The House of Favourite Newspapers

Berlusconi; Waziri Mkuu aliyebondwa usoni na kuvunjwa pua

0

Hebu vuta picha, mheshimiwa waziri mkuu amemaliza kuwahutubia wananchi na sasa anapeana nao mikono na kusaini vitabu vya kumbukumbu, ghafla anatokea njemba mmoja na kumvurumishia kitu kizito akiwa jirani naye kabisa, mheshimiwa anadondoka chini huku damu kibao zikimvuja! Unaweza kuona kama ni hadithi ya kutunga, si ndiyo?

Basi kwa taarifa yako, tukio kama hilo limewahi kumpata aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi. Ilikuwaje? Ilikuwa ni Desemba 13, 2009 wakati waziri mkuu huyo wa zamani wa Italia akisalimiana na wananchi,  ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Milan Piazza del Duomo.

Akiwa anafurahi na wananchi wake, ghafla aliibuka mwanaume ambaye baadaye alitambuliwa kwa jina la Massimo Tartaglia, mkononi akiwa ameshika sanamu maarufu nchini humo, Milan Cathedral Statue.

Kufumba na kufumbua, mwanaume huyo akamvurumishia waziri mkuu usoni, ikatua sawia katikati ya pua na mdomo na kusababisha aanguke chini kama mzigo. Damu chapachapa zikaanza kumtoka ambapo ilibidi walinzi wake wamnyanyue kwa kasi ya kimbunga na kumkimbiza kwenye gari lake huku akianza kupewa huduma ya kwanza.

Hata hivyo, mwenyewe alikuwa hataki kutulia sehemu aliyolazwa, akawa anainuka na kutaka kushuka kwenye gari, hali iliyowapa waandishi wa habari nafasi nzuri ya kumpiga picha usoni, akiwa ametapakaa damu chapachapa.

Baadaye gari alilokuwemo liliondolewa eneo hilo kwa kasi na waziri mkuu huyo akawahishwa hospitalini ambapo majibu ya picha za X-Ray alizopigwa, yalionesha kwamba alivunjika mfupa laini wa pua pamoja na kuvunjika meno mawili, ikabidi alazwe hospitalini kwa siku kadhaa.

Akiwa hospitalini, walinzi wake walifanikiwa kumnasa kijana mwingine aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 26 akijaribu kupenya kuingia kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Berlusconi. Baada ya kupekuliwa, kijana huyo alikutwa na magongo mawili na visu viwili katika gari lake na kuwekwa kizuizini ingawa baadaye aliachiwa.

Baadaye taarifa zilisambaa kwamba mwanaume aliyemjeruhi Berlusconi alikuwa na matatizo ya akili ingawa hakuwahi kuripotiwa kusababisha vurugu za aina yoyote zaidi ya tukio hilo. Baadaye mwanaume huyo aliomba radhi kupitia vyombo vya habari na kueleza kwamba alikuwa hajitambui wakati anafanya tukio hilo.

Berlusconi alitoka hospitalini Desemba 17, siku nne baada ya tukio na kuzungumza na waandishi wa habari ambapo alijitapa kwamba yupo fiti.

Katika utawala wake, Berlusconi ambaye pia ni mmiliki wa kampuni kubwa ya habari (media house) nchini Italia, alikuwa akikabiliwa na skendo za kula rushwa, matumizi mabaya ya ofisi, ngono na madai mazito kwamba alikuwa akishirikiana na kundi hatari la Mafia.

Leave A Reply