visa

VIDEO-BIBI AFANYIWA UTAPELI, AMLILIA RAIS MAGUFULI!

DAR ES SALAAM: Ni stori ya kusikitisha ambayo inamhusu bibi aitwaye Mwanahawa Mshamu Ngomari ambaye anadai kutapeliwa nyumba yake iliyopo Kawe Ukwamani jijini Dar huku kijana aliyefahamika kwa jina la Felix Urio akitajwa kuhusika na utapeli huo mzito.  Akizungumza na Gazeti la  Amani pamoja na +255 Global Radio, huku akilia kama mtoto mdogo, bibi huyo mwenye umri wa miaka 89 anadai kuwa Urio ambaye ni mwanaye wa kufikia amehusika kwenye utapeli huo kwa kuiba hati ya nyumba yake kisha kwenda kuitumia kukopea benki.

MSIKIE BIBI HUYO

“Nilibahatika kuzaa mtoto mmoja wa kiume ambaye alifariki mwaka 1989, huyo mtoto wangu alipata watoto watatu, mmoja alifariki pia, kwa sasa nimebaki na wajukuu wawili. “Wajukuu zangu walipokuwa wakubwa walienda kuwa na maisha yao, mimi nikabaki na wapangaji tu. Huyu kijana Urio akawa amenizoea sana, ikafika wakati kwa wema wangu nikamfanya kama mwanangu tu.

“Kutokana na jinsi nilivyokuwa namuamini, sikuwa na wasiwasi naye kabisa, sasa kuna siku aliniletea karatasi na kuniambia nisaini, mimi na ubovu wangu wa macho na kwa kuwa sijui kusoma, akaniambia niweke dole gumba. “Kumbe maelezo ni kwamba mimi nimekubali awe mwanangu wa hiyari na awe na mamlaka ya kudili na mali zangu zote ikiwa ni pamoja na kwenda kulipia bili za maji na kodi ya majengo.

“Tatizo lilikuwa pale nilipoumwa, kuna siku huyu kijana aliiba hati ya nyumba yangu, inavyoonekana walikwenda kuchukulia mkopo benki. Nikiwa sina hili wala lile, mwaka 2015 wakaja watu wa benki na kusema kuwa nimekopa na nimeshindwa kulipa hivyo wanataka kuipiga mnada nyumba.

“Nilishangaa maana sijawahi kukopa popote. Ikabidi twende kule benki na kukuta kwamba Urio alichukua hati ya nyumba na kumpa mtu aliyefahamika kwa jina la Catherine, wakakopa shilingi milioni 70, Urio akiwa ndiye mdhamini kwa kutumia hati ya nyumba yangu, naomba Rais Dk John Magufuli au yule waziri anayeitwa Lukuvi wanisaidie,” alieleza bibi huyo kwa masikitiko makubwa.

Naye jirani wa bibi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Imani Kasimu alidai kuwa, Urio ndiye anayehusika kwenye utapeli huo na kwamba serikali ya Rais Magufuli imsaidie bibi huyo asije akapokwa haki yake. “Inatuuma sana kuona huyu Urio anataka kumtapeli bibi wa watu. Sisi hatukubali, tutamsaidia mpaka bibi huyu apate haki yake,” alisema jirani huyo huku akiungwa mkono na mjirani wengine.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimahewa, Khalidi Ibrahimu alisema kuwa alipata taarifa kuwa kuna watu wa benki wamefika kwa bibi huyo na kutaka kuuza nyumba yake kwa madai kwamba alikopa na ndipo alipoamua kufika kujua undani wake.

“Mwaka 2015 walikuja watu wa benki wakidai kuwa wanataka kuuza nyumba, ikabidi niwazuie na kuwaambia hii nyumba ni ya huyu bibi. Nikazungumza na bibi kumuuliza kama alishawahi kuchukua mkopo benki, akaniambia hajawahi.

“Baada ya kufanya uchunguzi wangu nikabaini kuna utapeli unataka kufanyika. Ndipo nilipokwenda benki ambayo maafisa wake walifika kwa lengo la kupiga mnada nyumba ya bibi huyo, nikakuta kule aliyechukua mkopo ni mtu anayeitwa Catherine na huyo Urio ni mdhamini na walitumia hati ya bibi huyu kukopea.

“Tulipomuuliza Urio hiyo pesa alipeleka wapi akadai eti alimpa bibi shilingi milioni 40 na nyingine akasema hajui iliko na hata Catherine mwenyewe hataki kusema kuwa yupo wapi wakati yeye ndiye aliyemdhamini. “Kwa hiyo kwa sasa hili suala lipo mikononi mwa Jeshi la Polisi, Urio yuko ndani na benki imetoa siku 60 ili suala hili liishe,” alisema kiongozi huyo.

MWANDISHI: Neema Adrian

MASKINI BIBI ALIVYOTAPELIWA- FULL VIDEO
Toa comment