



SPIKA wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ameiomba Benki ya NMB kutoa elimu kwa wananchi ili wajue jinsi ya kutunza fedha za mikopo yao.
Ndugai ameyasema hayo wakati NMB ilipofanya ziara ya kukabidhi jumla ya viti na meza 63 kwa Shule ya Mnyakongo pamoja na mabati 250 kwa Shule ya Chiwe zilizopo Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Spika amesema kuwa NMB wana kila sababu ya kuendelea kutoa elimu ya utunzaji fedha kwa wananchi kama wanavyofanya kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili wawe na ujuzi zaidi.
Aidha amesema kuwa watu wengi wanakopa fedha lakini hawajui wazifanyie nini baada ya kuzichukua.
‘’Yaani unashangaa muda mchache ukikutana na watu hao hakuna cha maana walichofanyia badala yake wanarudi katika maisha yya chini badala ya kusonga mbele kimaisha, ’’ alisema Ndugai na kuongeza kwamba kutokana na hilo kuna sababu ya elimu hiyo kutolewa kwa wananchi ili wakope fedha huku wakijua wanakwenda kuzifanyia nini.
Pia amefafanua kuwa ameshakutana na matukio mengi ambapo ndugu jamaa na marafiki waliokopa bila ya kupata mafanikio yoyote.
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi, alisema kuwa wataendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli hivyo wametenga maeneo manne kwa ajili ya kusaidia jamii.
Mlozi ameyataja amaeneo hayo kuwa ni elimu, afya, kilimo na utunzaji fedha kwa vijana mpaka watu wa rika la juu kwa lengo la kuwainua kiuchumi kwa kunufaika kwa kupitia NMB.
Hata hivyo amesema kuwa mpaka sasa tayari Shilingi milioni 400 zimeshatolewa kwa ajili ya misaada katika shule na hospitali ukiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa na akaongeza kwamba NMB iko pamoja na serikali kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.
Wakati huohuo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mnyakonga, Mpokeeni Sanga, alisema kuwa walikuwa na upungufu wa madawati 70 na hivyo wanaishukuru NMB kuwapa viti 63 na meza 63 na ambavyo wanaamini vitasaidia
kupunguza uhaba waliokuwa nao.
Sanga amewahakikishia NMB kuwa vitu hivyo watavitunza ili wanafunzi wengine waje kuvitumia hapo mbeleni na amewaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia jamii kwani wamekuwa mfano wa kuigwa nchini.
Vilevile, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Chiwe, Aaron Mango, alisema kuwa mabati waliyopewa yatawasaidia kuezeka mabweni ya wasichana ambayo yanajengwa shuleni hapo


Comments are closed.