Biashara Yawaita Yanga Wafanye Biashara ya Kipa
UONGOZI wa Biashara United, umeweka wazi ikiwa mabosi wa Yanga wanahitaji saini ya kipa wao namba moja, Daniel Mgore ni suala la kukaa mezani ili kufanya mazungumzo.
Imekuwa ikielezwa kuwa, Yanga inahitaji kuboresha kikosi chao hasa upande wa mlinda mlango baada ya kipa wao namba moja, Metacha Mnata kusimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu, huku mkataba wake ukielekea ukingoni.
Pia katika kikosi hicho, Faroukh Shikalo na Ramadhan Kabwili ambao ndiyo makipa waliobaki, nao mikataba yao inaelekea kumalizika mwishoni mwa msimu huu.Akizungumza na Spoti Xtra, Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Mataso, alisema:
“Hakuna ambaye anaweza kumzuia mchezaji, huyu Mgore tumemkuza wenyewe kutoka timu ya vijana, kama kuna timu inamuhitaji iwe Yanga ama Azam FC, ni suala la kuzungumza.”
STORI: LUNYAMADZO MLYUKA, DAR