The House of Favourite Newspapers

Bilionea Laizer Balaa, Ni Baada Ya Kulipwa Bil 7 za Madini

0
Saniniu Laizer

KWA Mwenyezi Mungu hakuna kukata tamaa ya maisha, kwani unaweza kulala maskini, lakini ukaamka tajiri.Hicho ndicho kilichotokea kwa baba mmoja wa Kimasai aliyetambuliwa kwa jina la Saniniu Laizer, mwenye umri wa miaka 52, mkazi wa wilayani Simanjoro Mkoa wa Manyara.

Siku chache zilizopita, Laizer alikuwa mtu wa kawaida tu, hakuwaza wala kufikiri hata kidogo kwamba angefikia hatua ya kutambulika kuwa bilionea nchini Tanzania na sasa ni maarufu kwa jina la Bilionea Laizer.


BALAA KAMA LOTE

Bilionea Laizer ni mchimbaji-madini mdogo ambaye Jumatano iliyopita, alitangazwa rasmi na Serikali ya Tanzania kuwa bilionea mpya nchini baada ya kuuza madini ya aina ya Tanzanite ambayo yana thamani ya shilingi bilioni 7.8 za Kitanzania na kusababisha balaa kama lote kwenye mitandao ya kijamii.

 

NI KAMA ALIKUWA NDOTONI

Madini hayo, moja lina kilo 9.2 likiwa na thamani ya shilingi bilioni 4.5 na la pili lina kilo 5.8 na thamani ya shilingi bilioni 3.3, hivyo kujitwalia shilingi bilioni 7.8 kama vile yupo ndotoni.Bilionea Laizer alikabidhiwa mkwanja wake huo akiwa jijini Arusha ambako pia ana vitega-uchumi vyake.Kwa mujibu wa wizara husika, madini ya uzito huo hayajawahi kupatikana katika machimbo ya Tanzanite yaliyopo Mererani wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Tanzanite ni madini yanayopatikana na kuchimbwa nchini Tanzania pekee hapa duniani.

 

SASA MIPANGO SI MATUMIZI

Kufuatia ukwasi huo aliojitwalia Bilionea Laizer, baadhi ya watu mitandaoni ambako ndiko maisha yaliko siku hizi, bila kujali wataalam wa uchumi na wasio wataalam, kila mmoja alikuwa na lake la kusema;

 

KUJENGA TOWER/MALL

Innocent Hamphrey ni mtaalam wa uchumi aliyehitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye analieleza gazeti hili kuwa, Bilionea Laizer anaweza kufanya uwekezaji mkubwa kiasi gani?Msomi huyo anasema, bilionea huyo anaweza kujenga tower (ghorofa refu) au mall (maduka kama ya Mlimani City) na miradi mingine mikubwa.“Anaweza kujenga tower moja kama zile tunazoziona Posta (Dar) au mall zenye ukubwa wa Mlimani City (Dar), Rocky City (Mwanza), Garden City (Nairobi-Kenya) au Acacia (Kampala-Uganda).


GHARAMA YA MALLU

kifuatilia thamani ya mall hizi, utakuta zinacheza kwenye kati ya shilingi bilioni 4 hadi 5, hivyo anaweza kuwa nayo.

 

USHAURI

Mtaalam huyo anamshauri Bilionea Laizer kupata washauri sahihi wenye utaalam wa masuala ya uchumi ili pesa hizo zisipotee bila habari.“Pesa ni pesa tu, zinaweza zikayeyuka kama barafu, ukigeuka huku na huku unakuta akaunti ya benki haina kitu, unashangaa.“Pia anaweza akapata washauri wazuri wakamshika mkono akanunua hisa kwenye makampuni ya uhakika kama ya madini, utalii mabenki na kilimo.“Lakini yote kwa yote, ardhi ndiyo investment (uwekezaji) wa uhakika na thamani yake inapanda kila kukicha, hivyo anaweza kujikita huko na pesa yake isipotee na badala yake iongezeke thamani,” anashauri mtaalam huyo.

MATUMIZI MILIONI 1 KWA SIKU

Mtaalam huyo anasema kuwa, kama Bilionea Laizer ataamua kutumia shilingi milioni moja kwa siku kama matumizi binafsi, kwa umri wake wa zaidi ya miaka 50, atatumia kiasi hicho hadi atakapoitwa na Mungu na chenji itabaki.

 

MAGARI YA BEI MBAYA

Jamaa huyo anasema kama Bilionea Laizer ni ‘kichaa wa magari’, basi anaweza kumiliki gari lolote la kifahari hapa duniani.Kwa kiasi hicho cha pesa, baadhi ya magari anayoweza kuyamiliki ni pamoja na; Rolls Royce la kati ya shilingi milioni 800 hadi bilioni moja au Lamborghini lenye thamani ya kati ya shilingi milioni 750 hadi bilioni moja.Mengine ni McLaren la kati ya shilingi milioni 700 hadi 900 na Bugatti Veyron la kati ya shilingi milioni 500 hadi 800.Pia anaweza kukatiza Mitaa ya Goliondoi jijini Arusha akiwa na Aston Martin la kati ya milioni 500 hadi 700, Ferrari la milioni 500 hadi 600 au Bugatti Chiron la shilingi milioni 400 hadi 600.

 

KAMA HANA MAKUU

Basi kama Bilionea Laizer hana makuu, basi atakuwa anaendeshwa kwenye Toyota Land Cruiser Exchanger la shilingi milioni 250 za Kibongo na hayo magari madogomadogo atatumia mkewe na wanaye kwenye mizunguko yao ya kila siku kama kuendea shuleni, chuoni, sokoni, kanisani, harusini, msibani au hata saluni!

 

WATU WAJIITA LAIZE

RBaadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii, wamekuwa wakijiita Laizer, wengine wakidai ni wa ukoo huo na wengine wakisema jamaa huyo ni mjomba wao.Baadhi ya mastaa kama video vixen maarufu Bongo, Anastazia Kimaro ‘Tunda’, sasa anajiita Tunda Laizer.

 

NAMBA YASAKWA

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, miongoni mwa namba za simu zinazosakwa zaidi kwa sasa, ni namba ya Bilionea Laizer huku zikifunguliwa akaunti nyingi feki zenye jina hilo kwenye mitandao ya kijamii.

 

HUYU HAPA BILIONEA LAIZER MWENYEWE

Mara baada ya kutangazwa kuwa bilionea mpya nchini, Laizer alikuwa na haya ya kusema juu ya atazifanyia nini pesa hizo?“Kwanza nimshukuru Mungu kwa sababu hii pesa ni nyingi. Ni pesa ambayo itatusaidia sisi kama familia, Serikali na jamii inayonizunguka.“Pili nina mpango wa kujenga shule kwa ajili ya watoto wangu na jamii kwa ujumla.“Pia nina matarajio ya kujenga mall Arusha. Kwa hiyo, nimefurahi sana kupata pesa hii”.

 

SERIKALI SASA INA UAMINIFU

“Nimepata faraja kubwa sana kuona Serikali yetu sasa ina uaminifu mkubwa. Kwanza nashukuru kwa Rais Magufuli kunitambua, nina furaha ya ajabu sana, moyoni najisikia vizuri sana.“Niseme tu kwamba, nilikuwa ninaishi maisha ya kawaida nikiwa mchimbaji mdogo, nitaendelea kuishi hivyohivyo kwa kukaa na watu na kutafuta maendeleo, nitaishi simpo tu, naamini baada ya muda nitapata jiwe (madini) lingine zaidi ya hayo.“Mimi kwenye maisha yangu, namuamini sana mtu mtaalam, kwa hiyo nasikiliza sana wataalam wanasemaje kwa sababu ukweli nina kiu ya kufanikiwa kwenye biashara.

 

KUHUSU KUONGEZA MKE

“Hapana, najua Rais wangu alikuwa anatania tu, namjua ni mtu mzuri anapenda utani, lakini mke wangu amefurahi sana na familia kwa ujumla,” anamalizia Bilionea Laizer.

Leave A Reply