao.
* * *
Kupotea kwa Imbori kulimchanganya sana Dickson kiasi kwamba akawa mtu wa kulia muda wote kama mtoto mdogo, mara kadhaa alijiuliza nani alihusika na utekaji wake lakini hakuweza kupata jibu.
Kwa kushirikiana na uongozi wa Hoteli ya Good Times walitoa taarifa kwenye vyombo vya habari na usalama, matangazo yakawekwa kila kona yaliyoambatanishwa na dau nono kwa mtu au watu ambao wangefanikisha kupatikana kwa msichana huyo.
“Umesikia hilo tangazo?” Sudan alimwambia Gabriel.
“Lipi?”
“Linalomhusu Imbori.”
“Hapana.”
“Kuna dau nono limewekwa kwa watakaofanikisha kumpata.”
“Kuliko dola 20,000?”
“Ndiyo.”
“Shilingi ngapi wameweka?”
“Dola 40,000.”
“kweli?
“Ndiyo.”
Baada ya kujiridhisha kuwa ilikuwa ni kweli dau nono liliwekwa kwa watu watakaofanikisha kumpata Imbori, Gabriel na Sudan walipanga kumsaliti Josephine, japo walikuwa wamekwisha kula pesa yake ya awali walifahamu asingeweza kufanya jambo lolote lile mbele yao.
Wakaamua kurudi katika Msitu wa Keneth Bull wakiwa na lengo la kumtafuta Imbori na kumrudisha mikononi mwa Dickson ili wale kitita hicho cha pesa, kuna wakati walishauriana kuwa wakifanikiwa kukichukua wangemrudishia Josephine pesa zake alizowapa.
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

