Bi Hindu: Napoteza Fahamu, Mwambieni Lulu Anikumbuke!

CHUMA Seleman ‘Bi Hindu’ ni mwigizaji mkongwe Bongo. Ni mmoja kati ya waanzilishi wa Kundi la Kaole Sanaa na ndiye aliyetoa jina hilo wakati kundi linaanzishwa. Umezoea kumuona akishabikia Klabu ya Simba, ila kihistoria aliwahi kucheza katika klabu hiyo wakati inaitwa Morning Star na Sunderland.

 

Kwenye uigizaji, Igizo la Gubu la Wifi ndilo lililomfungulia njia. Baadaye alionekana kwenye filamu, ukungwi, UMC kisha utangazaji. Mara ya mwisho alionekana kwenye Tamthiliya ya Maneno ya Kuambiwa.

Bi Hindu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 81, miezi kadhaa iliyopita zilisambaa tetesi kwamba anaumwa na yupo hoi kitandani.

 

Katika mahojiano maalum na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lililomtembelea nyumbani kwake, Magomeni-Mapipa jijini Dar, Bi Hindu anasema baadhi ya watu walionekana kumjali kwa kumtembelea na kumsaidia kile walichokuwa nacho, lakini ukweli ni kwamba bado hali yake ni mbaya kiafya kiasi cha kuhitaji msaada wa hali na mali kwa yeyote anayeguswa;

IJUMAA WIKIENDA: Pole sana Bi Hindu, tatizo ni nini hasa?

 

BI HINDU: Nashukuru. Nilianza kuumwa muda kidogo. Sasa hivi ni takriban miezi tisa nipo kitandani. Kabla ya hali yangu kuwa mbaya, huko nyuma nilichukulia kawaida kwa sababu nilikuwa na goita shingoni. Ndugu zangu wakasema inaweza ikawa ndiyo inasababisha maumivu mwilini.

 

IJUMAA WIKIENDA: Tatizo hasa linalokusumbua ni nini?

BI HINDU: Nilikwenda hospitalini, madaktari wakanipima na kuniambia mifupa yangu imelika (imesagika).

 

IJUMAA WIKIENDA: Ni sehemu gani ya mwili ambayo inakuuma sana?

BI HINDU: Sehemu ya bega la mkono wangu wa kulia ndiyo inaniuma sana mpaka ninapoteza fahamu. Nimeshakwenda Muhimbili nikafanyiwa oparesheni ya kwanza, lakini haikusaidia. Ikabidi nifanyiwe oparesheni ya pili ambayo baada ya kukaa siku tatu, hali ilizidi kuwa mbaya na sasa hivi ndiyo siamki, naumwa na kupoteza fahamu kila wakati. Mkono unaniuma, hapa nilipo najisikia hata kufa.

 

IJUMAA WIKIENDA: Madaktari wamekuhakikishia kuna uwezekano wa kupona kabisa?

BI HINDU: Ndiyo, nimeambiwa uwezekano wa kupona upo na sasa hivi kuna vidonge nimepewa, ambavyo natumia kwa siku 30, lakini tatizo ni pesa. Pesa zote nilizokuwa nazo benki, nimetumia kwa matibabu na sasa nimebaki mtupu.

 

IJUMAA WIKIENDA: Ombi lako kwa Watanzania ni lipi?

BI HINDU: Naomba wanitazame kama mama yao, ni msanii mkongwe, sina uwezo wa kipesa kama ilivyo kwa watu wengine, naomba kama kuna mtu yeyote ambaye ataguswa na hali yangu, basi anisaidie.

IJUMAA WIKIENDA: Mungu akikusaidia sasa hivi ukapona, utarudi kwenye fani yako ya uigizaji na utangazaji?

 

BI HINDU: Sana, nimemisi kwelikweli. Naomba Mungu anipe uzima nirudi hata sasa hivi.

IJUMAA WIKIENDA: Mara kadhaa nimekuwa nikikusikia ukimsifia mwigizaji Lulu (Elizabeth Michael) pale anapostahili pongezi na pale anapokosea, umekuwa ukimuonya kama mzazi. Vipi tangu umeumwa amewahi kuja kukujulia hali?

 

BI HINDU: Ni kweli nampenda sana Lulu, lakini tangu nimeumwa, hajawahi kuja kunijulia hali, nadhani Mungu bado hajamjaalia kufika hapa. Sijajua kama alipata taarifa kutoka kwa Majizo (mchumba’ke Lulu), lakini namuombea Mungu ampe imani aweze kuja kuniona.

 

IJUMAA WIKIENDA: Una lipi la kumwambia Lulu?

BI HINDU: Namwambia hii ni dunia, maisha ayatazame, nani anampenda na wapi alikotoka, mimi na yeye (Lulu) tuliongea mangapi Kaole? Inshaallah mwambieni anikumbuke, awe karibu na mimi.

Mbali na Bi Hindu, pia IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na mwanaye, Mwanaidi Adamu ambaye alikiri mama yake kuumwa na kuongeza kwamba anaomba kama kuna mfadhili yeyote, ajitokeze.

kumsaidia ili apone.

 

MWANAIDI: “Mimi ni mtoto wa saba kwa Bi Hindu. Ni kweli mama yetu anaumwa sana, ametimiza miezi tisa sasa yupo kitandani. Awali alikuwa anasumbuliwa na goita na mkono, sisi tukajua labda goita ndiyo imesababisha mkono kuuma, lakini tulipokwenda Hospitali ya Muhimbili, madaktari wakatuambia kwamba tatizo la mkono ni lingine wala halihusiani na goita.

 

Tunapitia changamoto kubwa sana kwa sababu mama ni wa kuhudumiwa kila kitu. Tatizo linalomsumbua mama ni mkono kuuma kiasi cha kumkosesha usingizi.

 

Changamoto tunayokumbana nayo ni pesa kwa ajili ya matibabu yake. Maombi yetu kwa Watanzania wenzetu, tunaomba watusaidie chochote ili tumpeleke mama yetu hospitalini.

Kama umeguswa na tatizo la Bi Hindu, unaweza kumsaidia kwa ajili ya matibabu kupitia namba 0715 585 864 au akaunti namba 019163007678 yenye jina CHUMA S MZEE iliyopo Benki ya NBC.

Pia unaweza kufika Ofisi za Global Publishers zilizopo Sinza-Mori jijini Dar nasi tutakuunganisha naye.

MAKALA: Memorise Richard na Khadija Bakari

Toa comment