Belle 9: Siwezi Kumsahau Masogange
“Upo mbali na Masogange…
Njoo uutulize mtima wange…
Upo mbali na Masogange eh…
Miaka mingi imepita baby, ila mi sijakuona…
Miaka mingi imekatika maa, ila mi sijakuona…
Kile kidonda changu cha mapenzi, moyoni bado hakijapona…
Nitapata afadhali mi, endapo we nikikuona…
Kama warembo mi nawaona wengi, tabia zao mi naona noma…
Najaribu shinda vishawishi, nisije mi kukupa ngoma…
Bado nakupenda wewe, wapi ulipokwenda…
Bado nakupenda wewe, wapi ulikokwenda…”
HII ni sehemu ya mashairi yenye hisia nzito ya Ngoma ya Masogange kutoka kwa Belle 9.
Ni zaidi ya miaka 10 iliyopita tangu ngoma hiyo itoke, lakini bado melodi na midundo yake inasikika, kwani ni miongoni mwa ngoma za zamani (TBT) za Bongo Fleva zinazosikilizwa kwenye mitandao ya kijamii.
Ni kutoka kwa mwanamziki mkali wa RnB Bongo, Abednego Damian ‘Belle 9’.
Kwa kuweka kumbukumbu sawa, Belle 9 na Diamond Platnumz au Mondi, wote walitoka kimuziki kipindi kimoja (mwaka 2009).
Wote walikuwa maandagraundi. Belle 9 akitokea Mji Kasoro Bahari, Morogoro mjini pale Mtaa wa Mafinga. Wengi walianza kutabiri kuwa Belle 9 angekuwa staa mkubwa zaidi kuliko Mondi kutokana na alivyokuwa anakuja vizuri.
Mondi yeye alitokea pale Tandale jijini Dar, mahali palipoaminika wanaishi watu wenye maisha duni.
Belle 9 na Mondi wote walitoka na ngoma kali. Belle 9 alitoka na Sumu ya Mapenzi kisha Masogange ambazo zilimtambulisha vizuri kwenye medani ya Bongo Fleva.
Mondi yeye alitoka na Nenda Kamwambie na Mbagala ambazo naye zilimtambulisha vyema kutokana na maudhui mazuri na melodi zilizojaa ufundi.
Kuna kituo kimoja cha redio kiliwashindanisha Belle 9 na Mondi mwaka 2010, ambapo wasikilizaji walipiga kura za nani zaidi, unajua nini kilitokea? Belle 9 alimgaragaza Mondi vibaya mno. Kipindi hicho Belle 9 alitamba sana aisee!
Baada ya muda fulani wa Belle 9 kuwa juu, ghafla alianza kusuasua na hapo ndipo Mondi alipopenya na kuanza kukimbiza kwa ngoma mfululizo na ushindani wa Mondi na Belle 9 ukabaki kuwa historia. Nini kilitokea? Ni makala ya siku nyingine!
Baada ya Sumu ya Penzi na Masogange, Belle 9 aling’ara na ngoma nyingine kama Wewe ni Wangu, Nilipe Nisepe, Umenitupa, Ladha ya Mapenzi, House Boy, Wanitaka, Burger Movie Selfie, Umefanana Naye, Vitamin Music, Wewe Nami, Listen, Shauri Zao, Amerudi na nyingine kibao (ni zaidi ya 50).
OVER ZE WEEKEND imebonga na Belle 9 ambaye amefunguka mambo mengi ikiwemo kumisi uwepo wa aliyekuwa video vixen katika ngoma yake ya Masogange, marehemu Agness Gerald ‘Masogange’ (RIP) aliyetangulia mbele ya haki Aprili 20, 2018;
OVER ZE WEEKEND: Unazungumziaje mapokeo ya ngoma yako mpya ya Umefanana Naye kwa sababu umekuwa kimya kwa muda mrefu?
BELLE 9: Kwanza ninamshukuru Mungu, mapokeo ya Umefanana Naye yamekuwa mazuri mno na kazi inaendelea kuonekana.
OVER ZE WEEKEND: Baada ya Umefanana Naye, je, nini kinafuata?
BELLE 9: Kifuatacho ni ngoma after ngoma. Hicho ndicho ambacho nimepanga kurudi nacho kwa sababu nilitulia kidogo. Ninawaahidi mashabiki wangu, najua ni wengi mno ndani na nje ya Bongo, hawatasubiri tena.
OVER ZE WEEKEND: Una ladha ya kipekee kwenye miondoko ya RnB. Je, unawezaje kuendelea kubaki kwenye chati?
BELLE 9: Hakuna njia nyingine ya kubaki kwenye chati zaidi ya kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kuheshimu watu ambao wamezunguka muziki wangu, ikiwemo vyombo vya habari na mashabiki wangu.
OVER ZE WEEKEND: Unaitazamaje Bongo Fleva ya sasa ukilinganisha na ya kipindi kile wakati unatoka kimuziki?
BELLE 9: Bongo Fleva ya sasa na ile ya zamani, zote ni nzuri maana kila kipindi lazima kibadilike ili maendeleo yaonekane. Ninafurahia sana muziki wa sasa na ninawaheshimu wasanii wa sasa na hata wa zamani.
OVER ZE WEEKEND: Ni muda sasa tangu Masogange atangulie mbele za haki, je, unamisi nini kutoka kwake kwa sababu wewe ndiye uliyemtambulisha kwenye ustaa?
BELLE 9: Ninamisi vitu vingi sana kutoka kwake na uwepo wake. Alikuwa rafiki mwema na mtu wangu wa karibu. Tulisaidiana sana katika vitu vingi. Naweza kusema siwezi kumsahau Masogange.
OVER ZE WEEKEND: Inasemekana umehama Dar, umehamia Morogoro. Je, ni kweli?
BELLE 9: Si kweli, mimi bado ninaishi Dar. Morogoro kuna familia yangu kwa maana ya wazazi, hivyo lazima niwe nakwenda kwa sababu ni nyumbani na mashabiki wangu wengi wako kule. Hivyo, kwenda kusalimia ni kitu cha kawaida tu.
OVER ZE WEEKEND: Tunajua ulifunga ndoa, lakini ilitawaliwa na usiri mwingi, kwa nini?
BELLE 9: Watu wanaweza kufikiria hivyo kwa sababu sikuitangaza, haikuwa ndoa ya siri maana hata familia yangu ilikuwa inajua na sikutaka kufanya kitu kikubwa sana maana nisingeweza kuhimili gharama. Mimi ni mwanamuziki mkubwa Afrika Mashariki si Morogoro, napenda kufanya vitu kwa kujiridhisha mimi na si watu wengine.
OVER ZE WEEKEND: Vipi unaonaje maisha ya ndoa?
BELLE 9: Maisha ya ndoa ni mazuri, yamenikubali na ninayafurahia sana.
OVER ZE WEEKEND: Vipi familia inaendeleaje na mmejaaliwa watoto wangapi?
BELLE 9: Familia inaendelea vizuri na watoto hawajambo, siwezi kusema nimejaaliwa watoto wangapi.
OVER ZE WEEKEND: Inasemekana msanii ukishaingia kwenye ndoa na muziki wako unashuka, kwa upande wako hii imekaaje?
BELLE 9: Si kweli kwa sababu ukimuangalia Jay-Z (mwanamuziki wa Marekani) tangu amemuoa Beyonce ni miaka mingi na ndiyo kwanza anazidi kuwa juu kwenye muziki wake na utajiri unaongezeka. Tatizo watu wanaongea bila utafiti ila kwa upande wangu naamini ndoa ni baraka, muziki una nafasi yake.
OVER ZE WEEKEND: Inasemekana unaringa sana na hupendi kujichanganya, je, kuna ukweli wowote?
BELLE 9: Siwezi kulazimisha mtu anijue muonekano wangu. Mimi ni binadamu, ninakosea labda hiyo inafanya watu wanielewe tofauti, hata mimi najijua siringi.
MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA NA KHADIJA BAKARI


