The House of Favourite Newspapers

BETHIDEI YA KIKONGWE MIAKA 103 YATIKISA DAR!

NINI Wema Sepetu! Mbwembwe nyiiingiii kwenye bethdei yake ya kutimiza miaka 30, je, angekuwa Bibi Catherine Abdallah Batemayo aliyesherehekea kutimiza miaka 103 ingekuwaje?  Jumamosi wiki iliyopita jijini Dar na hasa Kitongoji cha Kitunda, tukio lililotikisa lilikuwa ni lile la bibi huyo kuimbiwa wimbo wa Happy Birthday to you, huku akiwa na karne moja ya uhai duniani.

Bibi Catherine Abdallah Batemayo

“Bado anajitambua, anaweza kusoma biblia bila kuvaa hata miwani,” alisema mjukuu wa bibi huyo aitwaye Dustan Shekidele. Bi. Kizee huyo alizaliwa Kijiji cha Mlalo, Lushoto mkoani Tanga Septemba 29, 1915, ambapo katika familia yake walizaliwa watoto tisa na kwamba wenzake wote walishatangulia mbele za haki.

UWAZI LATINGA KWENYE SHEREHE

Kufuatia kuwepo kwa taarifa kwamba bibi huyo ameandaa sikukuu ya kuzaliwa kwake akishirikia na baadhi ya wanaye, Uwazi lilitinga kwenye sherehe hiyo mapema na kumshuhudia bibi huyo akiwa kwenye maandalizi ikiwa ni pamoja na kufanyiwa ‘make up’.

UWAZI: Shikamoo bibi.

BIBI: Marahabaa.

UWAZI: Bibi eti leo kuna nini hapa kwako.

BIBI: Wapi?

UWAZI: Hapa nyumbani kwako? Bibi huyo alionekana kushindwa kujibu swali hilo hadi pale mjukuu wake alipomfafanulia zaidi.

BIBI: Ni bezidei yangu, (Isomeke kama birthday).

UWAZI: Unatimiza miaka mingapi.

BIBI: Eeee …mingi sana. Anajibu bibi huyo na baadaye kusaidiwa na mjukuu wake kuweka idadi ya miaka 103.

SHEREHE YAANZA

Majira ya saa 11 jioni, siku hiyo ya sherehe ghafla bibi huyo aliyekuwa akisindikizwa na wanaye kadhaa alijitokeza mbele ya waalikwa huku akiwa amependeza ile mbaya kwa nguo na mapambo aliyopambwa.

Nderemo na vigelegele vilitawala huku muziki nao ukisindikiza kwa mbali ujio wake. Aidha alipomaliza kuketi mahali alipoandaliwa, shughuli ilifunguliwa na mjukuu wake Shekidele ambaye aliwakaribisha waalikwa na kutoa historia fupi ya bibi huyo.

Wimbo wa; Kata Keki Tule, Kata Keki Tuuleee haukwenda mbali ambapo bibi huyo alijikokota kwa nguvu zake hafifu na kuwalisha baadhi ya watoto, wajukuu, watukuu na nyanya zake waliokuwa wamefika kwenye sherehe hiyo.

Aidha baada ya watu kula, kunywa na kucheza muziki vya kutosha Uwazi liliamua kufanya mahojiano maalumu na bibi huyo kwa lengo la kujua mengi kuhusu maisha yake.  Hata hivyo pamoja na uwezo wa kujieleza aliokuwa nao bibi huyo, kuna wakati kumbukumbu zake zilikuwa zinapotea jambo lililomfanya mjukuu wake amsaidie kufafanua.

UWAZI: Bibi unamfahamu rais Magufuli (John)?

Bibi huyo aliguna huku akimtazama mwandishi wetu ambapo mjukuu wake alifafanua kuwa:

“Alipofanya sherehe yake ya kuzaliwa miaka takriban mitatu iliyopita alikuwa vizuri katika kumbukumbu, nakumbuka wakati huo ndiyo kulikuwa na vuguvugu la uchaguzi, alitabiri rais Magufuli angeshinda.

“Wakati huo alisema kwamba anatamani akishinda siku moja ahudhurie kwenye bethidei yake…” alisema mjukuu na kukatizwa na sauti ya bibi huyo:

“Leo kaja?” Akimaanisha rais Magufuli.

MJUKUU: Hahaha, aje kwani ulimwalika?

BIBI: Eeeeh!

MJUKUU: We bibi lini ulimwalika? Mwenzio ana majukumu makubwa ya kitaifa.

BIBI: Mmmh! Aliguna bibi huyo kwa masikitiko na kusema kwa sauti ya chini: “Mwambieni naye aje.”

MWANDISHI: Ungependa umwambie nini?

BIBI: Aongoze nchi.

Hata hivyo, baada ya kuona maelezo ya bibi huyo anayetajwa kumpenda Rais Magufuli yanakwenda mbele na kurudi nyuma, Uwazi lilitambua kuwa umri wa kikongwe huyo umesonga mbele na kwamba alihitaji muda wa kuburudika zaidi kuliko kuulizwa maswali.

AFURAHIA PICHA KWENYE SIMU

Mjukuu wake Shekidele alipotaka kumthibitishia Mwandishi Wetu kuwa bibi huyo ana uwezo mkubwa wa kuona, alimuonesha picha alizompiga kwenye sherehe hiyo ambapo alionekana kuzifurahia.

“Eee…mimi huyu,” alisema bibi huyo baada ya kujitazama kupitia picha na kushangazwa jinsi alivyokuwa amepambwa. Furaha yake ilizidi hasa pale alipooneshwa namna ya kuzisogeza picha hizo kwa kutumia kidole chake (touch) ambapo alionekana kutabasamu muda wote.

Katika hatua nyingine bibi huyo alishangaza wengi pale alipokuwa akisoma meseji za kumtakia heri ya sherehe ya kuzaliwa kwake zilizotumwa kutoka kwa wajukuu na vituuu vyake ambao hawakufanikiwa kuhudhuria sherehe hiyo. Mbali na tukio hilo la kushangaza la kusoma sms bila miwani, pia kila aliyemsogelea alimuombea na kumtakia maisha marefu kama yeye.

SIRI YA KUISHI MIAKA MINGI NI NINI?

Wataalam wa masuala ya afya kutoka vyuo mbalimbali duniani wamekuwa wakibainisha mara kadhaa katika tafiti zao kuwa siri kubwa za kuishi miaka mingi ni kuzingatia kanuni bora za afya.

Miongoni mwa mambo ambayo yametajwa kuchangia kuwafanya watu waishi muda mrefu kwa mujibu wa Chuo Cha Maisha Na Mazingira cha Austraria ni pamoja na kufanya mazoezi, kuepuka msongo wa mawazo, kula vyakula bila kushiba kupitiliza na kutafuta furaha kila wakati.

Nchi inayotajwa kuwa na wakazi wanaoishi miaka mingi zaidi ya 100 ni Japani ambapo Kisiwa na Okinawa kinatajwa kuwa na watu wanaozingatia kanuni bora za afya.

Nchini Tanzania wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 37, mwaka 1978 hadi kufikia miaka 65, mwaka 2018, hii ni kwa mujibu ya Ripoti ya Makadirio ya Idadi ya Watu kuanzia mwaka 2013- 2030 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ‘NBS’.

Kwa msingi huo uwepo wa wazee wanaozidi miaka ya makadirio ni jambo jema kwa vile linaonesha kuwa taifa linaendelea kupiga hatua katika kuimarisha afya ya watu wake.

STORI: RICHARD

Comments are closed.