The House of Favourite Newspapers

Beki KMC aliyeipa Yanga mabao matatu, afunguka

BEKI wa kati wa KMC, Ally Ally amefunguka kuwa haikuwa makusudi kujifunga katika mpira wa krosi uliopigwa na mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu.

 

Beki huyo alijifunga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku beki huyo akidaiwa kurudia kujifunga na kutoa nafasi za kufunga kwa Yanga katika kila mchezo wanaokutana.

 

Beki huyo alijifunga katika mchezo na Yanga, akiwa Stand United msimu uliopita, kisha kufanya kosa akiwa KMC kwenye mzunguko wa kwanza msimu huu, lililopelekea Yanga kupata faulo ya bao la ushindi lililofungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’.

 

Pia alijifunga tena kwenye mchezo wa wikiendi iliyopita, timu yake ikifa 2-1, hii inaonyesha kuwa ameshashiriki kuwapa Yanga mabao matatu hadi sasa.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Ally alisema kuwa anashangazwa na watu kudai imekuwa kawaida yake kujifunga wanapocheza na Yanga, jambo ambalo halina ukweli kwa upande wake huku akiuliza kwa nini hawasemi alivyomdhibiti mshambuliaji wa timu hiyo, Heritier Makambo.

 

“Kwanza sikufanya makusudi kujifunga halafu kwa ule mpira ulivyopigwa na wakati naruka kuokoa kwa bahati mbaya ndiyo ukawa umeingia wavuni lakini halikuwa kusudi langu kufanya hivyo.

 

“Hayo mengine ni makosa ya sehemu ya mchezo halafu suala la sijui nafanya makusudi kuruhusu au kujifunga siyo kweli, mbona hawasemi nimezuia mara ngapi na nimemzuia Makambo asipige vichwa katika ile mechi,” alisema Ally ambaye ni Mzanzibar.

Comments are closed.