The House of Favourite Newspapers

UBA YASHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUTOA MISAADA HOSPITALI YA TEMEKE

Ofisa Mwendashaji Mkuu wa Benki ya UBA Tanzania Flavia Kiyanga (kulia) akikabidhi mashuka kwa Mbunge wa jimbo la Temeke Abdallah Mtolea (kushoto) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Benki ya UBA Tanzania ilitoa mashuka 100 kwa Hospitali ya Rufaa ya Temeke ikiwa ni njia ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Wa pili kushoto ni Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angela Kairuki na wa pili kulia ni Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke Dkt Amaan Malima.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki na Mbunge wa jimbo la Temeke Abdallah Mtolea (kushoto) kwa pamoja wakionyesha mashuka yaliyotolewa na Benki ya UBA Tanzania kwa Hospitali ya Rufaa ya Temeke.
Shughuli ya upokeaji msaada ikiendelea baina ya Ofisa Mwendashaji Mkuu wa Benki ya UBA Tanzania Flavia Kiyanga (kulia) akikabidhi mashuka kwa Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angela Kairuki.

 

 

 

Benki ya United Bank for Africa Tanzania (UBA) imesherehekea siku ya wanawake duniani kwa kutoa msaada wa mashuka 100 kwa Hospitali ya Rufaa ya Temeke ya jijini Dar es Salaam ikiwa ni moja ya njia ya kutekeleza programu yake ya kusaidia jamii inayoizunguka.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu analiyeshughulikia uwekezaji, Angela Kariuki, Mbunge wa Jimbo la Temeke Abdallah Mtolea na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo walipokea msaada huo kwa niaba ya uongozi wa hospitali ya Temeke.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Kariuki alisema kuwa siku ya wanawake duniani ni siku maalum kwa wanawake kusherehekea fursa za kijamii, kiuchumi, mila pamoja na mafanikio kwenye siasa. Kwa maana hiyo, nimefarajika sana baada ya kutambua kuwa wanawake wanafanya kazi na benki ya UBA Tanzania wamechangisha fedha kutoka mfukoni mwao na kununua mashuka haya 100 ambayo tumeyapokea hapa.

 

 

Wangeweza kutumia fedha hizo kwenye sherehe zingine lakini wakaona umuhimu wa kuja kusherehekea hii siku muhimu kwa watu ambayo kwenye jamii hawajiwezi na wenye magonjwa mbali mbali. Hii ni kitu muhimu na wameweza kuwa mfano bora ambao ningeomba na wengine waweze kufanya kama hivyo, alisema Kariuki.

Waziri Kariuki alisema kuwa wanawake ni watu muhimu kwenye familia na pia kwenye jamii. Kwa maana hiyo, ni lazima kila siku mfanye kazi kwa bidii ili kuweza kupata mafanikio. Vile vile, ni muhimu kutambua ya kwamba wanawake mnazo fursa za kupata mafanikio kwa wanaume lakini ni vizuri kutumia muda wenu vizuri na kufanya kazi kwa malengo ili kufikia mafanikio. Naomba UBA Tanzania pamoja na wadau wengine wa maendeleo kuendelea na moyo huu wa kusaidia jamii na sisi kama serikali tutaendelea kuwaunga mkono.

 

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke Dkt. Amaan Malima alitoa shukrani kwa benki ya UBA Tanzania kwa msaada huo wa mashuka huku akisema kuwa hospitali hiyo imekuwa na uhaba mkubwa wa mashuka na hivyo msaada huo umekuja kwa muda muafaka. Msaada wenu tumeupokea kwa moyo wa dhati. Hapa kwenye hospitali yetu kila kitanda huwa kinatumia hadi mashuka saba kwa siku kulingana na mgonjwa anayekitumia. Kwa maana hiyo ni lazima upungufu utakuwepo. Tunawashukuru sana na tunawaomba kuwakaribisha kwa siku za baadaye kwa msaada  huu, Dkt Malima alisema.

Kwa upande wake , Ofisa Mwendashaji Mkuu wa benki ya UBA Tanzania Flavia Kiyanga alisema kuwa kusaidia jamii yenye mahitaji maalumu imekuwa ni moja ya programu ya benki hiyo ya muda mrefu. Jamii inayotuzunguka ni muhimu sana kwetu. Kutoa kwa ajili yao ni programu maalum sisi kama benki na leo tumeona ni vizuri kuja kuwatembelea wagonjwa hapa Hospitali ya Rufaa ya Temeke pamoja na kutoa msaada huu wa mashuka kwani tunaamini hawa watu wenye mahitaji maalum pia wanatajika kuonyesha upendo, Kiyanga alisema.

Kiyanga alisema msaada wa mashuka hayo umetokana na wafanyakazi wanawake wa UBA Tanzania ambao wameweza kutoa baadhi ya kipato chao ili kuja kusherehekea siku ya wanawake duniani kwa wagonjwa hapa Temeke. Tunayo furaha kubwa kuweza kutimiza moja ya lengo letu lakini zaidi tunawashukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke kuweza kutupokea vizuri na kukubali msaada wetu alisema Kiyanga huku akiongeza kuwa wao kama benki wanatakia uponaji wa haraka kwa wagonjwa waliolazwa hapo ili waendelea na shughuli zao za kila siku.

Comments are closed.