BEKI MATATA ANUKIA MAN U

Kalidou Koulibaly

MANCHESTER United imeamua kuwaweka mastaa wake wawili sokoni ili kufungua njia ya kumsajili beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly.

Kwa muda mrefu Manchester United imekuwa inamfukuzia beki huyo wa timu ya taifa ya Senegal. Aliyekuwa kocha wa Manchester United, Jose Mourinho alitaka kumsajili mwanzoni mwa msimu huu wa 2018/19 lakini uongozi wa klabu hiyo uligoma kutoa fedha.

Hata hivyo, kuna taarifa kuwa kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer anamtaka Koulibaly, ambaye anahesabiwa kama miongoni mwa mabeki bora duniani kwa sasa. Kufuatia hali hiyo, Manchester United imeamua kuwaweka sokoni beki Marcos Rojo na kiungo Maroune Fellaini.

 

Manchester United imeamua kuuza wachezaji hao ili kupunguza ukubwa wa kikosi chao na fedha zitakazopatikana waongezee kumnunua Koulibaly, Habari kutokana ndani ya Manchester United zinasema kuwa Solskjaer hajaridhishwa na kiwango cha mabeki wa sasa wa klabu hiyo.

Hata hivyo, Manchester United itapata wakati mgumu kumuuza Rojo kwa kuwa ni majeruhi. Kutokana na hali hiyo, Rojo amerudi kwao Argentina ili kuweza kupata matibabu zaidi. Katika hatua nyingine, Manchester United ipo
tayari kumuuza Fellaini kwa kitita cha pauni milioni 15. Klabu zinazotajwa kutaka kumsajili Fellaini ni pamoja na AC Milan, Porto na Guangzhou Evergrande ya China.

 

Fellaini amekuwa na wakati mgumu tangu ujio wa Solskjaer kutokana na kujikuta anasugua benchi mara kwa mara. Kiungo huyo ameingia kama `sub’ (mchezaji wa akiba) katika mechi sita ambazo Manchester United imekuwa chini ya Solskjaer. Manchester United imepata matumaini ya kumpata Koulibaly kwa kuwa mchezaji mwenyewe anataka kuondoka Napoli.

 

Koulibaly ameuomba uongozi wa Napoli kukubali ikiwa Manchester United watatoa ofa ya kumsajili. Beki huyo anataka kuondoka Italia baada ya kuchoshwa na kashfa za kibaguzi anazokumbana kwenye viwanja ya soka vya Italia. Koulibaly hivi karibuni alipata wakati mgumu wakati timu yake ilipocheza na Inter Milan. Hata hivyo, uongozi wa Napoli unasita kumuuza Koulibaly kwani ni mchezaji tegemeo wa timu

Loading...

Toa comment