KATIKA kuendeleza jitihada zake za kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii, Benki ya NBC imedhamini hafla maalumu ya kuchangisha fedha iliyoandaliwa na Klabu ya Rotari ya Bahari jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Hafla hiyo iliandaliwa na klabu hiyo ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia wenye mahitaji maalumu katika jamii ya watanzania ikiwemo mradi wa kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama, vyoo na ujenzi wa kituo cha kufundishia kwa njia ya mtandao katika Shule ya Sekondari ya Mtakuja iliyopo eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na wa Kati wa NBC, Evance Luhimbo alisema NBC kwa miaka kadhaa imekuwa ikishughulisha katika kusaidia shughuli za jamii katika maeneo mbalimbali kama vile elimu, afya na masuala ya ujasiriamali,
“Sisi ni jukumu letu kama benki kurudisha katika jamii sehemu ya faida tuipotayo katika biashara yetu, NBC ni benki kongwe yenye uzoefu katika kutoa huduma bora za kibenki kwa zaidi ya miaka 52, hivyo tutaendelea kusapoti miradi kama hii yenye kuleta tija katika jamii”, alisema.
Pamoja na hayo alisema mara baada ya kupokea maombi ya kuchangia hafla hiyo kutoka Klabu ya Rotari, benki yao haikusita kuitikia wito kwani ni imani jamii ikiwezeshwa kiuchumi na kielimu na jamii ikiwa na afya bora inaweza kuchangia vizuri katika kuleta maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Aidha Bwana Lhimbo aliitaja baadhi ya shughuli za kijamii ambayo NBC imefaya ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa vya ujenzi wa madarasa katika shule za mkoani Lindi, Zanzibar, msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa Morogoro pamoja na kutoa elimu ya masuala ya kifedha na ujasiriamali katika shule mbalimbali nchini.
Baadhi ya miradi ambayo imeshafanikishwa na Klabu ya Rotari ya Bahari ni pamoja na matibabu ya moyo kwa watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ukarabati wa maktaba katika shule ya msingi buyuni, upanuzi wa kituo cha mafunzo ya ufundi stadi katika kituo cha masista cha Carmel, Kurasini, ukarabati wa maktaba katika Shule ya Sekondari ya Mtakuja pamoja na kutoa misaada ya aina tofauti katika vituo vingine vya walemavu na wasiojiweza.
Comments are closed.