The House of Favourite Newspapers

BENKI YA NMB YASAIDIA ELIMU WILAYA ZA MOMBA NA ILEJE

Wanafunzi wa Shule ya sekondari Ileje wakibeba madawati  baada ya kuyapokea. 
Wanafunzi wa Shule ya sekondari Ileje wakionyesha furaha yao baada ya kupokea msaada.

 

 

WAKUU  wa Wilaya za Ileje na Momba Mkoani Songwe wamepongeza Benki ya NMB kwa msaada  wa kujitokeza kusaidia miundombinu ya elimu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihaza za Serikali kuwahudumia wananchi.

 

Wakuu hao ni Jumaa Irando wa Momba na Joseph Mkude wa Ileje walitoa rai hiyo jana kwa nyakati tofauti wakati wakipokea msaada wa vifaa vya shule kutoka Benki ya NMB ambayo ilitoa bati 254 kwa Halmahauri ya Tunduma Wilaya ya Momba na madawati 50 kwa shule za Msingi Nyerere na sturi 184 za maabara shuleni kwa shule za Sekondari za Ileje na Kafule zote za Wilayani Ileje huku vyote vikigharimu Sh 25 milioni.

 

 

Irando alisema Mji wa Tunduma ni miongoni mwa miji inayokuwa kwa kasi kutokana na ongezeko kubwa la watu hivyo wamekuwa na changamoto lukuki kwenye suala la miondombinu ya shule kwa Serikali pekee kulitimiza bali kwa kuungwa mkono na wadau mbalimbali kama walivyofanya NMB.

 

 

“Kwa kweli tunachangamoto kubwa sana hapa Tunduma, kuna ongezeko kubwa la watoto wanaoanza darasa la kwanza kila mwaka tofauti na makisio au matarajio tunayokuwa tumejiwekea.

 

 

Jambo hili linafanya kuwa na msongamano mkubwa mashuleni kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati pia, hivyo NMB mmetuangalia kwa jicho la pekee kabisa kuona tunahitaji msaada wenu na wadau wengine waige hili jambo kwa ajili ya kuisadia jamii yetu,”

 

Alisema mahitaji ya huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu yanahitaji kuungwa mkono na taasisi na mashirika mbalimbali ya kijamii kama inavyofanywa na Benki ya NMB.

 

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude alisema imetekeleza wajibu wao na thamani yao kwa Watanzania hususani wananchi wa Ileje ambao kimsingi wapo pembezoni kabisa mwa nchi.

 

Alisema ‘Nawashukuru sana NMB kutukubalia ombi letu na leo hii kutuletea sturi na madawati kwetu sisi tunauthamini mno mchango wenu na katika hili tunazidi kuwaunga mkono kwa jitihada zenu, na tuwaahidi tutahakikisha vifaa hivi vinatunzwa ili vidumu kwa muda mrefu’.

 

Awali Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Straton Chilongola alisema benki ya NMB inatambua umuhimu wa elimu na afya kwa Watanzania hivyo katika kipindi cha mwaka huu wa 2019, NMB imetenga Sh1 bilioni kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwamo afya, elimu na majanga ya dharula kwa nchi nzima.

 

Hivyo benki hiyo itaendelea kusaidia katika sekta hiyo ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi za Serikali za kuwahudumia wananchi wake. Alisema NMB ni wadau muhimu kwa Serikali na Watanzania hivyo wanao wajibu wa kuunga mkono juhudi za maendeleo kwa sababu jamii wanayoisaidia ndiyo inayowawezesha kupata faida katika biashara yao.

 

“Tunambatua changamoto ya elimu na afya, sisi NMB tunazipa kipaumbele sana kwa sababu hizi sekta mbili ni muhimu mno katika ustawi wa jamii yetu,” alisema Chilongola.

Comments are closed.