The House of Favourite Newspapers

BEN POL: KAOKOTA DODO , KASAHAU ALIKOTOKA !

Benard Paul ‘Ben Pol’

WASWAHILI wana msemo wao pale mtu anapobahatika na kitu fulani, utasikia; ‘ameokota dodo chini ya muarobaini’ ikiwa na maana kuwa amefanikiwa kupata kitu ambacho hakikutarajiwa na wengi.

 

Kwa miaka ya hivi karibuni kumeibuka wasanii wengi kuokota madodo chini ya muarobaini. Tumeona kwa msanii wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ’Harmonize’ akimpata mwanamke wa kizungu raia wa Italia, Sara.

 

Tumeona pia kwa msanii Hussein Machozi ambaye ‘kazamia’ nje ya nchi akiwa anaishi na mwanamke wa kizungu raia wa Italia, pia tumeona kwa msanii mwingine Rama Dee ambaye anaishi nchini Australia na mwanamke wa Kizungu aliyezaa naye mtoto mmoja. Ukiachilia wasanii wengi kuokota madodo kwa wazungu, msanii wa Bongo Fleva, Benard Paul ‘Ben Pol’ naye ameingia katika listi ya waliookota madodo ambapo amenasa kwa mtoto wa kitajiri kutokea nchini Kenya, Anerlisa Muigai.

 

ANERLISA NI NANI?

Ni binti wa miaka 31, aliyetokea familia ya kitajiri akiwa ni mtoto wa kwanza ambapo mama yake, Tabitha Karanja anamiliki kiwanda kikubwa cha kutengeneza bia kiitwacho Keroche Breweries kinachosambaza vinywaji vyake eneo kubwa nchini Kenya.

 

Baada ya kufanya kazi na mama yake kupitia kiwanda cha bia, 2013 Anerlisa aliamua kufanya biashara ya kujitegemea na ndipo alipoanzisha kampuni yake mwenyewe aliyoiita NERO. Kampuni hiyo ambayo imempatia utajiri mkubwa alionao sasa, inadili na kutengeneza maji ya kunywa aina ya Executive ambayo huhifadhiwa kwenye chupa spesho na hata upatikanaji wake ni kwenye maeneo yenye hadhi.

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes lililotoka mwaka jana, linamtaja Anerlisa kuwa miongoni mwa vijana 30 wanaokuja kwa kasi katika ujasiriamali Afrika. Pia Jarida la Business Elites Africa linamtaja Anerlisa kuwa miongoni mwa matajiri Afrika wenye umri chini ya miaka 40. Anerlisa anamiliki jumba la kifahari pande za Nairobi, magari kama yotee likiwemo Range Rover Evogue na Jeep, anamiliki viatu vya kifahari aina ya Manolo Blahnik zaidi ya pea 100 vyenye thamani ya shilingi milioni mbili kwa pea moja.

 

BEN POL ALIPATAJE DODO?

Vyanzo mbalimbali vinadai kuwa, Anerlisa alikaa na timu yake na kupendekeza kufanya shoo ya kuwapongeza wote wanaosapoti biashara yake ya maji. Kupitia kwenye ukurasa wake wa Instagram, akaweka baadhi ya kumbi za kisasa walizokubaliana nazo na kuandika:

 

“Mmoja kati ya wasanii kutoka Afrika Mashariki, Ben Pol amekubali kuwa nasi.” Inadaiwa kuwa, baada ya Ben Pol kufika na kufanya shoo hiyo, Anerlisa alimtumia pia kwenda kupeleka misaada kwa watoto yatima ambapo kwenye ukurasa wake wa Instagram Ben Pol aliandika; “Nimeshukuru sana kupata nafasi ya kutembelea Kituo cha Watoto cha Makadara (MAKADARA CHILDREN CENTRE) hapa Nairobi. Ni kituo ambacho kinawachukua watoto kutokea mitaani na kisha wanasaidiwa malazi, chakula, elimu na mahitaji mengine. Niliambatana na @anerlisa.”

Baada ya hapo Ben Pol hatukumuona Bongo, alikuwa tayari ameingia kwenye uhusiano, kuelekea Sikukuu ya Krismas, mwaka jana alionekana na Anerlisa ndani ya ndege wakielekea Paris, Ufaransa na Mwaka Mpya walitua Dubai na kote huko walikuwa kwenye hoteli za kifahari. Limekuwa jambo la kawaida kila mmoja kuonesha alama za mapenzi kwenye mitandao.

 

AMESAHAU ALIPOTOKA?

Yawezekana, kama ilivyokuwa kwa wasanii wengine ambao wameokota madodo na wamekuwa wakionekana Bongo kwa ‘machale’ na muziki kwao wanafanya kawaida tu akiwemo Hussein Machozi, Rama Dee, Mr Paul na wengineo. Ben Pol mara ya mwisho mwaka jana alitoa Ngoma ya Siyo Mbaya akiwashirikisha The Mafik na kwa sasa ameelekeza zaidi kula bata na Anerlisa na haijajulikana atarudi lini tena Bongo.

Makala: ANDREW CARLOS

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

 

Comments are closed.