The House of Favourite Newspapers

Bilionea Aliyeoa Wake Wawili Dar Yamkuta!

0
Siku ya ndoa ya Bilionea Javan.

DAR ES SALAAM: Bilionea Javan Bidogo ambaye mapema mwaka huu aliibua gumzo kubwa baada ya kuoa wanawake wawili kwa siku mbili mfululizo wikiendi iliyopita yalimkuta ya kumkuta, baada ya jumba lake la kifahari, ambalo pia hutumika kama ofisi yake, kufungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Risasi Mchanganyiko linaandika.

 

 

…Akiwa kwenye gari na mkewe.

 

KISIKILIZE CHANZO

Chanzo chetu cha habari, ambacho kiliomba hifadhi ya jina na sehemu kilipo, kilisema kuwa kinazo taarifa kuhusu kufungwa kwa utepe mwekundu katika nyumba ya mfanyabiashara huyo mkubwa wa madini, ambaye anamiliki kampuni iitwayo Javan Group Of Companies.

 

“Niamini, huyo jamaa anadaiwa malimbikizo ya kodi ya kiwango kikubwa cha fedha na ameshindwa kulipa. Watu wa TRA walimwita na kumpa siku kadhaa alipe, nasikia hajalipa, kwa hiyo wameifunga hiyo nyumba yake kwa lengo la kuipiga mnada,” kilisema chanzo hicho na kuongeza kuwa mali zote zilizomo ndani ya nyumba hiyo pia zimezuiliwa.

 

Akiambatana na mkewe.

 

RISASI LATIMBA MJENGONI MBEZI

Baada ya kupewa ubuyu huo, Risasi Mchanganyiko likaamua kutumia muda kujiridhisha, hivyo kufanya safari hadi Mbezi Beach, maeneo ya Kwa Zena ambako ndipo nyumbani kwa Javan, ambaye pia anatajwa kama mtaalam wa mambo ya madini na miamba.

 

UTEPE MWEKUNDU WAZUNGUSHWA GETINI

Katika lango kuu la kuingia ndani ya jumba hilo la ghorofa moja, utepe mwekundu ulikutwa umefungwa ili kuhakikisha hakuna kitu kinaingia wala kutoka huku akionekana mlinzi ambaye alikataa utambulisho wake kuchukuliwa, alidokeza kuwa yupo hapo kwa maelekezo ya TRA.

 

Nyumba yake ikiwa imewekewa uzio.

 

 

SAFARI KUELEKEA OFISINI TRA

Baada ya kujiridhisha juu ya kufungwa kwa nyumba hiyo, Risasi Mchanganyiko lilichapa mwendo hadi ofisi za TRA mkoa wa Kinondoni ambazo zipo Mwenge kwa ajili ya kupata maelezo ya kina na likiwa ofisini hapo, lilikutana na ofisa mmoja ambaye baada ya kuulizwa kuhusu ishu hiyo alisema anazo taarifa hizo, lakini asingependa kunukuliwa.

 

“Tunachojua sisi kuna madai ya kodi ya huyo bwana kwenye kampuni zake mbili zinaitwa JICL nafikiri, sina taarifa sahihi sana, lakini nafikiri watu wa madeni wanaweza kukusaidia,” alisema ofisa huyo na kuwaelekeza waandishi wetu zilipo ofisi hizo.

 

 

 

NDANI YA OFISI YA MADENI

Katika ofisi hiyo, Risasi Mchanganyiko lilimkosa bosi wa kitengo cha ufuatiliaji madeni baada ya kuambiwa alikuwa nje ya ofisi, lakini msaidizi wake, Josephat Mwaipaja alipatikana.

 

Baada ya kusikiliza maelezo ya kwa kina, Mwaipaja alikiri kuwa nyumba hiyo ya Javan, imefungwa na wao (TRA) kupitia wakala wao, Kampuni ya Udalali ya Yono.

 

“Jamaa anadaiwa kodi kweli na tumefanya hivyo katika hatua za awali, kuhusu kiasi cha fedha kinachodaiwa hiyo naomba muende kwa Meneja wa Mkoa, yeye ndiye mwenye kuweza kuwa na majibu,” alisema.

 

JAVAN HAPATIKANI KWA SIMU

Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Javan kupitia simu yake ya mkononi lakini haikupatikana hewani na hata katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp hakuwa hewani.

Hali ilivyo kwenye jumba hilo la Javan.

 

TUJIKUMBUSHE

Machi 25, mwaka huu katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Javan alifunga ndoa na Elvas Kulengwa na baadaye kufanyika kwa sherehe kubwa katika Ukumbi wa Akemi Golden Jubilee Towers ambako Asha Juma, aliyeolewa siku iliyofuata, naye alikuwepo katika shughuli zote za harusi hiyo.

Katika sherehe ya harusi ya pili ambayo ilifanyika Serena Hotel baada ya Asha Juma kuolewa, pia Elvas Kulengwa alionekana akiwa mwenye furaha iliyowashangaza wengi.

 

JAVAN BIDOGO NI NANI?

Javan Enock Bidogo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Javan Group Of Companies ambayo ina jumla ya kampuni tanzu tano ambazo ni Javan Investment Co Ltd, JICL Drill Limited, JICL Drill Mozambique LDA, JICL Consultant Ltd na Javan Tanzania Limited ambazo zinajishughulisha na madini ya aina mbalimbali kama dhahabu, shaba, almasi, makaa ya mawe, Nickel na mengineyo kadhaa.

Waandishi: Gladness Mallya, Ally Katalambula, Boniphace Ngumije.

 

WAANDISHI WETU, RISASI MCHANGANYIKO

INATISHA! Mzee Amwagiwa, Anyweshwa Tindikali!

Leave A Reply