Bilionea Saidi Lugumi, “Sibagui Dini Zao, Mungu ndiye Amenibariki Kuwalea Watoto Hawa” – Video
Bilionea Saidi Lugumi amesema kwa sasa kuna watoto yatima zaidi ya 800 kutoka maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam ambao anawahudumia kwa kila kitu ikiwemo chakula, mavazi, malazi, elimu, afya nk, na hiyo inatokana na wito alionao kutoka kwa Mwenyezi Mungu na si vinginevyo
Lugumi ameeleza hayo mbele ya wanahabari leo, Jumatano Desemba 25.2024 alipokutana na watoto hao mtaa wa Msufini, wilaya ya Kinondoni kwa ajili ya kushirikinao dua na kisomo maalum sambamba na kushirikinao chakula cha pamoja alichokiandaa kwa ajili yao
Sambamba na hilo, katika kuboresha makazi yao Lugumi amesema kwa sasa anajenga majengo sita (6) ya ghorofa huku malengo yakiwa ni kujenga ghorofa nane (8) kwa ajili ya watoto hao, kwenye maeneo tofauti ya jiji hilo, ambapo jengo moja kati ya hayo linajengwa eneo hilo la Msufini
“Hii ni nyumba yao (jengo la ghorofa), nyumba kama hizi ziko sita (6) lakini tumeanzia hapa kwa sababu nyumba hii iko mbioni kumalizika, chakula tutakula na wao hapa, na wenyewe wameweza kuwa na furaha kuona sehemu yao, kila kituo kinatarajiwa hakitazidi kukaa watoto 100, unaona nyumba kama hii ni watoto 100 tu na kwa namna Mungu anavyonijaalia nitazidi kuongeza, kwa sasa tumepanga nyumba kama tatu na nyingine tumenunua lakini bado hazitoshi”