The House of Favourite Newspapers

Benki Ya NBC Yakabidhi Kombe La Ubingwa Wa Ligi Kuu Kwa Yanga

0
Wachezaji wa Yanga wakishangilia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC mwaka 2022/2023 mara baada ya kukabidhiwa kombe lao kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mbeya Juni 9, 2023: Mdhamini mkuu wa ligi ya NBC, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) leo imekabidhi kombe la ubingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa timu ya Yanga ambayo ndiyo bingwa kwa msimu wa 2022/2023.

Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa ilifanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, huku ikishuhudiwa na mamia ya wapenda soka wakazi wa jiji hilo na maeneo ya jirani.

Akikabidhi kombe hilo kwa Yanga mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera aliishukuru benki ya NBC kuwa mdhamini mkuu wa ligi kuu ya Tanzania bara na kusema kuwa udhamini wa NBC umekuwa na matokeo chanya kwa soka la Tanzania.

Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Waziri Barnabas (wa tatu kushoto) akishangilia kombe la Ligi kuu ya NBC mara baada mabingwa wa msimu huu 2022/2023 Yanga kukabidhiwa, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa NBC, David Raymond. Wengine ni wachezaji wa Yanga na wafanyakazi wa NBC.

“Udhamini wa NBC umewezesha kuongeza ushindani kwenye ligi na kuboresha soka letu. Leo hii tunajivunia kuwa na ligi bora barani Afrika tukishikilia nafasi ya tano. Naipongeza sana benki ya NBC kwa kufanya mambo makubwa katika ligi na soka la nchi yetu kwa ujumla,” alisema Homera.

Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza timu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa na kusema kuwa haikuwa rahisi kwa timu hiyo kuibuka kinara wa ligi kutokana na ushindani mkali kutoka kwa timu pinzani.

Kwa upande wake mkurugenzi wa fedha wa NBC Barnabas Waziri alisema NBC itaendelea kuwa mdhamini mkuu wa ligi na kuongeza kuwa benki hiyo pia itaendelea kutoa mchango katika sekta ya michezo kwa upana wake.

Wachezaji wa Yanga na baadhi ya viongozi wao wakishangilia kombe hilo baada ya kukabidhiwa.

“Pamoja na soka, tumekuwa tukisadia michezo mingine kama riadha kupitia NBC Dodoma marathon. Nia yetu ya kusaidia sekta ya michezo hapa nchini ni thabiti na tutaendelea kusaidia,” alieleza

Mkurugenzi huyo alisema udhamini wa NBC kwenye ligi kuu umekuja na maboresho kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa bima kwa wachezaji wa ligi kuu pamoja na familia zao pamoja na mikopo ya mabasi kwa vilabu vinavyoshiriki ligi.

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said akiwa kwenye picha ya pozi na mchezaji wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki na kombe la ubingwa wa NBC.

“Juzi tumezindua kombe jipya lenye hadhi na ambalo leo litakabidhiwa kwa bingwa waligi.

Ili kuongeza hamasa kwa wachezaji na makocha, tumekua tukitoa tuzo mbalimbali kwa makocha na wachezaji bora wa mwezi,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliipongeza Timu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo na pia alizipongeza timu zote zilizoshiriki ligi ambayo ushindani wake umekuwa ni mkubwa.

Leave A Reply